Jose Mourinho anaweza kumaliza uteja kwa Jurgen Klopp? Mechi nane
walizokutana Jose kashinda mechi moja na kupata sare mechi 4 huku
akifungwa tatu
Alama mbili pekee zinawatenganisha hawa watu na wako kwenye vita ya
kupigania nafasi ya pili mpaka sasa.
Wanakutana katika uwanja wa Old Trafford, mechi ya kwanza walitoka
suluhu. Jose Mourinho anamkaribisha tena Jurgen Klopp katika uwanja
wake wa nyumbani, kipi kitakuwa nguvu kwake leo?
Mechi nyingi msimu huu mtu pekee ambaye amekuwa akiwapa uhai Machester
United na kuiweka timu mchezoni kwa muda mrefu ni golikipa David De
Gea
Amekuwa mlinzi dhabiti wa kikosi cha Manchester United, ulinzi wake
umeifanya timu kuwa salama na kuwa ndani ya mchezo kwa muda mrefu.
Maendeleo ya Safu mbili za Ulinzi yakoje kwa timu zote mbili??
Tangu Liverpool wamnunue Van Djik wamenufaika kwa kiasi kikubwa sana,
timu imekuwa haina makosa mengi binafsi nyuma, hata aina ya magoli
waliyokuwa wanafungwa awali kwa sasa yamekuwa nadra sana.
Mfano kabla ya Van Djik , Liverpool walikuwa wakiruhusu magoli
yanayotokana na Krosi au kona. Lakini tangu aje imekuwa nadra kuona
Liverpool wakiruhusu aina hiyo ya magoli kwa sababu Van Djik amekuwa
madhubuti kuokoa mipira hiyo.
Liverpool katika michezo 6 iliyopita amefungwa magoli matatu tu na
kuondoka na clean sheets nne.
Wakati Manchester United imeruhusu magoli manne na kuondoka na Clean
sheets tatu katika michezo hiyo sita iliyopita.
Kwa hiyo kwa hivi karibuni safu ya ulinzi ya Liverpool imekuwa imara
na isiyokuwa na makosa mengi binafsi ukilinganisha na safu ya ulinzi
ya Manchester United.
Manchester United kuingia kama “underdogs” itakuwa na msaada kwao ?
Bila shaka Manchester United leo hii ni “underdogs” kwenye mechi ya
leo, hii inaweza ikawa na faida na hasara
Faida inakuja pale Manchester United watakapokubali kupokea hali hiyo,
hii itawasaidia kuwaheshimu Liverpool. Kitendo ambacho kitajenga
nidhamu na umakini ndani yao
Presha kubwa haitokuwa ndani yao, hali ambayo itawafanya wawe na
utulivu kwa ƙkila nafasi wanayoipata
Hasara ni pale watakapokuwa ogopa hiki kitawafanya wawe na maamuzi
yaliyo na upungufu wa umakini ndani yao.
Hivo wanatakiwa wakubali hali ya wao kuwa underdogs katika mechi hii.
Ukitoa De Gea Upi uimara wa Manchester United?
Kuwa na wachezaji tofauti wa kubadili matokeo. Mfano katika mechi
mbili zilizopita kumekuwa na aina tofauti ya watu waliohusika kubadili
matokeo ya Manchester United
Mechi ya Chelsea Lukaku na Lingard walikuwa chachu ya ushindi wa
Manchester United kwa kutoka nyuma ya goli moja.
Mechi ya Palace walitoka nyuma ya magoli mawili na wakashinda, mtu
aliyebadili matokeo ni Nemanja Matic.
Hii inatosha kukuonesha kuwa Manchester United ina watu wengi
wanaoweza kubadili matokeo ndani ya dakika tisini.
Upi ubora wa Liverpool?? Hapana shaka safu yao ya ushambuliaji ni safu
bora kwa sasa , kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya msimu
huu katika mechi nane walizocheza wamefanikiwa kufunga magoli 28 ikiwa
ni timu iliyofunga magoli mengi zaidi, kwenye ligi kuu ya England
ndiyo klabu ya pili kwa kufunga magoli mengi nyuma ya Manchester City.
Aina yao ya kushambulia kwa kasi ndiyo ubora wao unapoanzia.
Kipi wakifanye Manchester United ?
Cha kwanza ni kuweka ulinzi dhabiti ili kutetengeneza uwazi katika
eneo lao la nyuma , uwazi ambao utatumiwa na wachezaji wa Liverpool
kuwaadhibu.
Roberto Firmino amekuwa chachu kubwa kule mbele kulingana na aina ya
mchezo anaocheza, anacheza kama false 9 hali ambayo inamfanya ashuke
chini, kila akishuka chini katikati lazima beki wa timu pinzani ashuke
kumkaba, akishuka naye kule nyuma huacha uwazi, uwazi ambao unatumiwa
na kina Saido Mane na Mohamed Salah, hivo Manchester United wanatakiwa
kuepuka kutengeneza uwazi eneo lao la nyuma.
Pia kwa sababu Liverpool hushambulia kwa kasi hali ambayo hufanya
kutojidhatiti nyuma. Hivo Manchester United wakicheza mashambulizi ya
kushtukiza inaweza ikawa na faida kubwa kwao.
Kipi wakifanye Liverpool?
Juu nimemwelezea Roberto Firmino, huyu ndiye mchezaji muhimu kule
mbele asiyeangaliwa sana. Kumtumia kama false 9 kutakuwa na faida
kubwa kwao kama nilivyoelezea huko juu.