in , ,

Kuna mgogoro unapikwa Chelsea

*TANGU kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya England (EPL) 2016/17, imekuwapo aina ya sintofahamu klabuni Chelsea*

Licha ya kwamba walitwaa ubingwa chini ya kocha mpya, Antonio Conte aliyepewa sifa, akisema kwamba alikuwa ndio tu anaianza kazi kubwa, mambo yameonekana kwenda ndivyo sivyo.

Pamekuwapo na kutokukubaliana au kutofautiana miongoni mwa ‘wazito’ wa Stamford Bridge juu ya kipi kifanyike, lakini pia kutokana na uhusiano mbaya unaoonekana kujengeka kati ya ofisa mmoja na mwingine, au kocha na mchezaji.

Baada ya sherehe kubwa za kutwaa ubingwa na kama kawaida kuzunguka ndani ya basi la wazi mitaani hapa kusherehekea, walipigwa butwaa baada ya kufungwa na Arsenal waliochukuliwa vibonde na hii ilikuwa ni kwenye fainali ya Kombe la FA.

Wachezaji walipotawanyika kwenda likizo na wengine kwenye mashindano tofauti, mshambuliaji imara na mfungaji mabao wao namba moja, Diego Costa, akarusha kibomu nyuma, akianika siri aliyokuwa ameambiwa na kocha Conte.

Mhispania huyo aliyezaliwa Brazil akasema kwamba aliambiwa na bosi kupitia ujumbe mfupo wa maandishi kwamba hakuwa kwenye mipango yake katika klabu hiyo kwa msimu ambao ungefuata, yaani msimu huu wa 2017/18. Costa akaweka bayana kwamba hakuwa anatakiwa tena hapo, lakini wadau walidhani suala hilo lingemalizika.

Tofauti kabisa na hivyo, utata umebaki; Costa amebaki huko alikozaliwa Brazil akiendelea na mazoezi na kushinikiza auzwe ili aondokane na Chelsea, akiapa kutorudi tena kucheza Stamford Bridge. Hapa London Conte alipoulizwa juu ya hilo alitaka waandishi waachane na masuala ya mchezaji huyo maana yamepita.

Diego Costa

Hata hivyo, msemaji wa klabu alitokea kunyoosha lugha, akisema kwamba Costa ni mchezaji wao halali bado na walikuwa wakimtaka aripoti kazini kwa ajili ya kuendelea na mkataba wake. Sasa hapo inaonekana kocha anakwenda kinyume na baadhi ya viongozi hapo, na haijulikani hatima ya Costa itakuwaje au nani ataiamua.

Inaelezwa sasa kwamba mmiliki wa klabu, Roman Abramovich amechoshwa na danadala za klabuni hapo, malalamiko yanayotolewa na huyu na yule na atachukua hatua muda wowote kuanzia sasa kuweka mambo yaende anavyotaka. Conte alipokwenda likizo aliacha maagizo kwamba mchezaji wao wa zamani, Romelu Lukaku anunuliwe hata kama ni kwa pauni milioni 70 au zaidi.

Ajabu ni kwamba kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho, ambaye sasa yupo Manchester United, alizunguka na kumchukua mchezaji huyo ambaye sasa anatamba vilivyo kwenye kikosi hicho, ambacho katika mechi mbili tu kimeshafunga mabao manane, kuchukua pointi sita za haraka na hawajafungwa.

Huku Chelsea walianza kwa kufungwa na klabu ndogo tu ya Burnley, na kuacha vichwa vikiwauma wadau ambao wanakumbuka bado kufungwa uwanjani Wembley kwa mara ya pili na Arsenal – kwenye ufunguzi wa pazia la msimu, yaani fainali ya Ngao uya Jamii.

Habari za ndani zinasema kwamba hata wachezaji watatu hivi waliosajiliwa klabuni hapo wameletwa kwa fedha toka mfukoni mwa Abramovich moja kwa moja. Inadaiwa pia hataki kusikia malalamiko wala kocha huyo akiwachagiza viongozi wengine hapo.

José Mourinho na Roman Abramovich, hawa hawakuwahi kuwa marafiki

Bilionea huyo wa Urusi alitoa fedha zilizowasajili Alvaro Morata kwenye ushambuliaji, kiungo Tiemue Bakayoko na beki Antonio Rudiger. Hata hivyo kuna sintofahamu kwamba ni nani hasa alishauri au kukubali maombi ya kuuzwa kwa mchezaji muhimu sana wa kiungo, Nemanja Matic kwa Man United ambaye huko anang’aa hasa.

Lakini kuna swali juu ya nani aliamua pia kuuzwa kwa wachezaji wadogo waliokuwa wakichipukia vyema klabuni hapo – Nathaniel Chalaboah na Nathan Ake ambao ingedhaniwa kwamba wangetunzwa vyema kwa ajili ya miaka ijayo.

Conte ameambiwa aache kukunja uso na kujenga uhusiano usio mzuri na watu lakini haonekani kubadilika, na amekuwa mtu mwenye uamuzi wa ghafla, kama alivyoamua kuondoka Juventus licha ya kwamba alikuwa amewapa ubingwa wa Italia.

Uongozi wa Stamford Bridge na mmiliki pia hawakufurahishwa na madai na majigambo ya Conte kwamba ilikuwa kama miujiza yeye kuwapa ubingwa Chelsea. Wanasema kwa nini iwe muujiza wakati klabu ilikuwa na wachezaji wazoefu wa kutosha na tena wa kimataifa na sasa ameongezewa watatu wa kimataifa, bado analalamika.

Tetesi zilizopo ni kwamba miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo ambao ni ama wazaliwa au wamekaa sana England wamepoteza ule uhusiano mzuri uliokuwa umejengeka baina yao na klabu, hasa baada ya kuondoka kwa Mwingereza Steve Holland aliyekuwa kocha msaidizi na ambaye sasa anafanya na Kocha wa Timu ya Taifa ya England, Gareth Southgate. Hiyo maana yake ni kwamba wachezaji wanaona picha kwamba wanataka kuletwa au kuwekwa zaidi wachezaji wa kigeni, na Conte amekuwa akitaka sana kusajili kutoka kwao Italia lakini amekwama.

Sehemu ya wachezaji wa sasa na wazamani wa Chelsea

Iwapo timu watafanya vibaya, kuna kila dalili kwamba Conte hatakuwa na wakati mzuri na anaweza ama kufukuzwa au kuondoka mwenyewe. Kitakachobadili mwelekeo huo ni timu kurudi kwenye njia za mafanikio na kufanya vizuri kwenye ligi nyumbani na Ulaya.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TUMSOME , TUMWANDIKE NA KUMWELEWA SIMBU

Tanzania Sports

MANCHESTER UNITED TUSIIPUZE , TUKAIDHARAU.