in , , ,

Hodgson na kashfa ya ubaguzi

 

*Hata hivyo wadau wengi wamsafisha

 

Kocha wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson anaweza kuwa mwenye furaha kubwa kwa kufaulisha timu yake kucheza Kombe la Dunia Brazil mwakani, lakini kuna makandokando yake.

 

Hodgson (66) amejikuta katika mtanziko baada ya jitihada zake za kutafuta uhakika wa ushindi kwa wachezaji wake wakati wa mapumziko dhidi ya Poland kuhusishwa na ubaguzi.

 

Katika mechi ya Jumanne usiku iliyoishia kwa ushindi wa England dhidi ya Poland kwa mabao 2-0, Hodgson anadaiwa kutoa mfano unaohusisha nyani na watu wanaokwenda anga za juu.

 

Kocha huyo anadaiwa kumtaka beki wa kulia, Chris Smalling kujitahidi kutoa pasi kwa winga Andros Townsend (mweusi) ambaye angetekeleza jukumu lote la kuhakikisha mabao yanapatikana, akimfananisha na miruko ya nyani au jitihada za wanaanga wanaokwenda anga za juu.

 

Hodgson, hata hivyo, kwa mujibu wa wadau wengi, akiwamo Townsend, Wayne Rooney na hata Chama cha Soka (FA), hakumaanisha kubagua yeyote wala kuhusisha suala hilo na tofauti ya rangi kwa wachezaji wake.

Andros Townsend akiwa na Kocha wake Roy Hodgson
Andros Townsend akiwa na Kocha wake Roy Hodgson

 

Hodgson, ambaye baada ya mechi alisema kwamba alikuwa na wakati mgumu kila vijana wa Poland walipovuka nusu yao na kuingia upande wa England, alifananisha kazi ngumu waliyokuwa nayo na zile za Nasa wanaokwenda anga za juu.

 

Kwa msingi huo, anaweza kuwa alirejea masuala ya nyani kutokana na uhodari wake wa kuruka kutoka tawi moja la mti hadi jingine pasipo kuanguka wala kuumia, japokuwa baadhi walinusa harufu ya ubaguzi.

 

Na hilo lilitokea kwenye chumba cha kubadilishia nguo, ambapo inadaiwa lilivujishwa kwa umma na mtu mmoja, na Hodgson aliomba radhi.

 

Townsend, mchezaji mpya kwenye timu hiyo mwenye umri wa miaka 22 alisema kwamba anashangazwa na kuzushwa kwa suala hilo na haelewi kwa nini limeibuliwa, kwani ana uhakika hakuna kosa wala ubaguzi uliomaanishwa na hakuna aliyeudhiwa.

 

Mwenyekiti wa FA, Greg Dyke anasema walichukua hatua za haraka kuchunguza tukio zima na kujiridhisha kwamba Hodgson aliyepata kuwa kocha wa Liverpool na West Bromwich Albion hakuwa na kosa lolote.

 

“Ameshafafanua kwa kina muktadha na kile alichosema na alichokuwa akisisitiza kwa wachezaji wake wakati wa mapumziko usiku wa Jumanne … anafanya mambo mazuri na makubwa kwa timu hii wala hakumaanisha kubagua yeyote,” anasema Dyke.

 

Wanaharakati wa kupinga ubaguzi, Kick It Out, wamepongeza FA walivyojitokeza mapema, kuchunguza na kuweka wazi kilichotokea badala ya kulala. Inaelezwa kwamba hakuna malalamiko yoyote rasmi yaliyokuwa yametolewa na wachezaji wa England hadi usiku wa kuamkia Ijumaa hii.

 

England wamefuzu kucheza Kombe la Dunia Brazil baada ya safari ngumu, ambapo walikuwa na wakati mgumu wa kuzidiwa na Ukraine, Montenegro na Poland.

 

Wameibuka washindi wa kwanza kwenye kundi lao la ‘H’ lakini Hodgson tayari amesema kwamba nchi yake haipewi nafasi kubwa miongoni mwa timu zinazotarajiwa kutwaa kombe hilo.

 

Hata hivyo ameshasema kwamba kuvuka hadi Brazil ni mafanikio makubwa zaidi kwake katika maisha ya ukocha wa soka.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Vermaelen afikiria kuiacha Arsenal

KAMATI YA UCHAGUZI YATANGAZA WAGOMBEA TFF