Kocha mpya wa timu ya Yanga Cedric Kaze kutua siku ya Alhamis mwezi huu ambapo Azam FC itakwaana na Mwadui katika dimba la Azam Complex.
Mchezo wa Azam dhidi ya Mwadui ni muendelezo wa ligi kuu Tanzania Bara mzunguko wa sita baada ya kushuhudia magoli 74 yakifungwa katika raundi tano.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya GSM Hersi Said ambayo inaidhamini Yanga amesema kuwa kocha huyo atatua siku hiyo hivyo mashabiki wakae mkao wa kula kumpokea.
“Bado mchakato wa kumleta kocha mpya unaendelea na kwasasa tupo kwenye hatua nzuri ambapo kuanzia wiki hii ya kesho atakuwa ameshawasili nchini.
“Ninadhani Oktoba 15 ambayo ni Alhamis anaweza kuwasili Tanzania rasmi kwa ajili ya kuendelea kukinoa kikosi ambacho kipo kambini kwa sasa,” amesema.
Kaze ndio Kocha chaguo la Yanga hasa kwa falsafa zake za kupiga pasi nyingi na mpira unaotazamika.
Aliyekuwa nyota wa Yanga Mrundi Amis Tambwe ameweka bayana kuwa Yanga wamepata kocha bora kabisa kwa kipindi hiki kutokana na historia ya Mwalimu huyo anapofundisha timu.
“Yanga wamepata kocha mzuri sana, naweza kusema wameramba dume kwani anauwezo mkubwa mpole pamoja na muelewa kwa wachezaji, safari hii naweza kusema kuwa huyu ndio kocha bora kabisa,” alisema.
Kaze bado yupo Canada ambako anaishi huko anatarajiwa kutua nchini kuanza kazi mara moja.
Hapo awali alishindwa kujiunga na Yanga kutokana na matatizo ya kifamilia kwa sasa yupo tayari.
Atakuwa na siku 23 kabla ya kuikabili Simba katika mchezo wa mkondo wa kwanza ligi kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Wanahabari wa Burundi wamesema kuwa kuna programu maalumu zinaandaliwa kwa makocha wan chi hiyo na Kaze ni mmoja ya waliofanikiwa kuzipata kule nchini Ujerumani.
Aliwahi kuwa moja ya makocha wa Barcelona ya watoto na alipewa mkataba mwingine aligoma akihitaji changamoto mpya.
“Nilipewa mkataba wa miaka mitatu Barcelona ya watoto nikakataa nahitaji changamoto mpya, huu ujuzi nilioupata huku natakiwa niurudishe nyumbani,” alisema.
Yanga walimuhitaji sana na waliweza kumvumilia kwani malengo yao yalikuwa baada ya mwaka kupinduka au kuisha kwa msimu ndio wangeachana na kocha aliyeondoka Zlatko maana walimpa mkataba wa mwaka mmoja.
Waliachana na kocha huyo kutokana na kutokuona dalili yoyote ya kuunganisha timu licha ya kuwa na wachezaji nyota.
Burundi imekuwa ikitoa makocha bora sana kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kutokana na mfumo wao mzuri wa Shirikisho lao la Mpira wa miguu.
Shirikisho lao linatoa kozi mablimbali kila mwaka kwa makocha wao ili wakae vizuri, hapa kwetu Seleman Matola moja ya makocha bora kabisa ila anakosa sifa za kuwa kocha mkuu kutokana na kutokuwa na taaluma ya juu, yaani leseni husika ya kuwa kocha mkuu.
Huu ni wakati wa TFF kuangalia namna gani inawasaidia makocha wetu ambao wanaonekana wanakiu ya maendeleo na wanabahati kuwapa sapoti ili wasonge mbele waje kuwa kina Kaze au Ndayiragije.
Licha ya hayo kufanikiwa kwao kunatokana na uthubutu kwani Tanzania wapo makocha wazuri wanakosa hali ya kujiamini.
Kuna makocha wana leseni sawa na hawa makocha wanaoingia nchini mfano Boniface Mkwasa, Mecky Mexime na Hemed Morocco kipi kinawashinda kuomba kazi tofuati na hapa.
Tutawapatia siku yao ya kuwachambua vizuri na kuwapa njia za kupita ili nao watusue katika harakati zao.
Mwisho tumkaaribishe Kaze kama kweli atatia timu, anatakiwa ajue kuwa kwa sasa kuna timu inacheza pira biryani, pira Sambusa, pira Kachori, ila hapo anapoenda bado kuna pira makande sasa yeye alibadilishe liwe pira pizza.
Wananchi wanataka ile ‘Kampa kampa tena’ kama ilivyokuwa kwa kocha Hans Van Pluijm aliyeiwezesha kutwaa mataji mawili mfululizo kabla ya George Lwandamina naye kuja kuchukua taji lao la tatu mfululizo ambalo ndio la mwisho tangu Simba nao wajibu mapigo.
Msimu huu umekuwa mgumu kwani Azam FC nao wana jambo lao hivyo akifika atengeneze timu viongozi wawe na subra.
Comments
Loading…