Nilikuwa namtazama mshambuliaji mpya wa Barcelona Sergio Kun Aguero wakati anatambulishwa Camp Nou nchini Hispania. Kun Aguero anakuwa nyota wa staa wa kwanza kusajiliwa na Barcelona. Pengine sitakosea nikisema ni usajili wa kumliwaza nahodha wao Lionel Messi baada ya kuondokewa rafiki yake Luis Suarez aliyeuzwa msimu uliopita kwenda Atletico Madrid.
Nyota hao wawili Messi na Suarez walikuwa marafiki wakubwa. Urafiki wa Messi na Kun Aguero ni wa miaka miaka mingi katika kikosi cha taifa cha Argentina. Inasemekana kuwa usajili huo unalenga kuhakikisha Lionel Messi anabaki klabu hapo kwani hadi sasa hatima yake haifahamiki iwapo atabaki Barcelona au ataamua kuondoka.
Ukimya wa Messi katika suala la mkataba mpya linatajwa kuwa ni mbinu ya kuangalia mwelekeo wa Barcelona chini ya rais mpya Laporta, kwa kusajili wachezaji wa daraja la juu ambao watamtuliza nyota huyo na kuona mipango madhubuti ya kusaka mafanikio.
Aguero ameondoka Manchester City akiwa mchezaji huru ambako alidumu takribani miaka 10 pamoja na kutwaa mataji mbalimbali. Kuondoka kwa kunatafsiriwa kuwa hakuwa kwenye mipango ya kocha Pep Guardiola. Yaani mshambuliaji ambaye hakuwa sehemu ya mipango ya Man City anasajiliwa na klabu kubwa Barcelona.
Kwa vyovyote vile lazima utajiuliza, ni nani yuko sahihi kati ya Barcelona na Man City. Ifahamike Man City haina mshambuliaji kaliba ya Kun Aguero, na zaidi amehamia katika timu yenye rekodi za kutisha katika mashindano ya Ulaya.
Kun Aguero katika miaka yake 10 aliyodumu Man City ametinga mara moja fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na amejiunga Barcelona ambako suala la kutwaa mataji ya UEFA ni kitu cha kawaida. Ni dhahiri amehama Man City timu yenye pesa nyingi Ulaya lakini haina historia wala ukongwe wowote katika soka la kimataifa barani Ulaya. Hiki nacho ni kichekesho kichungu mno kwake na inabidi akimeze.
Kun Aguero ameondoka Man City ambako mfungaji wao bora msimu ulioishia majuzi 2020/2021 ni kiungo mshambuliaji Ilkay Gündogan. Nyota huyo ametupia wavuni jumla ya mabao 13. Hata kwenye mchezo wa fainali ya UEFA Mei 29 mwaka huu Kun Aguero alikalishwa benchi na safu ya ushambuliaji kuongozwa na Kevin De Bruyne na Bernardo Silva ambao hawakufua dafu mbele ya mabeki wa Chelsea. Hiki ni kichekesho kichungu ambacho Kun Aguero amekimeza, kwamba inakuwaje kocha mwenye akili timamu unamwacha mshambuliaji wako namba moja benchi katika fainali kisa kuwa mtumwa wa falsafa yako badala ya kucheza mfumo kulinagana na adui alivyo.
Pengine kuumia mara kwa mara kwa Sergio Aguero kulichangia kutokuwa mfungaji bora. Hata hivyo hoja hiyo inapingwa kutokana na mwenendo wa kocha Pep Guardiola kwa sababu anapanga mfumo wake wa kila siku huku akishindwa kubadilika kulingana na adui, tena adui aliyemtandika mara 7 kabla. Ilihitaji akili ndogo tu kutambua madhara ya kulazimisha mfumo uleule dhidi ya adui yuleyule. Kwahiyo Kun Aguero hakufeli bali Gaurdiola alifeli kumtumia.
Kun Aguero anasikitisha zaidi, wakati alipokuwa mchezaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Atletico Madrid miaka ya nyuma alihusishwa na timu kubwa kama Real Madrid,Barcelona,Manchester United na Bayern Munich, lakini akakimbilia Manchester City ambako hakukuwa na kivutio chochote zaidi ya pesa za waarabu kulipa mishahara minono.
Katika kipindi alichokaa Man City baadhi ya timu zilizomhitaji zimetwaa mataji ya Ulaya kwa kugawana huku Kun Aguero katika miaka 10 aliyokaa Man City ameambulia kucheza fainali moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hiki ni kichekesho kichungu sana kwa mchezaji wa aina yake.
Na sasa baada ya kuachwa amalize mkataba wake, amejiunga na Barcelona ambayo nayo inajijenga baada ya mafanikio makubwa. Kwahiyo Kun Aguero anakwenda kuwa kama Punda. Hiki ni kichekesho kichungu, kwa sababu mchezaji nyota kaliba yake wakati ule alitakiwa kujiunga na timu yenye mipango Ulaya. Mwenzake Diego Forlan alipoondoka Atletico Madrid alijiunga na Manchester United, ikiwa na maana alikuwa amepanda hadhi.
Ila kwa miaka kumi Kun Aguero alikuwa akicheza ‘ndondo’ huko Man City na amekumbuka umuhimu wa kupandisha hadhi yake wakati wa machweo. Kwamba jua limemchwea, nyakati zake zinashuka na Barcelona wanajijenga upya hali ambayo atajiongezea msongo wa mawazo tu kuchezea timu ambayo inahangaika angalau ipate hata kombe la Mfalme kufuta machozi. Alipaswa kujifunza kwa akina Thiery Henry aliyehama Arsenal kwenda Barcelona ikiwa kali na moto wa kuotea mbali ambako alifanikiwa kutwaa taji la Ulaya.
Sijui msimu ujao Barcelona watavuna nini, lakini kwa jinsi walovyocheza msimu ulioisha ni wazi wataharibikiwa zaidi kama hakutakuwa na marekebisho kwenye kikosi chao. Kipigo cha aibu cha mabao manne kwenye dimba la nyumba kutoka kwa PSG kilitoa ujumbe kuwa timu hiyo inatakiwa kufanyiwa mapinduzi makubwa.
Hili ni funzo hata kwa wachezaji wetu Tanzania wanatakiwa kuchukua fursa haraka za kupanda hadhi katika timu mbalimbali kwa sababu mwisho wa siku pamoja na fedha wanazolipwa katika mishahara yao, kutwaa makombe ni kitu muhimu kwa maisha yao ya soka.
Comments
Loading…