Angalau Brendan Rodgers anaweza kupumua vyema, baada ya Liverpool kupata ushindi wake wa kwanza kwenye ligi kuu.
Kocha huyo mpya aliyeanza kazi Anfield msimu huu,imebidi asubiri hadi mzunguko wa sita kushinda, baada ya timu kuanza msimu vibaya kuliko ilivyopata kutokea katika nusu karne.
Rodgers alikuwa mtu mwenye furaha, baada ya vijana wake wakicheza ugenini kuwaadhiri Norwich City kwa mabao 5-2, Luis Suarez akitoka na ‘hat trick’.
Stock City na Sunderland nao walifuata nyayo za Liverpool, kwani hawakuwa wameshinda mechi tangu ligi kuanza. Stoke waliwafunga Swansea 2-0 wakati Sunderland wakiwalaza Wigan 1-0.
Katika michezo minane ya Jumamosi hii, nyavu zilitikiswa mara 29.
Arsenal walianza kuugulia kipigo baada ya ulinzi mbovu kuwezesha Chelsea ambao hawakuwa na nguvu sana kuwafunga mabao 2-1.
Walicheza nyumbani mbele ya washabiki wao wengi, lakini Arsenal walibabaika kwenye beki, sababu kubwa ikionekana ni kutochezeshwa beki wa kimataifa wa Uerumani, Per Mertesacker ambaye hucheza vyema na nahodha Mdachi,Thomas Vermaelen.
Arsene Wenger ameshindwa kutoa sababu za kutomchezesha Mjerumani huyo, ambapo badala yake alimchezesha Laurent Koscielny.
Alikuwa Koscienly aliyeshindwa kumdhibiti mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres kupachika bao la kwanza baada ya mpira wa adhabu wa Juan Mata, na goli la pili alijifunga akitaka kuzuia adhabu nyingine ya Mata.
Uchezaji wa Koscienly ni ule wa kutanua uwanja, kusonga mbele kusukuma mashambulizi, tofauti na wa Mertesacker anayetulia kama beki na kuhakikisha hakuna madhara langoni mwake.
Ni kwa kuwapo kwake hapo nyuma muda wote, Vermaelen naye hutoka mara nyingi kushambulia, na kwa mechi zote walizocheza pamoja, walizuia fursa nyingi za wapinzani wao.
Gervais Lombe Yao Kouassi ‘Gervinho’ aliipatia timu yake bao la kusawazisha muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kuisha.
Gervinho aliyekuwa akihaha uwanja mzima alimalizia kazi nzuri ya winga Alex Oxlade-Chamberlain aliyechukua nafasi ya Abou Diaby aliyeumia.
Kwa ushindi wao, Chelsea ya Roberto di Matteo wamejitanua kileleni kwa pointi 16.
Tottenham Hotspurs walisafisha nyota kwa kuwafunga Manchester United nyumbani kwao mabao 3-2, ushindi wa kwanza Old Trafford tangu 1989, Garry Lineker alipowafunga.
Vijana hao wa Andre Villas-Boas walipata bao la kuongoza dakika ya pili tu ya mchezo, baada ya shuti la Jan Vertonghen kumgonga beki Jonny Evans wakati likielekea langoni.
Tottenham waliendelea kutawala mchezo na kuandika bao la pili baadaya Gareth Bale kumtoka beki anayelilia timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand na kumvukisha mpira kipa Anders Lindegaard.
United walichomoa bao moja dakika ya 51 kupitia kwa Mreno Nani, lakini dakika moja tu baadaye, Mmarekani aliyesajiliwa msimu huu Spurs, Clint Dempsey alionesha thamani yake kwa kuungisha mpira wa Bale kimiani.
Man U hawakuchoka, kwani Robin van Persie alimlisha Shinji Kagawa aliyefunga bao, na baada ya hapo Mashetani Wekundu walihangaika, wakitumia kila mbinu kutafuta bao la kusawazisha bila mafanikio.
Nusura mambo yawaendee tena vibaya matajiri wa jiji la Manchester na mabingwa watetezi, Manchester City, kama si Edin Dzeko aliyeingia karibu na mwisho wa mchezo kufunga bao la ushindi.
City walikuwa nguvu sawa na Fulgam katika uwanja wa Craven Cottage, wageni wakichukua dakika 10 tu kupata bao.
Alikuwa Mladen Petric aliyempeleka sokoni Joe Hart na kufunga nyuma yake mkwaju wa penati, baada ya Pablo Zabaleta kumwangusha John Arne Riise ndani ya eneo la hatari.
Golikipa wa Fulham, Mark Schwarzer aliokoa hatari nyingi lakoni mwake, lakini yalimshinda, dakika mbili kabla ya nusu ya kwanza kumalizika, pale Sergio Aguero alipoweka kimiani mpira wa Carlos Tevez uliotemwa.
Ushindi huo mwembamba unamwacha Roberto Mancini katikati ya kauli zake tata – kwamba waamuzi wako dhidi ya timu yake na kwamba anaamini watatetea ubingwa wao.
Everton wameendelea kuwa tishio kwenye ligi, ambapo jana wakicheza nyumbani Goodison Park waliwanyuka Southampton mabao 3-1.
Saints walianza kicheko, wakidhani wangeendeleza ushindi wa wiki iliyopita, kwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Gaston Ramirez, lakini ilikuwa sawa na kuchokoza nyuki, kwani vijana wa David Moyes walisawazisha kupitia kwa Leon Osman na Nikica Jelavic aliyefunga mabao mawili.
Everton hawajawahi kuanza vyema ligi kuu kama hivi tangu mwaka 2004, na ni kawaida yao kuanza kwa kufungwa na sare, japokuwa hufufuka mwishoni na kushinda, hasa dhidi ya vigogo.
Timu nyingine iliyokaribia kupata ushindi wa kwanza kwenye ligi kuu ni Reading, ambao walinyang’anywa tonge mdomoni na mshambuliaji mahiri wa Newcastle United, Demba Ba aliyefunga kwa mkono bao la pili la kusawazisha.
Mchezaji huyo wa kmataifa wa Senegal ndiye alisawazisha pia bao la kwanza la Reading, na kuzima furaha ya washabiki katika Uwanja wa Madjeski.
Reading walifungua pazia kwa bao la Jimmy Kebe na Jobi McAnuff.
Mchezaji mrefu wa Stoke City, Peter Crouch alifunga mabao mawili katika uwanja wa Britannia na kuwaacha hoi Swansea walioshindwa kujibu mapigo.
Steven Fletcher wa Sunderland amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi zote tano za mwanzo za msimu huu, ambapo Jumamosi hii alifunga bao pekee dhidi ya Wigan.
Kabla ya ushindi wa jana, Sunderland walikuwa wametoka sare mechi zao zote. Timu hii na Reading wapo nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya timu nyingine 18, kwa vile mechi kati yao iliahirishwa baada ya uwanja wao – Stadium of Light kujaa maji wiki kadhaa zilizopita.
Comments
Loading…