in

Makali ya Simba haya hapa na wembe wa Yanga Ligi Kuu 

Yanga FC

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania umeanza. Macho na masikio yatakuwa kwa timu za  Yanga,Simba,Azam ambazo zinabariwa kunyakua taji la Ligi kuu. Lakini idadi kubwa ya  washabiki wanazitazama Simba na Yanga kwa jicho la tatu na ndizo ambazo zinachochea mvuto  wa Ligi Kuu.  

Ni timu mbili ambazo ni kioo cha soka la Bongo. Simba na Yanga zimeanza Ligi Kuu msimu  mpya kwa namna tofauti. Yanga waliibanjua Kagera Sugar, kabla ya kuvaana na Geita Gold  wikiendi iliyopita. Simba walianza mkoani Mara kwa kupepetana na Biashara United na kutoka  suluhu, kabla ya kuitandika Dodoma Jiji wikiendi iliyopita. 

TOFAUTI ZAO 

Katika michezo yao miwili hadi sasa Simba wamekuwa walewale, wanacheza pasi fupi fupi,  kuandaa mashambulizi kutoka nyuma, kwenda langoni mwa adui. Kwa lakini kwa Yanga  wamekuwa mahiri katika maeneo ya winga na mabeki wa pembeni.  

Eneo la beki wa kati linaonekana kuwa imara zaidi huku mabeki wake wakiwa na umri mdogo.  Dickson Job na Bakari Mwamyeto wanaongoza jahazi la Yanga. Pia mabeki wao wa pembeni  kulia Djuma Shaban, beki wa kushoto Kibwana Shomari na winga wa kulia Jesus Moloko na  kushoto Farid Mussa wameanza msimu kwa kuzisumbua safu za ulinzi.  

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ina Yacouba Sogne, Herieter Makambo, Yusuf Athuman, Ditram  Nchimbi na Foston Mayele. Ni uamuzi wa kocha Nasredine Nabi kuoanga mshambuliaji wa  kuanza naye. 

Kwa Simba wameanza msimu wakikabiliwa na majeruhi wengi, Sadio Kanoute,Shomari  Kapombe,Ousamane Sakho,Joash Onyango,Thadeo Lwanga na Kennedy Juma. Hii inampa  wakati mgumu kocha wao Didier Gomes kupanga kikosi cha kwanza. Katika michezo miwili  Simba wamepata pointi nne.  

Tofauti za timu hizo mbili ni kwamba kwamba Simba wanacheza kwa falsafa yao, lakini Yanga  bado hawaonekani kucheza kitimu kama walivyo wapinzani wake. Yanga wana ukuta  mgumu,kiungo kigumu na safu hodari ya ushambuliaji lakini ingali haina kasi na muunganiko  mahususi katika mbinu zao. 

MASTAA WAO 

Yanga wana viungo wawili wapya Yannick bangala na Khalid Aucho. Halafu wa golikipa  mgumu na akili nyingi Djigui Diarra, kisha wana miguu ya kupachika mabao ya kutosha pale  mbele iwe kwa mfumo wa kupanga washambuliaji wawili au mmoja lakini  Makambo,Mayele,Sogne,Athuman na Nchimbi wana uwezo wa kupachika mabao ya kutosha.

Simba wana kiungo hodari Sadio Kanuote na mawinga wawili hatari Peter Banda na Duncan  Nyoni wote kutoka nchini Malawi. Bado wana miguu yao yenye mabao ya kutosha kutoka kwa  nahodha John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere. 

Mastaa wa timu hizo mbili wanacheza kusaka ushindi, lakini kwa kiasi fulani Simba wanacheza  mpira wao wa kutafuta ushindi huku wakionesha burudani. Yanga wameleta shughuli pevu  katika mechi zao mbili. 

MATARAJIO KWA VIPAJI VIPYA 

Simba wamesajili nyota wapya Peter Banda, Duncan Nyoni raia wa Malawi, na wengine Sadio  Kanoute,Pape Osmane Sakho kutoka Senegal, Yusuf Mhilu, Jimmy Mwandike. Mashabiki  wanataka kuona vipai vipya vikiziba mapengo ya Cletous Chama na Luis Miquissone, wakati  Yanga hawataki kukumbuka ukame wa mabao wa Ditram Nchimbi na Michael Sarpong.  

