in

Ikiwezekana ‘tumfukuze’ Fei Toto Ligi Kuu Bara

Fei Toto

FEISAL SALUM maarufu kama Fei Toto ameongeza muda wa kuichezea klabu ya Yanga. Nyota huyo ni zao la soka la Zanzibar ambalo linasifika kuwa na vipaji vya hali ya juu akiwa anapita njia ya kiungo Abdi Kassim na beki mahiri Nadir Haroub waliopata kutamba katika klabuni hapo.

Katika eneo la kiungo Feisal Salum anajua nakshi nakshi na kuupamba mpira kana kwamba mwanamitindo.  Ana kipaji. Ni mchezaji wa kiufundi. Mbunifu. Lakini amenyimwa kasi na misuli ya mwili ya kutosha. Ni mchezaji ambaye huwezi kuhisi ana madhara hadi pale anapofanya vitu vyake ndani ya uwanja.

Uchezaji wake unahitaji walinzi wawili wa kiungo ambao wanasaidia kurahisisha kazi yake. Fei Toto anachojua ni kupika mabao, kuituliza timu miguuni mwake na kuhakikisha wapinzani wanausaka mpira kwa tochi.

Kwenye mchezo wa kwanza wa AFCON dhidi ya Senegal Fei Toto hakufua dafu kiufundi. Aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike aliliona hilo, hivyo ndani ya dakika 29 uwanjani alimwita benchi.

Kwa mtazamo wangu natamani watanzania ‘tumfukuze’ Fei Toto hapa nchini. Tupige kelele zaidi. Tuwalazimishe Yanga ‘wamfukuze’ Fei Toto aende kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Tuwahimize Yanga wafanye hivyo kwa maslahi yao wenyewe kwa kuwa watapata nafasi ya kuzikaribisha klabu nyingine kuona kama kisima cha kuibua vipaji hivyo kutembelewa na mawakala au wawakilishi wa timu mbalimbali.

LIGI ZA KUMFAA

Katika soka nchini wengi kwa sasa wanamtazama nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kama mfano wao. Samatta kwa sasa anakipoga katika klabu ya Aston Villa ya Ligi Kuu England. Tangu akiwa Simba alionesha kiu ya kusaka mafanikio zaidi ambapo TP Mazembe walipofika nchini Tanzania kucheza soka hawakuwa na muda wa kuremba remba kwani waliwasilisha ofa yao ya kumsajili na kumpeleka jijini Lubumbashi.

Miaka michache baadaye Samatta aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika na mchezaji bora wa Afrika wa Ligi za ndani.

Safari ya Samatta kufika Genk inajulikana kabisa. Haina chenga na inaonesha wazi pasipo siri yoyote; kwamba nyota huyo aliitafuta fursa ya kucheza soka barani Ulaya ambapo sasa anakipiga kwenye ligi aliyopenda.

Nikimtazama Fei Toto najiaminisha kuwa sio wa kubaki hapa tena.  Ni mchezaji wa kupanda daraja jingine na kuzichezea klabu kama vile TP Mazembe, Orlando Pirate, Kaizer Chiefs, Zesco, Zamalek, Club African, Esperance sio mbaya atakuwa mbali.  Timu hizo zinacheza katika Ligi ambazo zitamfaa nyota huyo na kuimarisha zaidi kiwango chake na taifa kwa ujumla.

Wakati fulani Kocha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Edna Lema amewahi kuniambia “Bado ni kijana mdogo, ana muda mrefu wa kucheza mpira hapa Bongo au nje, la muhimu atengenezwe zaidi akianzia hapo hapo Yanga kwanza. Kwenda nje inawezakana, na kwa umri huu safari yake ya kuwa bora itatengenezwa na atafikia mafanikio mazuri akizingatia,”

Ni wakati wa wa ‘kumfukuza’  Fei Toto aende nje hata Afrika kusini. Nasema hivi kwa sababu kikosi chetu angalau kinaleta hamasa pale tunapokuwa na wachezaji wanaocheza nje. Tunao Abdi Banda, Simon Msuva,Mbwana Samatta, Hassan Kessy,Thomas Ulimwengu,Rashid Mandawa, na Elius Maguri kwa kuwataja wachache. Tunahitaji mastaa wengi nje ya nchi yetu.

Kadiri tunavyokuwa na wanasoka wakulipwa ndivyo tunainua nafasi ya kuwa kikosi bora cha Taifa Stars. Nyota wetu wakipata maarifa katika nchi zilizoendelea bila shaka wataborosha soka letu nchini.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

‘Midomo’ inayonogesha timu za Ligi Kuu Bara

Barca

Barcelona kumuuza MESSI au kumnunua LA MASIA