*Chelsea wanapanda ‘mdogo mdogo’
*Mwamuzi wa akiba azimia uwanjani
Leicester wanaoongoza Ligi Kuu ya England (EPL) wamepunguzwa kasi kwa
kulazimishwa sare ya 2-2 na wagumu West Bromwich Albion, lakini kocha
wao, Claudio Ranieri amesema watapambana kuutafuta ubingwa.
Ilikuwa mechi nzuri, ambapo West Brom walitoka nyuma na kuhakikisha
wanapata pointi moja, tena wakiwa kwenye uwanja wa vinara hao wa muda
mrefu ambao hawakutarajiwa kabisa kufanya vyema, kwani walishatabiriwa
hata kushuka daraja.
Salomon Rondon alifanikiwa kumzidi maarifa Robert Huth na kuwapa West
Brom bao la kuongoza kabla ya Danny Drinkwater kusawaazisha kisha Andy
King akafunga bao lililodhaniwa lingekuwa la ushindi kwa Leicester.
Haikuwa hivyo, kwani West Brom walipata bao kupitia kwa Craig Gardner
aliyechonga vyema mpira wa adhabu ndogo.
Leicester waliendelea kutafuta ushindi, ambapo mara mbili mipira ya
wachezaji wake iligonga mtambaa wa panya. Wanabaki juu kwa tofauti ya
pointi tatu dhidi ya wanaowafuata, Tottenham Hotspur ambao wanaweza
kushika usukani wakipata ushindi Jumatano hii ugenini kwa West Ham.
Leicester wenye pointi 57 wamewaacha Arsenal umbali wa pointi sita, na
Jumatano hii Arsenal wanakipiga na Swansea. West Brom waliopoteza
mechi mbili tu kati ya 10 zilizopita wanashika nafasi ya 13 wakiwa na
pointi 36.
CHELSEA WANAPANDA ‘MDOGO MDOGO’
Chelsea wanaendelea kupata nafuu na sasa wamepanda hadi nafasi ya
nane, huku tishio la kushuka daraja chini ya Jose Mourinho likiondoka.
Wamefanya hivyo kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Norwich ugenini Carrow
Road chini ya bosi wa mpito, Guus Hiddink. Beki wa pembeni wa Chelsea,
Kenedy ndiye alifunga bao la kwanza kutoka umbali wa yadi 20 baada ya
kutiliwa mpira na Eden Hazard katika sekunde ya 39 tu, likiwa bao la
mapema zaidi katika EPL msimu huu.
Diego Costa alifunga bao la pili kuelekea nusu ya kwanza kumalizika,
katika kile kilichoonekana na wachambuzi wa mambo kwamba alikuwa
ameotea. Norwich ambao sasa wametupwa eneo la kushuka daraja hawakuwa
wazembe; walipambana ambapo mpira wa Cameron Jerome uligonga mwamba
kabla ya Nathan Redmond kufunga.
Norwich sasa wamepoteza mechi nane kati ya tisa zilizopita na kocha
wao, Alex Neil amelalamikia bao la Costa, akisema walau wangekwenda
sare. Wamevuna pointi moja tu kati ya 24 zilizokuwa mbele yao
kuzipigania.
MWAMUZI AZIMIA, MATOKEO MENGINE EPL
Katika matokeo mengine, Bournemouth wakicheza nyumbani waliwafunga
Southampton 2-0 katika mechi ambayo mwamuzi wa akiba, Kevin Friend
alizimia baada ya kujigonga kichwa kwenye chuma za eneo alikokuwa
amesimama kabla tu ya nusu ya kwanza kumalizika.
Mwamuzi huyo alitibiwa kwa muda uwanjani kabla ya kupelekwa hospitali
kwa uchunguzi na tiba zaidi. Mwamuzi wa kati, Mike Dean alisitisha kwa
muda mechi hiyo kabla ya kupuliza kipenga kuashiria kipindi cha
mapumziko na muda wa nyongeza haukuchezwa.
Kipindi cha pili kilichelewa kuanza kwa dakika tano, kwani mbadala wa
Friend alikuwa akitafutwa. Aliyechukua mikoba hiyo ni Dean Treleaven,
mwenye sifa zote za urefa lakini hajapata kuwa katika mechi ya ligi.
Ilikuwa siku nzuri kwa Bournemouth, kwani wamejiondoa kwenye eneo la
kushuka daraja kwa umbali wa point inane. Saints walipoteza nafasi
nzuri ya kufunga mapema, pale Charlie Austin alipobetua mpira kiupande
na kushindwa kufunga, hivyo wakabaki wakihangaika na watani wao hao
katika pwani ya kusini mwa England.
Bournemouth walifunga baada ya kipa Fraser Forster kuutema mpira wa
adhabu ndogo wa Matt Ritchie kisha Steve Cook akautumbukiza wavuni.
Benik Afobe aliwahakikishia ushindi The Cherries kwa kufunga akipokea
tena mpira wa adhabu ndogo wa Ritchie. Hii ni mara ya kwanza kwa
Bournemouth kuwafunga Saints katika ligi tangu 1958.
Sunderland na Crystal Palace walikwenda sare ya 2-2 na kuwafanya
Sunderland kuondoka kwenye eneo la kushuka daraja, japo kwa tofauti ya
mabao na Norwich na Newcastle, kwani wote wana pointi24 huku Aston
Villa wanaoshika mkia wakiwa na pointi 16.
Fabio Borini ndiye aliwanasua Sunderland kwenye matatizo baada ya
kusawazisha dakika ya 90. Dame N’Doye’s ndiye alianza kufunga bao kwa
Sunderland, lakini Connor Wickham akafunga mabao mawili katika kipindi
cha dakika mbili. Wangeshinda, Palace wangekuwa wamepata ushindi wa
kwanza katika mechi 11, lakini Borini aliyeingizwa kipindi cha pili na
kocha Sam Allardyce alifanya kweli kwa kucheka na nyavu, akionekana
kuwa ‘super sub’.