Washambuliaji wa Yanga wana kazi ya kufanya msimu huu, sawa na wachezaji wapya wa  Simba ambao wanatarajiwa kuchukua nafasi za Chama na Miquissone. Matarajio hayo ndiyo  yataamua kuwa wamefanikiwa au hawajafnikiwa. Matarajio makubwa waliyonayo mashabiki wa  pande zote mbili ndiyo presha inayowakabili pia wachezaji wao. 

WALINZI NA WAFUMANIA NYAVU 

Ili timu iweze kuchukua ubingwa inatakiwa kuruhusu mabao machache kuingia katika lao. Pia ni  lazima timu iweze kupachika mabao mengi ya ushindi ili pointi tatu zipatikane.  

Ushindani uliopo katika safu ya ushambuliaji Simba ndiyo itakuwa chachu ya kutetea ubingwa  wao. John Bocco,Chriss Mugalu,Meddie Kagere watakuwa na jukumu la kupachika mabao ya  kutosha ili kuipa nafasi Simba kutetea ubingwa wao. Ili kazi za washambuliaji ziwe rahisi  inatakiwa mawinga wao Yusuf Mhilu,Peter Banda na Duncan Nyoni watengeneze mabao. 

Yacouba Sogne,Herieter Makambo,Yusf Athuman,Fiston Mayele na Ditram Nchimbi  wanatakiwa kupachika mabao ya kutosha kuipa ubingwa Yanga kwa mara kwanza baada ya  kuukosa kwa miaka minne mfululizo. Ili washambuliaji wa Yanga wafanye kazi kwa ufanisi ni  lazima mawinga wao Farid Mussa,Deus Kaseke, Jesus Moloko, wazalishe nafasi nyingi za  magoli. 

UKUTA WA KIUNGO 

Khalid Aucho, Yannick Bangala, Tonombe Mukoko watakuwa na kazi ya kumlinda Feisal  Salum ili afanye kazi yake kwa ufanisi. Viungo hao wakabaji watakuwa na jukumu kujenga ukuta wa kiungo ambao hautakuwa rahisi kuwaruhusu wapinzani kuwakaribia mabeki wao. 

Taddeo Lwanga,Sadio Kanoute,Jonas Mkude,Muzamiru Yassin, watakuwa na kazi kubwa ya  kuijenga ukuta wa timu na kuhakikisha Rarry Bwalya anafanya kazi yake kwa ufanisi kwa  kuzalisha nafasi za kutosha za mabao.

GOLINI KUNA WAGUMU 

Aishi manula ni glikipa namba moja nchini Tanzania. huyu amedumu kikosi kwa muda mrefu  tangu alipohamia akitokea Azam FC miaka minne iliyopita. Kwa mantiki hiyo eneo la golikipa  lina mtu imara mwenye kila sifa za kuwa mlindamlango hodari katika soka la kisasa Tanzania.  

Yanga wamesajili golikipa mpya huyo raia wa Mali. Djigui Diarra ni bonge la golikipa. Uwezo  wake langni si wa kutiliwa shaka. Silaha ya tatu ni uwezo wa golikipa Djigui Diarra ambaye  anacheza kama makipa wa kisasa. Djigui anaweza mkubwa kupiga pasi kuwafikia walengwa ili  kuanzisha mashambulizi, anacheza kama sentahafu ikiwemo kuosha hatari langoni mwake.  

UAMUZI WA MBINU 

Kwa Simba mfumo wa 4-2-3-1 au 3-2-4-1 ndiyo njia yao ya kupata mafanikio. Simba wanao  viungo wann wakabaji, Taddeo Lwanga,Jonas Mkude,Muzamiru Yassin na Sadio Kanoute,  ambao mwalimu wao Didier Gomes ataamua nani aanze kikosi cha kwanza. 

Yanga wanaonekana kujikita katika mfuo 4-2-3-1 au 4-2-1-3-1 na 4-5-1. Mifumo hii kutokana na  aina ya viungo na washambuliaji walionao. Yanga waanza na viungo wakabaji wawili Yannick  Bangala,Zawadi Mauya,Khalid Aucho ua Tonombe Mukoko. Utakuwa uamuzi wa kocha  mwenyewe nani aanze mchezo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Tanzanian Volleyball sadly on verge of Death

Taifa Stars

Taifa Stars kiwango bora bila ushindi ni kilio