Beki wa kimataifa wa Simba Shomari Kapombe atatarajia kuondoka nchini Julai 3 kwenda nchini Uholanzi kwa ajili ya majaribio la soka la kulipwa.
Kapombe ni moja ya wachezaji wa timu B ya Simba ambaye alipandishwa mwaka juzi katika timu kubwa akiwa anacheza kama kiungo lakini baadaye alikuwa akibadilishwa nafasi na kuzimudu na kupachikwa jina la mchezaji ‘Kilaka’.
Kwa mijibu wa Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Zacharia Hanspoppe alisema kuwa mchezaji huyo anatarajia kuondoka nchini kuanzia Julai 3 kwenda Twente FC tayari kwa ajili ya majaribio.
Hata hivyo wiki iliyopita Mwenyekiti wa Simba Aden Rage alisema kuwa tayari amekwisha saini barua na kumpa wakala wake ya kumruhusu mchezaji huyo kwenda katika majaribio hayo.
Hata hivyo alisema kuwa mchezaji huyo amekwisha chelewa siku kadhaa mpaka sasa kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine katika timu ya taifa.
Kapombe ni moja ya wachezaji ambao wapo katika timu ya taifa na hivi karibuni alicheza mechi ya kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Ivory coast lakini ndoto hizo ziliisha baada ya Stars kupoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 4-2 katika umchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Kapombe atakuwa bado anakibarua kingine katika timu ya Taifa pale itakapokuwa ikicheza na Uganda Julai 13 katika uwanja wa Taifa kuwania kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) mwakani nchini Afrika kusini.
Rage alisema kuwa kwa sasa hawatasema dau kamili la mchezaji huyo wanachosubiri majibu kutoka Twente FC kama atakuwa amefuzu ndipo wataweka wazi dau la mchezaji huyo.
Endapo mchezaji huyo atafanikiwa kucheza katika klabu hiyo ataweka rekodi ya kuwa mchezaji Mwafrika wa kwanza kucheza katika timu hiyo ambayo inacheza ligi kuu ya Uholanzi.
Kwa upande wa mchezaji mwenyewe alisema kuwa yupo tayari kwenda kufanya majaribio hayo kwani uenda ikawa ndoto yake inaanzia hapo ya kwenda kucheza nje ya nchi.
FC Twente imeandika katika tovuti yake kwamba wakati wowote kuanzia sasa, Kapombe anayetumika kama beki wa kushoto siku hizi, atakuwa huko kwa majaribio.
Kapombe aliyezaliwa Januari 28, mwaka 1992 aliibukia katika klabu ya Polisi Morogoro kabla ya kujiunga na Simba SC miaka mitatu iliyopita.
FC Twente maskani yake yako Enschede, ikicheza Ligi Kuu ya Uholanzi, maarufu kama Eredivisie na ilianzishwa mwaka 1926. Hawa ni mabingwa wa Kombe la KNVB na Johan Cruijff Schaal mwaka 2011, na wamekuwa mabingwa wa Eredivisie msimu wa 2009–2010.
Timu hiyo, inayotumia Uwanja wa nyumbani wa De Grolsch Veste tangu 1998, pia imeshika nafasi ya pili mara tatu Eredivisie na walikuwa pia washindi wa pili wa Kombe la UEFA msimu wa 1974–1975 na kwa ujumla wametwaa Kombe la KNVB mara tatu.
Comments
Loading…