in , ,

Liverpool watadumisha tabasamu lao?

KATIKA mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, bingwa wa zamani Liverpool anatarajiwa kukutana na mtetezi Real Madrid. Liverpool wanafurahia soka lao kwa sasa wakiwa chini ya kocha mpya Arne Slot. Liverpool wapo kileleni mwa Ligi ya Mabingwa, hawashikiki na wamekuwa gumzo kati ya timu zinazofikiriwa kunyakua ubingwa. Kana kwamba haitoshi Liverpool wapo kileleni mwa Ligi Kuu England (EPL) na wamekaa hapo kwa raha zao. Wapo katika zama mpya ambazo zinasimamiwa na kocha Arne Slot. Bila shaka viongozi wa Liverpool wanafurahia uamuzi wao wa kumwajiri mwalimu huyo kuchukua nafasi ya Jurgen Klopp aliyeng’tuka. Je nini siri yao? Na upi udhaifu wao

Mchezo wa kasi

Pengine tunaweza kusema ni mwendelezo wa Gegenpressing iliyoletwa na Jurgen Klopp. Lakini Arne Slot ameongeza na mtindo wa Kiholanzi wa ‘Total Football’ kwamba wanapiga pasi nyingi kwa kasi ama kupiga mipira mirefu kwa kasi kwenda maeneo ya mawinga. Liverpool ya sasa imekuwa ikicheza kwa wingi zote mbili kwa kasi huku eneo la namba 9 likiwa halina mwenyewe. Mchezo huo umechangia Dawrin Nunez kusugua benchi mara kwa mara, na nafasi yake kuchezwa na Mohammed Salah na Lucho (Luis Diaz). Wawili hawa wamekuwa wakicheza kwa kuingia eneo la namba 9 wakitokea pembeni. Mara nyingi huingia eneo la hatari kwa kasi ya ukokotaji wa mipira ama kupokea pasi ndefu.

Benchi lenye akili

Gapko na Nunez ni wachezaji wanaoweza kuanza kikosi cha kwanza katika timu yoyote, lakini hapa Liverpool wanasugua benchi. Pamoja na kukaa kwao benchi ni aina wachezaji wanaoleta mabadiliko kwenye timu kila wanapoingizwa. Hii ina maana timu inapokuwa na wachezaji wenye sifa ya kufanya mabadiliko zaidi maana yake wanaiwezesha kuwa na machaguo mengi kulingana na mchezo. Ili kucheza na Arsenal lazima kuwe na mkakati tofauti, sawa na Man City au Chelsea n.k. Mikakati ya Liverpool imekuwa kukabiliana na wapinzani wao kwa namna tofauti, lakini msingi wao wa kwanza wa kupiga pasi ndefu umebaki kuwa uleule wa kiholanzi. Lakini mabadiliko ya wachezaji wao yana maana benchi lao lina watu wenye akili za maana kuleta mabadiliko. Katika eneo la golikipa hata akikosekana Allison Becker bado Liverpool imekuwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele. Ili timu isonge mbele lazima itengenezewe utayari wakati wowote.

Mapumziko

Arne Slot amekuwa akitoa mapumziko kwa wachezaji wake. Mbinu ya kupunguza muda wa kutumika kikosini imewesha wachezaji kuongeza nguvu na ari. Jina la Joe Gomez linaingia katika eneo la beki wa kati au pembeni. Gomez amekuwa akichukua nafasi ya Trent Alexander Arnold, ambaye anapotolewa uwanjani zikiwa zimesalia dakika 10 au 15 maana yake anapata muda wa kupumzika kisha mwingine anayeingia anapata muda wa kujiimarisha na kuwa tayari wakati wowote. Katika safu ya ulinzi wa kushoto Robinson amekuwa akipumzishwa na nafasi yake huichezwa na Tsamikas. Mabadiliko ya namna hiyo yamewafanya wachezaji wawe na utimamu na ari kwani hucheza kwa zamu au kupokezana. 

Kombinenga ya mabeki wa kati

Joel Matip ameondoka Liverpool. Jeuri ya Liverpool kumruhusu Joel Matip imetokana na uwepo wa kinda Ibrahima Kounate. Katika safu ya ulinzi Liverpool wamejitahidi kuweka wachezaji maana na ushirikiano wao umetengeneza kombinesheni nzuri. Kwa hapo nyumbani Tanzania unaweza kuwatazama Dickson Job na Ibrahim Bacca wa Yanga, wawili hao wameifanya safu ya ulinzi iwe imara zaidi. Hilo ni sawa na Ibrahima Kounate na nahodha wake Virgil van Djik wameunda kombinenga nzuri na yenye hatari klabuni hapo. Licha ya kuwa na umri wa miaka 33 sasa Virgil anaonekana kuwa na ari zaidi akishindana na kumuongoza chipukizi wake Kounate. Safu ya ulinzi imekuwa chachu ya kupunguza mabao ya kufungwa hivyo kuimarisha ari ya idara nyingine.

