Mchezaji mpya wa Liverpool, Christian Benteke ameanza kuipa ushindi timu yake, japokuwa bao alilofunga dhidi ya Bournemouth lilionekana kuwa na utata.
Lakini kwa vile ushindi ni ushindi tu, Liverpool wameshinda mechi zao zote mbili za awali na wanaweza kujipa moyo kwamba wamelamba dume kwa kumsajili mshambuliaji huyo wa kati kutoka Aston Villa kwa kitita cha pauni milioni 32.5.
Benteke alitikisa nyavu dakika ya 26 akiwa karibu kabisa na kipa Arthur Boruc, na utata wa bao hilo unakuja kwa sababu Philippe Countinho alikuwa ameotea waziwazi alipokuwa anajaribu kuifikia majalo ya Jordan Henderson na mwamuzi Craig Pawson akaruhusu bao.
Bournemouth watasikitika kwa bao hilo kukubaliwa, ikizingatiwa walicheza vyema na wangefurahi hata kuambulia sare, lakini sasa wamepoteza mechi zote mbili za mwanzo.
Walifunga bao la kichwa kupitia kwaTommy Elphick mapema, lakini mwamuzi akalikataa kwa madai kwamba Dejan Lovren alikuwa amechezewa rafu kabla ya bao kuingia.
Bournemouth wanafundishwa na kocha mwenye umri mdogo zaidi katika Ligi Kuu ya England, Eddie Howe na wanaonesha kwamba watakuwa wazuri kadiri ligi inavyoendelea huku kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers naye akiwa na ahueni kwani shinikizo dhidi yake linapungua.
Wageni hao wa ligi kuu walishindwa mechi ya kwanza kwa kufungwa na Aston Villa kwa bao kama la Jumatatu hii, watatakiwa kujiimarisha katika eneo la ushambuliaji, kwani ni mara chache sana kipa wa Liver, Simon Mignolet alionekana kutiwa kashikashi.
Mwamuzi wa mechi hiyo alishindwa kutumia kanuni mpya za kuotea zilizoanza kutumia mwanzoni mwa ligi hii, ambapo zinasema wazi kwamba mchezaji aliye katika eneo la kuotea ataadhibiwa ikiwa atajaribu kuugusa mpira ulio karibu naye, na ndivyo alivyofanya Coutinho.
Hata hivyo alishindwa kuupata mpira huo, ndipo Benteke akauwahi na kuutia kimiani. Mshambuliaji wa zamani wa kati wa Newcastle, Alan Shearer alieleza kusikitishwa kwake na kutozingatiwa kanuni hiyo, bao likaruhusiwa na Bournemouth wakaachwa wakiuguza kidonda chao.
Kocha Rodgers alipoulizwa juu ya kupewa bao lisilo na wageni kunyiwa bao, alidai kwamba hakuona matukio yote mawili lakini cha muhimu zaidi kwa timu ni kwamba wameshinda katika mechi waliyokwishajiaminisha kwamba ingekuwa ngumu.
Aliwapongeza wachezaji wake kwa kulinda vyema lango na kucheza vyema zaidi hata baada ya kupata bao.
Kocha wa Bournemouth, Howe, alisema ni ngumu kupokea matokeo ya jinsi hiyo lakini hawana cha kufanya.
Kwamba wanaendelea kujifunza na kupokea mambo machungu na kwamba uwezekano wa kufanikiwa bado ni mdogo, watajijenga zaidi kwa ajili ya mechi zijazo.
Alisema hakuzungumza sana na waamuzi, kwamba walikuwa na kazi ngumu lakini atajadiliana nao binafsi kwa sababu anataka kupata mrejesho juu ya maamuzi hayo.