in , , ,

Leicester kama wanamsukuma mlevi

*Waendelea kupaa, Arsenal wamefufukia Everton

*Chelsea wakachomoa dakika za mwisho kwa tuta

*Man City vs Man United mtoto hatumwi dukani leo

Leicester wameendelea kuruka vihunzi katika kusaka ubingwa wa England,
ambapo katika mechi dhidi ya Crystal Palace walipata ushindi wa 1-0 na
kuacha vumbi kwa wanaowakimbilia na kibindoni wamefikisha pointi 66.

Bao la Riyad Mahrez lilitosha kuwapaisha umbali wa pointi nane zaidi
ya wanaoshika nafasi ya pili – Tottenham Hotspur na 11 zaidi ya
wanaofuata – Arsenal, japokuwa Leicester wamecheza mechi moja zaidi.

Vinara hao wanaofundishwa na Claudio Ranieri wamekuwa kana kwamba
wanamsukuma mlevi kwa jinsi wanavyoserereka kwa ushindi wa mara kwa
mara, na Mtaliano huyo baada ya mechi hiyo aliwaruhusu vijana waende
majumbani mwao wakaburudike.

Mahrez alishindwa kufunga bao la mapema baada ya kupatia majalo na
mfungaji mwingine matata, Jamie Vardy, lakini akasahihisha makosa
yake. Damien Delaney alikaribia kuwsawazishia Palace dakika za
majeruhi, lakini mkwaju wake ukagonga mwamba.

Palace wapo katika hali mbaya, kwani hawajapata kushinda tangu Desemba
19 mwaka jana kwenye mechi za Ligi Kuu ya England (EPL); wakishika
nafasi ya 16 na pointi zao 33. Vijana hao wa Alan Pardew walioanza
vyema ligi wanaweza kutumbukia kwenye eneo la kushuka daraja
wasipokaza mkanda, kwani wanaowafuata wanazo pointi 28, wengine 25 na
wengine 24.

Ranieri ameongeza idadi ya pointi anazotaka ili watwae ubingwa,
akisema anahitaji wafikishe 84 na taji litakuwa lao, kwani hata Spurs
wakishinda mechi zote zilizobaki wataishia pointi 82.

ARSENAL WAENDA KUFUFUKIA KWA EVERTON
ARSENAL WAENDA KUFUFUKIA KWA EVERTON

Arsenal wamejibu vyema vipigo kwenye mashindano mawili tofauti kwa
ushindi katika EPL, walipokwenda kuwachakaza Everton kwao Goodison
Park kwa mabao 2-0. Arsenal walitoka kufungwa na kuvuliwa Kombe la FA
na kutolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Kwa ushindi huo, Arsenal sasa wamefikisha pointi 55 na kocha wao,
Arsene Wenger amefurahishwa, akisema kwamba vijana wake wamepasi
jaribio gumu la kisaikolojia. Ilikuwa mechi nzuri kwa Washika Bunduki
wa London, wakitumia silaha tofauti kidogo.

Danny Welbeck aliyetoka kwenye majeruhi siku si nyingi aliwaamsha
vitini washabiki waliosafiri kutoka London dakika ya saba tu, baada ya
kutiliwa pasi nzuri na Alexis Sanchez, akamzunguka kipa Joel Robles na
kufunga bao lake la nne kwa msimu huu.

Dakika tatu kabla ya mapumziko, kijana Alex Iwobi aliyecheza kwa mara
ya kwanza EPL aliifungia timu yake bao la kwanza. Huu ulikuwa ushindi
wa kwanza kwa Arsenal katika mechi nne za EPL, na walitawala kabisa
mchezo huo.

Chelsea wakachomoa dakika za mwisho kwa tuta
Chelsea wakachomoa dakika za mwisho kwa tuta

Everton wanaofundishwa na Roberto Martinez, na waliotoka kuwatupa
Chelsea nje ya Kombe la FA walionekana dhaifu, ambapo ni mashuti
mawili tu yalilenga goli na katika mechi tano zilizopita za mashindano
haya, wamepoteza nne. Wameketi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi
wakiwa na pointi 38 sawa na wanaoshika nafasi ya 13 – Bournemouth.

Iwobi (19), raia wa Nigeria alifurahia kupangwa, lakini zaidi kufunga
bao, kiungo huyo akisema kwamba ndoto zake zimeanza kutimia. Amepanda
kuanzia akademia ya Arsenal ya Hale End na alicheza kikosi cha kwanza
kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana kwenye Kombe la Ligi ambapo
walikung’utwa 3-0 na Sheffield.

Japokuwa alizaliwa Lagos, Iwobi amecheza kwa timu za vijana za England
kabla ya kuamua kuchezea Nigeria na ameshaibukia kwenye kikosi cha
wakubwa cha Super Eagles, akicheza huko mara mbili. Mchezaji wa zamani
wa Nigeria, Jay-Jay Okocha ni mjomba wake.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Man City mdomoni mwa PSG

Tanzania Sports

Mourinho ndani Man U?