*Chelsea wawapiga Everton 6-3
Rekodi nyingine imeandikwa, kwa Everton waliowakaribisha Chelsea kutunguana mabao kiasi cha kufikisha tisa, wenyeji wakilala kwa 6-3, ikiwa ni rekodi ya pamoja ya saba kwa mabao mengi kwenye mechi moja.
Chelsea sasa wameshinda mechi zao zote tatu za Ligi Kuu ya England (EPL) na mchezaji wake, Diego Costa akifunga mabao mawili Jumamosi hii na kufikisha jumla ya manne, kwani kwenye mechi mbili zilizotangulia alifunga moja moja.
Kadhalika Samuel Eto’o akicheza dhidi ya Chelsea, klabu yake ya zamani, alifanikiwa kuwatungua bao moja, lakini furaha haikukamilika kwa sababu matajiri hao wa London waliondoka na pointi zote, tofauti na wakati kama huu msimu uliopita ambapo Everton walishinda 1-0.
Costa ambaye Chelsea walikuwa wanadai ameumia na huenda asingecheza, alifunga bao la kwanza sekunde ya 35 baada ya kuwatoka wachezaji wa Everton. Kuna madai kwamba Jose Mourinho alidai ameumia ili asiitwe kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Hispania, lakini akaitwa.
Muda dakika mbili tu baada ya bao hilo, Branislav Ivanovic aliyeonekana kuwa ameotea alifunga bao la pili na muda mfupi baadaye nusura Everton wabaki 10, kwani kipa wao, Tim Howard alidaka mpira nje ya eneo lake, lakini waamuzi wakakaa kimya.
Katika dakika ya 30 Kevin Mirallas alifunga bao la kwanza kutokana na pasi ya Seamus Coleman lakini dakika saba tu baadaye Everton walipigwa bao la tatu, ambapo mpira wa Eden Hazard ulimgonga Coleman, ukampita Howard na kujaa wavuni.
Steven Naismith alipunguza deni kwa kufunga la pili dakika mbili baadaye, lakini Chelsea wakajibu kupitia kwa Nemanja Matic dakika tano tu baada ya hapo, ubao ukasomeka 4-2. Dakika mbili tu baadaye Eto’o aliwaliza Chelsea kwa bao lake dakika ya 76, lakini Ramires naye akafunga dakika ya 77 na kufanya mabao kuwa 5-3.
Pilika ziliendelea, timu zote zikionekana kuwa nzuri kwenye ushambuliaji lakini dhaifu katika ama beki au makipa, na alikuwa Costa aliyemalizia kazi kwa kufunga bao la sita dakika ya 90 kutokana na kosa la beki Muhamed Besic.
Wakati Mourinho ameeleza kutofurahishwa na mizania ya timu yake kwa kukubali kufungwa mabao matatu, kocha Roberto Martinez wa Everton alilalamikia wachezaji wake kwa ulinzi mbovu. Wiki iliyopita waliongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal, lakini kipindi cha pili wakaruhusu yote kurudishwa, wakaishia kutoka 2-2 na sasa wana pointi tatu tu kutokana na mechi tatu, wakishinda moja, sare moja na kupoteza moja.
Mechi nyingine zilizokuwa na mabao mengi siku zilizopita ni Portsmouth 7-4 Reading (2007), Tottenham 6-4 Reading (2007), Tottenham 9-1 Wigan Athletic (2009), Manchester United 8-2 Arsenal (2011), Arsenal 7-3 Newcastle (2012) na West Bromwich Albion 5-5 Manchester United (2013). Pamekuwapo mechi nyingine 12 katika EPL zilizozaa mabao tisa kama haya ya Jumamosi hii.
Comments
Loading…