in , , ,

Gharika Manchester City

*Wachakazwa 3-1 na vibonde Southampton

*Arsenal, Chelsea, Spurs, Swansea kicheko

 

Mabingwa wa Soka wa England, Manchester City wameangukia pua kwa kuchakazwa mabao 3-1 na timu dhaifu ya Southampton.

Kocha Roberto Mancini aliyeingia uwanja wa St. Mary’s akiamini angeondoka na pointi zote tatu muhimu, hakuamini vijana wake walipopokea kipondo hicho.

Itabidi Man City wajilaumu wenyewe, maana mabao yote yalitokana na uzembe wao, likiwamo la kujifunga wenyewe moja kwa moja, Gareth Barry akiumimina mpira kwenye kona ya juu ya goli lake.

Kiungo wa Southampton, Jason Puncheon alipachika bao la pili, baada ya mkwaju wa Jay Rodriguez kuokolewa.

Steven Davis aliandika bao la tatu kiulaini kutokana na makosa ya kipa wa kimataifa wa England, Joe Hart, aliyeutema mpira uliopigwa na Rickie Lambert.

City walipata bao lao kupitia kwa Edin Dzeko, lakini halikutosha kuzuia Saints kumpa ushindi wa kwanza kocha mpya, Mauricio Pochettino, na kushika nafasi ya 15.

Ilikuwa siku mbaya na yenye baridi kwa Mancini, kwa sababu maana ya matokeo hayo ni kwamba Manchester United wanaweza kutanua pengo la uongozi wa ligi kwa pointi 12 Jumapili hii wanapowavaa Everton.

Ilikuwa mechi ambayo City walicheza hovyo kwenye ulinzi, pasi mkaa na ushambuliaji duni, hivyo kombe lao kuwa rehani, kwani imebakisha michezo 12.

Hii ni mara ya saba kwa Man City kukubali kipigo cha mabao matatu (haijafungwa zaidi ya hayo) katika mechi za ligi kuu chini ya Mancini.

Vipigo viwili vizito zaidi ya hiki cha Jumamosi ni kile walichogawiwa na Arsenal cha 3-0 Oktoba 2010 Etihad na kingine kama hicho kutoka kwa Liverpool Aprili 2011.

Chelsea wa Rafa Benitez walifufukia kwa Wigan, baada ya kuwachapa mabao 4-1 Stamford Bridge na kujiimarisha katika nafasi ya tatu.

Mabao ya Chelsea yalifungwa na Ramires, Frank Lampard, Marko Marin na Eden Hazard.

Lile la kufutia machozi la Wigan lilifungwa na Shaun Maloney, lakini timu hiyo ya Roberto Martinez imebaki katika eneo la kushuka daraja.

Tottenham Hotspurs nao walitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuwafunga ‘Wafaransa’ wa Newcastle mabao 2-1, japokuwa kwa shida.

Magoli ya Spurs yalifungwa na Gareth Bale aliye kwenye chati sasa, huku Newcastle wakipata lao kupitia kwa mshambuliaji mpya, Yoan Gouffran aliyeumia baadaye na kubebwa kwa machela kutolewa uwanjani. Spurs wanabaki nafasi ya nne na Newcastle ya 16.

Arsenal walijitahidi na kushinda ugenini, licha ya kucheza watu 10, baada ya Carl Jenkinson kupewa kadi ya pili ya njano katika mchezo dhidi ya Sunderland.

Santi Cazorla aliwafungia Arsenal bao pekee, likiwa ni la 50 kwa ligi msimu huu, baada ya kazi nzuri ya Theo Walcott. Washika bunduki hao wa London walimpoteza Jack Wilshere aliyeumizwa.

Arsenal wanabaki nafasi ya tano huku Sunderland wakiwa wa 13.

Queen Park Rangers (QPR) wameedelea kuburuta mkia kwa tofauti ya pointi nne, baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Swansea ugenini.

Reading waliokuwa wameanza kuamka, walichezea kipondo cha mabao 2-1 kutoka kwa Stoke City.

Kwa matokeo hayo Reading wanashika nafasi ya 17 na Stoke ya 10.

Norwich na Fulham walitoshana nguvu kwa kwenda suluhu, hiyo ikimaanisha Norwich wanashika nafasi ya 14 na Fulham ya 12.

Kabla ya mechi ya Man United na Everton katika uwanja wa Old Trafford, Aston Villa wanaosuasua watawakaribisha West Ham United katika dimba la Villa Park, jijini Birmingham.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

England bado kazi mbichi

Mali wakomalia ushindi wa tatu