in , ,

Kumbe JOSE MOURINHO alishindwa kuishi na wachezaji wa ‘INSTAGRAM’

Makocha wanaofaa kuchukua nafasi ya JOSE MOURINHO

Nilikuwa natazama mahojiano ambayo alikuwa anafanya na kituo cha BeinSposrts. Kituo ambacho kwa sasa Jose Mourinho ni mchambuzi.

Moja ya vitu vingi alivyoongea , aliongea kitu kimoja ambacho kilinipa picha halisi kwanini Jose Mourinho alifukuzwa pale Old Trafford.

Alikuwa anaelezea namna ambavyo alikwaruzana na mchezaji mmoja ambaye alikuwa hataki kukosolewa hadharani.

Mchezaji huyo alimfuata Jose Mourinho na kumwambia kuwa asiwe anamkosoa mbele ya wachezaji wenzake.

Yani awe ana mwiita pembeni wakiwa wawili ndipo hapo amkosoe. Kitendo hiki Jose Mourinho alikiona cha kitoto sana.

Kwanini ? , kwa sababu kàtika maelezo yake alijikinga kuwa alikuwa sawa kwa kutolea mfano wa kina Didier Drogba.

Ambao kila alipokuwa anawakosoa hadharani walikuwa hawakasiriki, badala yake maneno yake yaliwatia hasira wachezaji.

Kiasi kwamba mchezaji alikuwa anapata nguvu ya kupigana sana ili kesho yake asikosolewe hadharani tena.

Na hii ilikuwa ni njia moja wapo ya wachezaji wale kufanya vizuri katika kipindi chao. Ndiyo ilikuwa chachu ya wao kupigana sana.

Hali imekuwa tofauti kabisa, mwaka 2005 na mwaka 2019 ni muda mrefu sana. Ni kizazi tofauti kabisa.

Vizazi viwili tofauti ambavyo vipo katika nyakati mbili tofauti kabisa. Nyakati za kina Didier Drogba zilikuwa nyakati za wanaume wenye roho ngumu.

Kwao wao hata ukiwaambia kitu gani hukipokea katika mlengo chanya. Ni wachezaji wachache sana kipindi hiki ukiwaambia kitu wakapokea katika mlengo chanya.

Unajua kwanini?, INSTAGRAM imewaharibu sana. Maisha yao wanayaona yako “PERFECT” Muda wote, hutakiwi kutoa kasoro zao mbele ya watu.

Hawajui kabisa kupondwa mbele ya watu ndiko humkomaza mchezaji ambaye huchukulia jambo hilo chanya.

Kosa kubwa huanzia pale mchezaji anapochukulia jambo hilo katika mlengo hasi. Hapo ndipo kosa linapokuja.

Atakuchukia wewe unayemwambia, na hatakuwa na nguvu ile ya kukupigania kama kocha kwa sababu wewe kocha umeonesha kutomkubali mbele ya wachezaji wenzake.

Kitu ambacho hakikuwepo kabisa enzi za kina Didier Drogba, enzi ambazo Jose Mourinho anazitolea mfano kujilinda.

Jose Mourinho alisahahu kabisa hiki kizazi alichokuwa anakifundisha ni kizazi cha INSTAGRAM.

Alishindwa jinsi ya kuishi nacho vizuri ili kiweze kumpigania kama ambavyo aliweza kuishi na kina Didier Drogba katika kizazi chao na kikampigania.

Alishindwa kuishi kirafiki na hawa wachezaji. Alishindwa kuishi kishikaji na hawa wachezaji na wao wakashindwa kucheza kishikaji.

Alishindwa hata kupata muda wa kuwakaribisha chakula cha usiku katika hotel ya nyota tano kwa ajili ya kunywa kwa pamoja.

Kunywa kwa pamoja, kutaniana kwa pamoja ili kutengeneza tu umoja kati yao. Hili alishindwa kulielewa kabisa.

Alishindwa kufahamu mahitaji ya kizazi hiki. Kizazi ambacho maisha yao huyaanika katika mitandao ya kijamii. Kizazi ambacho kinahitaji sifa.

Kizazi ambacho kabla ya kukikosoa lazima uanze na kukisifia sana ndipo hapo unakuwa na uwezo wa kukikosoa bila hata kulumbana na urafiki unabaki pale pale.

Jose Mourinho anatakiwa afahamu kwa kizazi hiki anatakiwa awe zaidi ya baba. Awe rafiki mshikaji, rafiki ambaye anataniana sana na wachezaji.

Rafiki ambaye anaishi na wachezaji kishikaji sana, na siyo kuishi na wachezaji katika misingi ya zamani. Misingi ambayo haiwezi kuwepo katika kizazi hiki.

Kila kizazi kina msingi wake, asijaribu kuishi maisha ya Leo kama alivyokuwa anaishi na kina Didier Drogba.

Dunia ya sasa ni tofauti sana , dunia ambayo imewajaza kina Antony Martial ambao muda mwingi wanautimia kwenye kioo.

Dunia ambayo kina Paul Pogba wanafikiria kuweka fashion kwenye mpira. Ndiyo dunia ambayo tupo. Ndiyo uhalisia halisi. Uhalisia ambao huwezi kuukwepa hata siku moja.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Unai anamuhitaji Ozil au Ramsey?

Tanzania Sports

Tumeacha kujadili UBOVU wa vilabu vyetu, tumehamia kwa WAMBURA