Kocha wa Timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson, amewataka wachezaji wa England kwenda ng’ambo na kucheza soka ya kulipwa katika nchi nyingine badala ya kung’ang’ania hapa.
Hodgson anayelazimika kuchukua wachezaji wanaocheza tu katika Ligi Kuu ya England (EPL), amesema wachezaji hao watapata muda mwingi wa kucheza katika timu za nje, na amewaasa chipukizi kufikiria sana hilo.
Amesema kwamba zaidi ya nusu ya wachezaji anaowachagua kwenye Three Lions hawana uhakika wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza katika klabu zao hapa, hivyo ni wakati wa kuchepuka kwa Waingereza kwenda kutafuta muda wa kusakata soka.
Maoni ya Hodgson yanakuja wakati Chama cha Soka (FA) kimekuwa kikitafuta mbinu kubana klabu kuwa na wachezaji wengi wa hapa kwenye timu zao na kuwachezesha, kikifikiria kwamba kuchezeshwa zaidi wageni kunasababisha kudorora kwa timu ya taifa.
Wachezaji bora zaidi kwenye EPL wanatoka nje ya nchi, na hata makocha wa klabu nyingi zilizo juu si Waingereza; kwa mfano wale wa klabu zilizoshika nafasi hadi ya tano kwa ubora msimu uliopita walikuwa wageni.
Hodgson aliyepata kuzinoa Liverpool, Fulham, West Bromwich Albion, Blackburn Rovers na nyingine zaidi ya 20 ndani na nje ya England, amesema ni bora wachezaji wa England wasambae kwenye klabu nyingine bora ng’ambo kuliko kusugua benchi kwenye klabu zao hapa.
Timu ya vijana ya England imefanya vibaya nchini Brazil majira haya ya kiangazi kwa kumaliza wa mwisho kwenye kundi lao na kushindwa kuvuka kuingia hatua ya mtoano kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Duni la vijana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1958.
Hodgson anasema kuwa baada ya England kutolewa mapema kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia la wakubwa nchini Brazil mwezi uliopita, England bado wana fursa nzuri kwa siku zijazo, kwa kutegemea chipukizi ambao wapo wengi.
Wachezaji wanaotambulika rasmi kucheza klabu kubwa nje ya nchi kutoka England ni beki wa kushoto wa zamani wa Chelsea, Ashley Cole aliyejiunga na Roma ya Italia; kipa Luke Steele aliyeko Panathinaikos ya Ugiriki na kipa Matt Jones wa Belenenses ya Ureno.
Wengine ni Kenny Pavey waAIK Stockholm ya Sweden, beki wa kushoto Jordan Stewart wa San Jose Earthquakes ya Marekani; Bradley Wright-Phillips wa New York Red Bulls; Marekani na mlinzi Charlie I’Anson anayechezea Alcoron ya Hispania na kiungo Josh McEachran aliyejiunga Vitesse Arnhem kwa mkopo wa msimu mzima.
Comments
Loading…