in , , ,

Kwaheri Reading, QPR


*Arsenal, Man U zakomaliana
*Vita yanoga nafasi nne za juu

Kuagana ni kuchungu heri ingekuwa kesho – lakini ukweli huo haukutaka kusubiri kwa klabu za Reading na Queen Park Rangers (QPR), zilizokuwa kama mgonjwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Wawili hao walikuwa na majaliwa yao mikononi mwao, lakini ama walicheza karata zao ndivyo sivyo katika mechi za tangu mwanzo wa msimu au kulitokea tatizo lililo nje ya uwezo wao, lakini hatima yao ni moja – kushuka daraja.
Nigel Adkins na Hary Redknapp waliishia kupeana mikono na tabasamu baada ya mechi dhidi yao iliyoisha kwa suluhu katika uwanja wa Madjeski, Reading, lakini mioyo yao ilijaa huzuni.
Adkins ameshuhudia kuteremshwa daraja Reading baada ya kufukuzwa kazi Southampton wenye kila dalili za kubaki Ligi Kuu ya England (EPL), huku Redknapp anayekubali kuwa na timu katika daraja la chini alifutwa kazi Tottenham Hotspurs msimu uliopita japokuwa aliwapeleka vyema wachezaji wake.
Ilikuwa klabu ambayo ingefungwa leo ingeshuka daraja bila maulizo, lakini kwa suluhu yao, wamejihukumu wenyewe, wakiacha furaha kidogo kwa walio juu yao, maana badala ya mchujo wa timu mbili sasa utabaki wa timu moja.
Reading na QPR zimemaliza ligi zikiwa mkiani, juu yao wakiwapo Wigan wanaoendelea kupambana, na wamekuwa na kawaida ya kuokoka katika mechi tatu hadi moja ya mwisho wa ligi, na bado wapo chini ya kocha Roberto Martinez, ambapo Jumamosi hii walikwenda sare na Tottenham Hotspurs.
Katika mechi nyingine, Manchester United walitandaziwa gwaride la heshima la ubingwa Emirates, lakini hawakuruhusiwa kuwafunga Arsenal, hivyo kuishia sare ya 1-1, baada ya bao la The Wallcot na tuta la nahodha wa zamani wa The Gunners, Robin van Persie.
Chelsea walio katika mbio za kutafuta nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, walifanikiwa kuwachakaza Swansea 2-0, hivyo kuwashusha Arsenal nafasi moja.
Ukiacha Manchester United waliokwishatwaa kombe, nafasi ya pili inashikwa na Manchester City, ya tatu Chelsea na ya nne ni Arsenal, huku ya tano wakiwapo Spurs ambao na Chelsea wana mchezo mmoja mkononi zaidi ya Arsenal.
Mtihani wa nafasi hizo mbili kati ya nne za juu, umewekwa juu ya kilinge cha mechi nne kwa Chelsea na Spurs na tatu kwa Arsenal, ambapo The Gunners watakabiliana na QPR, Wigan na Newcastle.
Chelsea walio bado katika harakati za kuwania taji la Kombe la Europa wanakabiliwa na mechi dhidi ya Manchester United, Spurs, Aston Villa wanaokwepa kushuka daraja na Everton wanaonyemelea nafasi ya nne.
Ama kwa upande wa vijana wa Andre Villas-Boas, mechi zao nne zilizobaki ni dhidi ya Southampton, Chelsea, Stoke City na Sunderland ya Paolo Di Canio.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Prisons retain union Volleyball title

Aston Villa wawaachia Wigan zigo