Baada ya miaka 29 katika kiti cha urais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika, Issa Hayatou amebwagwa kwenye uchaguzi uliofanyika hii leo huko Adis Ababa, Ethiopia. Ameshindwa dhidi ya Ahmad Ahmad ambaye ni mkuu wa Chama cha Soka cha Madagascar.
Mkameruni huyo amekuwa rais wa shirikisho hilo tangu mwaka 1988, ambapo pamoja na utata na changamoto nyingi vilivyokuwa vikimkabili katika uongozi wake lakini aliweza kushikilia nafasi hiyo mbaka hatima yake hii leo.
Mkameruni huyo amepoteza uchaguzi huo kwa kura 20 dhidi ya 34 za mpinzani wake. Amepoteza uchaguzi huo kwa tofauti kubwa ya kura lakini huu ni wakati wake wa kuachia nafasi hiyo chini ya utawala wa mtu mwengine.
Kabla ya kupoteza uchaguzi wa leo Hayatou alipokea upinzani mara mbili tu kwenye nafasi yake ambapo aliibuka na ushindi mnono kwenye chaguzi zote mbili na kubaki kwenye nafasi yake.
Hayatou mwenye umri wa miaka 70 sasa alikuwa akiomba ridhaa ya kuliongoza shirikisho hilo kwa muhula wa nane. Anasifiwa zaidi kwa kuongezeka kwa idadi ya timu za Afrika kwenye michuano ya Kombe la Dunia na kuongeza kitita cha zawadi kwenye mashindano ya soka barani humu.
Ahmad alihitaji kula 28 pekee kuweza kushinda kiti hicho cha urais lakini amepata ushindi wa kishindo ambao ni kielelezo tosha kuwa kambi ya meneja wake wa kampeni Philip Chiyangwa imefanya kazi nzuri na kubwa mno.
Ushindi wa Ahmad umeleta mshangao kwa wengi ambao walitarajia kuwa rais wa muda mrefu, Hayatou angeendelea kushikilia nafasi yake, lakini pengine huu ni mwanzo mpya kwa soka la Afrika kwa kuwa anakuja rais mpya baada ya takribani miongo mitatu.
Ahmad wa miaka 57 na mwenye watoto wawili aliwahi kuwa mchezaji na kocha wa mpira wa miguu kabla hajachukua nafasi ya uongozi wa juu katika Shirikisho la Mpira wa Miguu la nchini Madagascar mwaka 2003.
Rais huyo mpya aliyeonekana mwenye furaha iliyopitiliza kwa ushindi huo anakuwa rais was saba kuliongoza shirikisho hilo lenye historia ya miaka 60. Anachukua nafasi ya muhula wake wa kwanza wa miaka minne na ameahidi kulifanya shirikisho hilo kuwa la kisasa na kuliongezea uwazi zaidi.
Wadau kadhaa wa soka la Afrika wametoa maoni yao kuhusiana na mwisho wa utawala wa Hayatou akiwemo makamu wa rais wa Chama cha Soka cha Ghana, George Afriyie aliyesema kuwa Hayatou amefanya kazi kubwa lakini huu ni wakati wa yeye kuachia kiti hicho.
Rais wa Chama cha Soka cha Liberia, Mussa Bility naye alisema kuwa Afrika imefanya uamuzi wa maana mno na wapo tayari kwa mabadiliko yaliyochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu.