in , , ,

NILICHOKIONA KWENYE MECHI ZA UEFA.

Wakati ukiwa unajiuliza mengi kuhusu Leicester City na kikosi chao
kufika robo fainali, mimi akili yangu bado haijatoka kwenye kikosi cha
Monaco.

Kuna kipindi Jadim alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwalea na
kuwatengeneza kina Anthony Martial, Kondogbia, Carrassico na wengine
wengi lakini mwisho wa siku watoto walimkimbia baba na kwenda kutafuta
maisha pengine katika miji ya Manchester Unitéd, Atletico Madrid,
Intermilan na sehemu zingine.

Nina hofu pia baba mzazi atakimbiwa na watoto wake wapya baada ya
msimu huu kuisha.

Bernaldo Silva ameshakuwa mtu mzima yule, ameshakomaa kukabidhiwa
nyumba kubwa zaidi ya Monaco kuiongoza.

Unaweza ukamwita Henry mpya, lakini mimi nitakukataza na sitoweza
kusema Mbappe ni Henry mpya,wapo wengi waliwahi kuitwa hivo kina
Sanogo, Martial lakini mpaka sasa wapo wamepumzika njiani baada ya
safari ndefu ya kufika alipokuwa anaishi Henry.

Kwa maana hii haitoi
maana halisi ya kwamba Mbappe ni moja ya vipaji bora ambavyo vitakuja
kuweka ufalme wao binafsi katika soka.

Katika umri wa miaka 18 ,msimu huu akiwa ameanza katika michezo 17 na
kufunga magoli 16 . Inaonesha kwamba huyu ni mfalme anayetakiwa
kutengeneza himaya yake.

Ulimuona Mendy ? Kama ulimuona hakika utakubaliana na mimi kuwa ni
moja ya watoto ambao wameshabalehe na kukomaa kuondoka nyumbani kwenda
kutafuta maisha sehemu nyingine.

Manchester City, imetolewa kwenye UEFA

Kina Yaya Toure wameshaondoka katika timu ya taifa ya Ivory Cost,
taratibu namuona Bakayoyo kuja kuwa mhimili mkubwa hapo baadaye. Jana
alitimiza majukumu yake ya kulinda na kushambulia kiufasaha.

Monaco walikuwa wameshamaliza mchezo kipindi cha kwanza, Manchester
City walikuja kuamka kutoka kwenye giza totoro kipindi cha pili, akawa
anahitajika mtu wa kutembea na tochi kuwaongoza wenzake katika giza
lile ,lakini Kun Aguero aliichomoa betri moja ya tochi ambayo ilikuwa
mpya na kuweka kuukuu kisha wakaanza kutembea kwenye giza totoro
wakiwa na mwanga finyu. Kwa ufupi Aguero hakuamua kuwapeleka
Manchester City robo fainali.

Pamoja na Monaco kupita kwenda robo fainali lakini safu yao ya ulinzi
haijakomaa, na safu ya ulinzi ya Manchester City ni mbovu.

Kukosekana kwa Gameiro kulinipa wasiwasi kama Antoine Griezmann
ataweza kucheza vizuri na mchezaji tofauti lakini ushirikiano wao na
Angel Correa ulitosha kuonesha kuwa Antoine Griezmann anaweza akacheza
na mchezaji yoyote.

Najua sifa nyingi zinastahili kwenda kwa Oblak, huyu alikuwa
anakosekana sana kipindi cha nyuma alipokuwa majeraha.

Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na kipa imara kwenye hii michuano, kama
ilivyo kwa Atletico Madrid, pia Leicester City kwa asilimia kubwa
Kasper Schmeichel amewabeba mgongoni leicester city kuanzia mechi ya
kwanza na ya pili. Ndipo hapo umuhimu wa goli kipa bora kuhitajika
kwenye hii michuano.

Pamoja na kwamba kikosi bora chenye njaa ya ushindi huitajika ili
kufika mbali kwenye michuano hii, pia bahati pia ina nafasi yake.

Sevilla walikosa bahati tangia mchezo wa kwanza ambapo walikosa nafasi
nyingi za wazi, hata mchezo wa pili bahati haikuwa upande wao mpaka
wakakosa Penalty.

Ile hali ya hewa ya uwanja wa King power ulikuwa unakupa picha gani ?
Mashabiki walikuwa na njaa, kitu pekee kilichokuwa kinahitajika
kutuliza njaa yao ni ushindi, ndiyo maana hawakuchoka kupiga kelele
kwa kuwahimiza na kuwakumbusha wachezaji kuwa chakula bora kilichokuwa
kinahitajika wakati huo ni ushindi.

Unaweza ukaangalia jinsi baadhi ya wachezaji wa Leicester City
walivyoanza kurudi taratibu kwenye viwango vyao vya msimu uliopita,
ukiachana na Ndindi kufanikiwa kuingia vizuri kwenye kikosi lakini
kina Drink Water, Vardy, Mahrez wamesharudi walipokuwa wanaishi msimu
uliopita, lakini kwa mchezo wa juzi Albrighton alikuwa bora kuzidi
wao.

Kadi nyekundu ya Alex Telles ndiyo iliyowafanya wapoteze mchezo kwanza
,Kadi nyekundu ya Maxi Perreira ndiyo iliyomaliza nguvu za FC Porto
kupambana kumtoa Juventus.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

PAMOJA NA KADI NYEKUNDU, FAHAMU MAMBO MANNE YALIYOSABABISHA UNITED KUPIGWA

Tanzania Sports

HAYATOU NJE URAIS CAF, AHMAD RAIS MPYA