Je, Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), Issa Hayatou atamudu uongozi wa muda aliopewa katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)?
Hilo ni swali linaloulizwa na wadau wa soka, hasa wa Ulaya, Asia na Marekani wakati shirikisho hilo likipita katika wakati mgumu.
Amekaimishwa kiti hicho baada ya Rais wa Fifa, Sepp Blatter kusimamishwa kujihuisha na soka kwa siku 90.
Blatter amesimamishwa sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini, wakituhumiwa kwa uongozi mbovu katika utoaji na upokeaji rushwa.
Hayatou kwa kuwa ndiye makamu mwenyekiti mwandamizi wa Fifa aliyebaki alipewa hatamu za uongozi.
Kamati ya Maadili ya Fifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Uswisi na mamlaka za Marekani wanaendelea na uchunguzi mpana juu ya tuhuma za wizi na utakatishaji wa fedha katika Fifa kwa miongo kadhaa chini ya Blatter na washirika wake mbalimbali.
Caf inasisitiza kwamba, Hayatou hana tatizo, anamudu kazi hiyo na aachwe aendelee nayo, hata kama kumetokea tetesi kwamba kuna mgogoro kuhusu afya yake.
Raia huyu wa Cameroon alitarajiwa kuwasili Zurich, Uswisi kuanza kazi yake Jumanne hii, lakini anadaiwa kukabiliwa na matatizo ya figo na huhitaji kuchujwa damu mara kwa mara.
Taarifa ya Caf imesema: “Tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa wa urais wa Caf, Hayatou, pasipo matatizo yoyote alichukua majukumu na kuyatekeleza vyema.
“Katika miaka ya karibuni si siri tena kwamba Hayatou ana matatizo ya figo na amekuwa akihudhuria kliniki kwa ajili ya kuchuja damu. Hajapata tatizo zaidi, akimaliza amekuwa daima akiendelea na majukumu yake kitaaluma kabisa.”
Hayatou (69) ndiye makamu wa rais wa Fifa aliyefanya kazi kwa muda mrefu zaidi miongoni mwa wanaotoka kwenye mabara mengine na sasa atafanya kazi za Blatter (79) hadi itakapoamuliwa vinginevyo.
Blatter na Platini wamekata rufaa kupinga uamuzi wa kuwazuia kujihusisha na shughuli zozote za soka kwa siku hizo 90.Watapelekwa mahakamani iwapo ushahidi utapatikana.
Pamoja na mambo mengine, Blatter anadaiwa kumhonga Platini 2011 ili asigombee urais kupingana naye, na muda mfupi baadaye Mfaransa huyo alijitoa. Hayatou amekuwa rais wa Caf tangu 1988.
Matukio haya yanakuja wakati Marekani ikiwa imeshawashitaki maofisa 14 kwa makosa yanayohusisha mamilioni ya dola tangu 1991. Saba kati yao walidakwa jijini Zurich kabla ya mkutano mkuu wa Fifa Mei mwaka huu.
Blatter alikuwa ameahidi kwamba angeachia ngazi Februari mwakani, akitoa ahadi hiyo siku nne tu baada ya kuchaguliwa tena kukalia kiti hicho. Alikuwa ameshauriwa asigombee na Platini.