*Aston Villa wawakimbiza uwanja mzima
*Pengo pointi 12 larudi kwa Man United
Mabingwa wa England, Manchester City wametolewa jasho na Aston Villa, lakini wakapata pointi tatu walizozifuata Birmingham.
Ilikuwa heka heka na mtafutano tangu kipindi cha kwanza, mabingwa hao wanaishika nafasi ya pili wakitafuta kupunguza pengo la pointi 15 kati yao na Manchester United wanaoongoza ligi.
Aston Villa kwa upande wao, walikuwa wakitafuta kuepuka kubaki kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja.
Kocha Paul Lambert alikiona kiti chake cha moto, akawa akihaha kulia na kushoto kutoa maelekezo kwa wachezaji wake, lakini bahati haikuwa yao.
Bao pekee la Carlos Tevez la dakika ya 45 lilitosha kuwazamisha Villa dimbani Villa Park, lakini ni dhahiri mabingwa watetezi nao wana safari ndefu.
Bao la City lilipatikana baada ya beki wa Villa, Ciaran Clark kushindwa kusafisha mpira eneo lao, akatokea Edin Dzeko aliyempokonya.
Dzeko aliyeingia badala ya Jack Rodwell aliyeumia, aliingia eneo la penati, akampasia Tevez aliyemlamba chenga kipa Brad Guzan na kutikisa nyavu.
Tevez alianza kama mpachika mabao pekee Jumatatu hii, baada ya Sergio Aguero kuumia goti wakati wa mazoezi kwa ajili ya mechi hii.
Kwa mechi 11 zilizobaki kwa timu zote za Ligi Kuu ya England (EPL, huenda itakuwa kama fainali, hasa kwa zinazowania ubingwa, ushiriki Ulaya na zinazokwepa kushuka daraja.
Matokeo hayo yameiachia City pengo la pointi 12 dhidi ya United, wakati Villa wanakuwa wa 18, kwa pointi 24, moja zaidi ya Reading na nne kuliko Queen Park Rangers (QPR) wanaokumbana nao mechi ijayo.
City walikaribia kufunga bao la pili, pale Yaya Toure alipogonga mwamba wa goli na mpira kurudi uwanjani, Mboznia Dzeko akaweka kimiani, lakini kibendera kilikuwa juu kwamba alikwishaotea.
Comments
Loading…