in , , ,

Liverpool watoa onyo

*Manchester City safi, Newcastle wazama

 

Liverpool wamepata ushindi mkubwa zaidi tangu kuanza msimu huu, pale walipowapa Norwich City kipigo cha mbwa mwizi.

Anfield ililipuka kwa hoihoi, nderemo na kumsifu kocha Brendan Rodgers, pale vijana wake walipopata ushindi mnono wa mabao 5-0.

Washambuliaji Luis Suarez na Daniel Sturridge walianza pamoja kwa mara ya kwanza, na kila mmoja alifunga, kuendeleza mapinduzi mekundu ya Rodgers.

Jordan Henderson alifungua karamu ya magoli, kabla ya wawili hao kufunga, kisha nahodha Steven Gerrard kabla ya Ryan Bennett wa Norwich kusindikiza langoni mwake majalo ya Raheem Sterling.

Mabingwa watetezi, Manchester City wanaowafukuzia vinara wa ligi Manchester United, walipata ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham.

Mfungaji wa mabao yote ni Mhispania David Silva, ambapo sasa limebaki pengo la pointi nne, japokuwa United Jumapili hii wapo ugenini kuumana na Tottenham Hotspurs.

Reading wamezidi kuzinduka, baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle wanaoelekea kuzidiwa na matatizo.

Walikuwa Newcastle walioanza kuliona lango la Reading kupitia kwa majeruhi aliyerejea, Yohan Cabaye, lakini Adam Le Fondre alitokea benchi na kupachika mabao mawili na Reading kuibuka kidedea.

Huu ni ushindi wa kwanza wa Reading ugenini msimu huu, ambapo pia wamejiondoa kwenye mstari wa kushuka daraja kwa tofauti ya mabao, kwani wanalingana na wawili walio chini yao kwa pointi 19.

Newcastle itabidi wajipange upya, vinginevyo wataendelea kuyumba, kwa sababu vipigo vimekuwa vya kurudia karibu kila wikiendi. Wameshampoteza mfungaji wao mahiri, Demba Ba aliyekwenda Chelsea na wamemkosa Loic Remy, aliyewakataa dakika za mwisho na kwenda Queen Park Rangers (QPR).

Swansea waliotolewa kwenye Kombe la FA na Arsenal Jumatano hii, waliamka na kuwafunga Stoke City mabao 2-0.

Walimrejeshea furaha kocha wao Mdenmark, Michael Laudrup, baada ya Jonathan De Guzman kufunga mabao mawili na Ben Davies moja katika kipindi cha pili.

Akicheza baada ya kuwekwa nje akiwa majeruhi muda mrefu, Michael Owen aliwafuta machozi washabiki wa Stoke, kwa kupachika bao kwa kichwa dakika za lala salama. Lilikuwa bao lake la kwanza msimu huu.

Sunderland walifanikiwa kukomboa mabao waliyofungwa na Wigan, kisha wakaibuka na ushindi wa mabao 3-2 ugenini.

QPR wanaokokota mkia kwa muda mrefu, walitoka sare ya bao 1-1 nyumbani kwa West Ham United.

Mshambuliaji wao mpya kutoka Marseille ya Ufaransa, Loic Remy alianza mechi ya kwanza na bao, lakini lilisawazishwa na Joe Cole, aliyerejea West Ham kutoka Liverpool Januari hii.

Kwa sare hiyo, QPR wamefikisha pointi 14, ambapo timu nne zilizo juu yao zimefungana kwa pointi 19. Kocha Harry Redknapp anajitahidi kufufua kasi na ari ya wachezaji wake, walioanza vibaya msimu kwa kufungwa mfululizo chini ya kocha Mark Hughes.

Katika mchezo wa mwisho kwa Jumamosi, Aston Villa walishindwa kupata ushindi muhimu, licha ya kuongoza kwa mabao 2-0, kwani West Bromwich Albion walijibu mashambulizi baadaye na kusawazisha.

Villa walikuwa wakijaribu kupata faraja ya ushindi baada ya kuvurunda kwenye mechi za ligi kuu na kombe la ligi kwa karibu mwezi mzima. Nyota wake,  Christian Benteke na Gabriel Agbonlahor walifunga mabao ya mapema na kutoa matumaini kwa kocha wao, ng Paul Lambert.

Hata hivyo, kocha wa West Brom, Steve Clarke naye alikuwa na kiu ya ushindi au sare, kwani alikuwa amefungwa katika mechi tatu zilizopita, hivyo aliongeza shinikizo kwa wachezaji wake kutokata tamaa.

Chris Brunt na Peter Odemwingie walifanikisha walichotumwa kwa kufunga mabao mawili, na West Brom wakaipata pointi waliyoisaka bila mafanikio muda mrefu.

Villa wamechomoka kwenye eneo la kushuka daraja, wakiwa pointi moja juu ya Wigan na Reading, wakati West Brom wamefungana kwa pointi na Arsenal na Liverpool kwa pointi 34, japokuwa Arsenal wana michezo miwili mkononi.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Unreasonable timing of AFCON

Chelsea wawararua wanyonge Arsenal