Manchester City wamepata ushindi kwa tabu dhidi ya Bournemouth na
kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England
(EPL).
Wakicheza kwenye dimba la Vitality, Man City wanaofundishwa na Pep
Guardiola kama kawaida mshambuliaji wa kati aliyekuwa namba moja,
Sergio Aguero alianzishwa benchi.
Hata hivyo, fursa yake ilikuja dakika 14 tu tangu mchezo kuanza
kutokana na kuumia kwa mbadala wake, Gabriel Jesus.
Baada ya nusu saa mchezoni, Man City walipata bao kupitia kwa Raheem
Sterling, baada ya kuwa amekataliwa mara mbili na kipa mahiri Artur
Boruc. Wenyeji walitupia mpira kwenye wavu lakini wakakataliwa, kwani
mwamuzi aliamua kwamba Joshua King alikuwa amevuta jezi ya John Stones
wakati akipanda kufunga.
City walikuwa na kipa namba mbili Willy Caballero badala ya Claudio
Bravo aliyesajiliwa na Guardiola kutoka Barcelona na alifanya kazi ya
ziada kumzuia Harry Arter kufunga, muda mfupi kabla ya Tyrone Mings
kujifunga kutokana na shinikizo la Aguero.
Sasa City wapo pointi nane nyuma ya vinara Chelsea wenye ponti 60 na
watakabiliana nao Stamford Bridge Aprili 5. Msimu wa 2011/12 walikuwa
hivi nyuma ya Manchester United mechi sita tu kabla ya ligi kumalizika
na wakaja kuchukua ubingwa.
Safari hii wana mechi 13 bado, na bosi wa zamani wa Barcelona na
Bayern Munich – Guardiola, anataka kuchukua mataji sba katika misimu
nane.
City wamewashusha Tottenham Hotspur hadi nafasi ya tatu wakiwa na
pointi 50 na wikiendi walifungwa 2-0 na Liverpool wakati Arsenal
wameteremshwa hadi nafasi ya nne na pointi 50 kadhalika.
Arsenal walishinda 2-0 dhidi ya Hull wikiendi lakini wameathiriwa na
kupoteza mechi dhidi ya Chelsea na Watford siku zilizopita.
Liverpool nao wameshushwa hadi nafasi ya tano wakiwa na pointi zao 49
wakati kama kawaida, Manchester United wamebaki katika nafasi yao ya
sita na pointi 48.
Wengine wote wamebaki kwenye nafasi zao bila kubadilika, ikiwa ni
pamoja na Sunderland na Crystal Palace kuwa mkiani kwa pointi zao 19
na Hull wakiwa nazo 20 kwenye nafasi ya 18, Middlesbrough wakiwa nazo
22, Swansea 24 na Bournemouth 26.