WIKIENDI iliyopita licha ya kuwatazama vigogo wa EPL, Manchester City dhidi ya Liverpool, tulikuwa na mjadala mzito juu ya nafasi ya golikipa. Katika kundi Sogozi la World Soccer, hoja ilikuwa ni namna gani Brazil imefika kuzalisha makipa bora nyakati hizi na kwanini kimewafikisha hapo.
Katika mchezo wa EPL kati ya Man City na Liverpool kulikuwa na tukio moja ambalo lilivutia machoni na akilini. Kuwaona makipa wawili wazaliwa wa Brazil wakiwa kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao lilikuwa tukio la kufikirisha. Alisson Becker alisimama kwenye milingoti ya lango la mabingwa watetezi wa EPL Liverpool. Edersson Moreno alikuwa amesimama katika lango la Manchester City.
Swali letu kuu kwenye makala haya ni je, lini Brazil iliwahi kuibua vipaji vya makipa abao walizichezea timu kubwa? Je, nini kimewafikisha Wabrazil hao kutamba katika kandanda kwa sasa?
Inafahamika kuwa Brazil ndiye bingwa wa Kombe la Dunia ambaye amelitwaa mara tano. Inafahamu Brazil ndiyo nchi ambayo imekuwa ikizalisha vipaji vingi vya soka duniani. Takwimu kutoka taasisi mbalimbali za kimichezo zinasema kuna wanasoka takribani 3,000 wa Brazil waliozagaa nc hi mbalimbali duniani.
Historia ya Brazil inaonesha kuwa imewahi kuwa na makipa hodari kama Claudio Tafarrel, Nelson Dida na Julio Cesar. Dida alikuwa kwenye kikosi cha dhahabu cha AC Milan nchini Italia chini ya kocha Carlo Ancelotti na kikiwa na mastaa kama vile Paolo Maldini, Mauro Camoranesi, Gennaro Gattuso, Richardo Kaka, Ambrosini, Clarence Seedorf na wengineo.
Kwa upande wa Julio Cesar alikuwa nyanda hodari wa Inter Milan ya Italia pia ambako amefanya mambo makubwa. Katika kipindi chake amecheza na mastaa kama vile Javier Zanneti,Samuel Eto’o, Zlatan Ibrahimovic na wengineo.
Rekodi zinaonesha kuwa makipa wa Brazil wamepata mafanikio zaidi katika Ligi Kuu Italia maarufu kama Serie A, ambako Julio na Dida kwa nyakati tofauti walitwaa mataji ya UEFA. Nje ya hapo makipa wa Brazil hawaonekani kutikisa dunia katika Ligi kama vile BundesLiga(Ujerumani),EPL(England), Ligue 1(Ufaransa), Ereviside (Uholanzi), La Liga (Hispania).
Kwa mtazamo wangu tangu kumalizika fainali za Kombe la dunia mwaka 2014 Brazil ambayo ilizabwa mabao 7 na waliokuja kuwa mabingwa Ujerumani inaonesha wanasuka nafasi za makipa kwa nguvu.
Kitendo cha makipa wao wawili Edersson na Allison Becker kutamba katika vikosi vya Manchester City na Liverpool kinapeleka ujumbe kuwa Brazil imeleta kizazi kingine cha walinda milango mahiri.
Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 kipigo walichokipata nchini humo kwenye mchezo wa nusu fainali kiliwakosesha kucheza fainali dhidi ya Argentina kwenye dimba la Maracana.
Kwa kawaida uwanja wa Maracana umekuwa ukiwaliza Wabrazil wengi, ni maarufu kwa msemo wa Maracanazo kutokana na vipigo vya dimba. Uwanja huo umekuwa ukiwaliza mno Wabrazil linapofika suala la kutwaa taji.
Ukiangalia rekodi zao za washambuliaji Brazil wametikisa dunia. Nafasi ya kiungo wakabaji wametikisa dunia, ambapo mmojawapo wa viungo hao ni Gilberto Silva ambaye mara kadhaa huwa nachati naye katika ukurasa wa Instagram masuala mbalimbali kuhusu soka, hususani Fainali za Kombe la dunia mwaka 2002 na maisha baada ya fainali hizo kipindi anachezea Arsenal.
Kwenye nafasi ya mabeki Brazil nao wamebahatika kuwa na miamba iliyotikisa kwa wakati wake. Katika kizazi hiki cha mwisho wapo Thiago Silva na David Luis ambao wamecheza pamoja tangu timu za vijana za Taifa. Wana mastaa wa kutosha katika nafasi mbalimbali lakini eneo la golikipa halikuwa na nyanda wengine waliotikisa nje ya Dida na Julio Cesar.
Turudi kwenye hoja ya msingi, kuanzia mwaka 2014 ingawa ni miaka 6 imepita, lakini mwelekeo wa Brazil unaonesha kuwapika makipa. Kuibuka kwa makipa hawa na kutamba EPL ni wazi Brazil inaendelea kurekebisha makosa yao ya miaka mingi kuwa na makipa ambao wengi walikuwa wanacheza Ligi za ndani. Dida na Julio Cesar kutamba ulaya ni kumetengeneza taswira chanya kwa makipa wa Brazil.
Hivyo ujio wa Allison Becker na Edersson ambao wamekuwa wakichuana kupata namba moja timu ya taifa Selecao, wamekuwa wababe ulaya. Liverpool aimetwaa taji la Ulaya ikiwa na Alisson Becker, kisha Edersson amekuwa mhimili wa mafanikio yote ya Manchester City chini ya Pep Guardiola.
Ni halali kusema makipa hawa wanawakilisha kizazi kipya cha makipa ambacho kinajaribu kupenya na kutamba kama wanavyofanya wachezaji wengine katika nafasi za mabeki wa kati,pembeni, viungo na kadhalika.
Wakati makipa wakiwa kwenye kiwnago bora na wanatamba Ulaya, bado kikosi cha Brazil hakionekani kuwa na makali. Baada ya fainali za Kombe la dunia mwaka 2002, Brazil ilikotwaa taji, haikuweza kutetea kwenye fainali za mwaka 2006. Katika fainali za mwaka 2010 Afrika kusini ikiwa chini ya Caralos Dunga haikuwa na maajabu. Kisha ikaja kuambulia taji la Olimpiki iliyofanyika jijini Rio De Janeiro.
Brazil imesua sua kiuwezo lakini imebahatika kuwa na makipa mahiri. Makipa ambao wamekuwa vinara EPL. Ni zama mpya, na wanaonekana kupikwa makipa zaidi wa Kibrazil.
Comments
Loading…