Safu ya kiungo

Wakati wa Jurgen Klopp Curtis Jones hakuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza. Hata hivyo alipata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Kocha wa sasa Arne Slot amegundua kitu muhimu kutoka kwa kiungo huyo. Hili ni ingizo jipya katika kikosi cha kwanza, na majukumu anayotumwa kufanya ndiyo chachu ya kucheza kikosini. Curtis Jones ana kismati cha mabao, mashuti makali, na mzuri katika kuweka uwiano wa kiungo wa ulinzi na ushambuliaji. Ni mkataji mzuri wa mipango ya adui kuelekea langoni mwao akiwa katikati ya dimba. Uchezaji wake kuanzia eneo la mstari wa katikati na mita 10 kuelekea eneo la 18 la adui ni dhahiri linamwezesha kuifanya timu hiyo iongeze shinikizo kwa wapinzani wao. Kwa maana hiyo ingizo la Curtis Jones limechangia kuimarisha Liverpool.

Je udhaifu wao uko wapi?

Timu inaposhinda inaficha siri za udhaifu wao. Liverpool wanmashinda, wapo kileleni Ligi ya Mabingwa na EPL kwahiyo kila mmoja anaona hawana udhaifu. Hata hivyo eneo la kwanza ambalo linajenga udhaifu wa Liverpool ni ushambuliaji. Kwa sababu asili ya wanaotegemewa ni mawinga wenye kasi na maarifa ya kufunga, lakini kama timu hiyo itadhibiti mianya ya kuwafikia mipira au pasi maana yake wanakwenda kupoteza nguvu kwenye kiungo.

Jambo la pili eneo la beki wa kati lina uwezo mdogo wa kukabiliana na wachezaji wanaotumia ubunifu na chenga nyingi ni rahisi kujichanganya. Kwa sababu mabeki wa kati ya Liverpool ni wale ambao wanaweza kupambana kwa nguvu za mwili,kuondoa hatari za mipira ya juu, kukabiliana na mipira ya krosi na kupiga ‘tackle’ nyingi. Hata hivyo uzoefu unaonesha Liverpool wana mabeki ambao wanapata shida kwenye uchezaji wa pasi nyingi na chenga za haraka. Unapokuwa na wachezaji kama Vini Junior, Rodrygo, Bernado Silva, Rafael Leao ama Sporting Lisbon ya Ruben Amorim na wengineo wa aina yake ni rahisi kufichua udhaifu wao. Kimsingi Virgil na Kounate hawana kasi wanapokabiliana na washambuliaji. Timu ikianza kuwakimbiza mwanzo-mwisho nina uhakika Liverpool watapoteana pale nyuma.

Golini ni eneo jingine ambalo washambuliaji wenye maarifa wanaweza kumfunga Allison au Keheller. Hawa ni makipa ambao wanafanya makosa mara kwa mara. Kwahiyo njia pekee ya kuwafunga ni pasi za haraka eneo la 18 na kubadilisha mwelekeo wa shambulizi. Kwa kawaida wanaonekana kuwa si wepesi wa maamuzi, kwani pasi za haraka kwenye 18 zinasababisha kutojua wapi mfungaji anaweza kutokea. Wapo makipa wenye uwezo wa kukisia wapi shambulizi litaelekezwa, lakini kwa Liverpool wanao wale wa kawaida licha ya umahiri wao mwingine.

Pasi ndefu na kukimbizana ni miongoni mwa silaha za Liverpool kwa sasa. Upigaji wa pasi huo mara nyingi unaelekezwa kwa Mohammed Salah au Lucho Diaz. Wawili hao wanapopokea pasi hizo wanakimbia kwa kasi kuelekea eneo la hatari. Inawezekana mpira umepigwa na kipa kisha ukamifikia mmojawapo na huingia eneo la hatari. Mbinu haiwezi kusaidia mbele ya mabeki wenye kasi na wale wanaokabiliana na wapinzani ‘mtu kwa mtu’ Eder Militao, Nathan Ake, William Saliba ni aina ya mabeki ambao wanatibua mbinu hiyo mara mchezaji anapokea mpira. Yaani Salah au Lucho akituliza huo au kabla anakuwa tayari amefikiwa na beki ambaye anavuruga au kubutua mpango. Ni rahisi mbinu ya mipira kufeli mbele ya mabeki wa aina hiyo au timu nzima kuwajibika kiuchezaji. 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Vipaji Vya Umiseta Na Umitashumta Huenda Wapi?

Tanzania Sports

Tujifunze Kuheshimu Uwekezaji Wa Vilabu Vidogo