in , , ,

TUNAPOINGIA JUMA LA 24 LA LIGI YA ENGLAND ?

 

*Arsenal, Man Utd chali…Leicester,Spurs, Liverpool safi…

Wakati mshambualji maarufu Thiery Henry akitathmini kufungwa kwa Arsenal na Chelsea (1-0), katika Sky TV Jumapili hii, aliwataja Tottenham Spurs, akadai: “Ghafla kufumba na kufumbua Tottenham wako pointi moja nyuma ya Arsenal. Wanakuja kasi sana.”

Thiery ambaye alianza maongezi hayo kwa kuwachambua Arsenal walivyoanza mechi vibaya dhidi ya Chelsea alikuwa na maana kuwa ligi ya England ya 2015 -16 haieleweki nani mshindi. Klabu yeyote inaweza kuchukua taji. Tathmini ya mshambualji huyu mashuhuri aliyezichezea Arsenal, Barcelona na Ufaransa alikuwa akirejea fikra za makocha wengi, hasa Arsene Wenger ambaye amekuwa akisema michuano ya mwaka huu ni vigumu kujua nani atakayeshinda.

Tumeingia juma la 23 la ligi ambapo timu ndogo isiyojulikana ya Leicester City inaongoza. Mwaka mmoja uliopita hakuna mshabiki yeyote wa mpira aliyekuwa akizungumzia Leicester City. Wala kocha Claudio Ranieri aliyetumuliwa na Ugiriki kutokana na matokeo mabaya ya kombe la FIFA la 2014, hakuwa akizungumziwa. Ranieri aliyewahi pia kocha wa Chelsea (2000-2004) amekuja juu na kila Leicester City inaposhinda majuma ya karibuni maikrofoni za wanahabari zinakitafuta kinywa chake kutaka kujua analofikiria.

Ana uchawi gani? Nini siri ya ufundi wa Leicester City? Ghafla wachezaji wa Leicester wanatafutwa na kudadavuliwa. Hadi sasa huenda Arsenal wakamnunua Ben Chilwel wa Leicester mwenye miaka 19 tu. Kocha wa England, Roy Hodgson, naye amekuwa akimwangalia mshambuliaji Jamie Vardy wa Leicester kwa macho manne. Vardy ameshafunga mabao mengi kama utitiri. Linganisha ufungaji wake na wa mkongwe  Jermain Defoe (New Castle) aliye na mabao tisa kipindi hiki.

Leicester wameshangaza. Lakini pia kuna Tottenham na mshambuliaji wake hatari, chipukizi Harry Kane. Kitakwimu, Kane amefunga bao kila mechi. Mwaka 2015 Kane aliongoza kwa mabao 14, akawapiku washambuliaji Olivier Giroud (8), Diego Coasta (6) na hata mchezaji bora wa 2015, Eddie Hazard (4).

SI ajabu basi ukawaona Tottenham na Leicester wakiwatisha tisha watani wa jadi Manchester United (nafasi ya 5), Manchester City (2), Arsenal (3) na Liverpool (7). Chelsea, mabingwa wa 2014-15 wako chini sana nafasi ya 14.

Msimamo wa EPL
Msimamo wa EPL

Tuko katikati ya mshike mshike huu na hadi sasa haijulikani nani atakayeinua taji la EPL. Je klabu zisizokuwa na desturi ya kushinda ligi ya England (miaka 30 iliyopita) kama Leicester City na Tottenham Spurs zimekuja juu ya Man United na Man City kutokana na utata wa makocha na wachezaji au kwa kupigana? Washabiki wanaulizana kwanini hadi sasa tuko juma la mwisho la ununuaji wa wachezaji wapya, Januari, na Man United na Chelsea hazijanunua wachezaji wapya? Arsenal imemnunua Mohamed Elneny (Misri na Basel) atakayeongeza nguvu ulinzi wa kati unaohimiliwa na Francis Coquelin. Kila timu inajikakamua kununua wachezaji wa kujazia jazia mapengo. Dirisha la soko la uuzaji wa wanasoka litakapofungwa yatabaki mapambano makali ya miezi mitatu.

Je ni kitu au mambo gani yanatakiwa ili kushinda?

Makocha Guus Hiddink na Arsene Wenger walipohojiwa baada ya mechi ya Jumapili walitoa hoja zinazosaidia kujibu swali hilo. Hiddink alisema ingawa Chelsea wako nafasi ya 14 na hawategemewi kushinda; lililo muhimu ni kutopoteza ari ya kupigana. Mabingwa hawakubali kushindwa hata wakiwa chini kabisa ya matarakimu.

Arsene Wenger aliulizwa lipi muhimu , hisia za kushindwa au kupoteza pointi? Akajibu pointi ndiyo muhimu lakini hisia za kushindwa pia ni muhimu. Kifupi kinachohitajika ni mchanganyiko wa pointi, kutokubali kudhalilika na kuwa na moyo wa ubingwa na upiganaji. Hilo ndilo litakaloamua nani bingwa wa ligi si tu ya England bali ligi yeyote nyingine duniani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

IS THE SCANDAL OF TENNIS MATCH FIXING RELATED TO US?

Tanzania Sports

YANGA YAWEKA REKODI