Ligi Kuu ya England (EPL) ipo katika hatua ngumu, ambapo kwenye mzunguko wa 27 Liverpool wameshinda kwa tabu huku Tottenham Hotspur wakipigwa.
Vita ya nafasi nne za juu inaelekea kuwa ya aina yake, ambapo Liverpool wakicheza nyumbani ilibidi wafanye kazi ya ziada kuweza kuwafunga Swansea 4-3.
Haikuwa rahisi kufikia hatua hiyo, na ilibidi kusubiri hadi dakika ya 74 kwa Reds kujipatia bao la ushindi kupitia kwa Jordan Henderson ambaye pia alifunga bao jingine awali dakika ya 20.
Mabao mengine ya Liverpool yalifungwa na Daniel Sturridge mapema katika dakika ya tatu nay a 36 huku Luis Suarez akikosa fursa za kufunga.
Swansea walipata mabao yao kupitia mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jonjo Shelvey katika dakika ya 23 na Godfrey Bonny aliyefunga dakika ya 27 kabla ya kutia kambani bao kwa penati dakika ya 47 baada ya kuwa ameangushwa eneo la hatari, ambapo kipa Simon Mignolet alishindwa kuizuia.
Liverpool sasa wamefikisha mabao 70 kwenye EPL, wakiwa vinara kwa kuwavuka Manchester City waliokuwa na moto wa kufunga lakini sasa wanaelekea kudhibitiwa.
SPURS WAADHIRIWA NA NORWICH
Katika mechi ambayo wengi walidhani ingekuwa rahisi kutoa ushindi kwa Tottenham Hotspur, ilishuhudiwa Norwich City wakiwazidi wageni wao.
Kocha Chris Hughton alikuwa na furaha kubwa kutokana na ushindi wa 1-0 kwa bao la Robert Snodgrass dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza, kwani alipoteza mechi kadhaa zilizopita na kuwa katika nafasi isiyo nzuri.
Ushindi wa Norwich umetia doa kubwa kwa Spurs wanaopigania nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ili kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (ECL).
Kipa wa Norwich, John Ruddy aliyepata kuwindwa na kocha Jose Mourinho ili ahamie Chelsea alikuwa wa msaada mkubwa kwenye mchezo, kwani aliwazuia kabisa akina Emmaunel Adebayor na Nacer Chadli walipopata nafasi za kufunga kipindi cha pili.
NEWCASTLE WAWAPIGA ASTON VILLA
Newcastle wamejifariji kutokana na kukwama kupata ushindi mechi nyingi zilizopota, lakini Jumapili hii wamewapiga Aston Villa 1-0.
Lilikuwa bao la Mfaransa Loic Remy aliyesajiliwa msimu wa kiangazi kutoka Queen Park Rangers (QPR) aliyewajazia maumivu Villa.
Bao lenyewe lilifungwa dakika za mwisho za mchezo na kuwawezesha Magpies kumaliza mechi nne mfululizo pasipo ushindi.
MSIMAMO WA LIGI
Kwa matokeo ya mechi za Jumamosi na Jumapili hii, Chelsea wanaendelea kuongoza wakiwa na pointi 60 wakifuatiwa na Arsenal pointi moja pungufu na Manchester City wenye pointi 57 na mchezo mmoja mkononi. Liverpool wana pointi 56 wakifurahia nafasi ya nne.
Wanaofuata kwenye msimamo kuanzia nafasi ya tano hadi ya 17 ni Spurs, Manchester United, Everton, Newcastle, Southampton, West Ham, Hull, Swansea, Aston Villa, Norwich, Stoke, Crystal Palace na West Bromwich Albion.
Nafasi tatu za kushuka daraja kwa sasa zinashikiliwa na Sunderland wenye pointi 24, Cardiff waliojikusanyia 22 na Fulham wenye 21.
Comments
Loading…