in , , ,

Ghana inapoteza kizazi chake cha dhahabu?

Ni huzuni tele kwa Ghana. Na sio tu kwa taifa hili lenye historia kubwa kwenye soka la Afrika, bali pia kwa mashabiki wa mchezo huu kutoka kila pembe ya dunia. Si maumivu ya kufungwa uwanjani pekee, ni hisia ya kushindwa kufanikisha ndoto. Ghana, taifa lililozoea kuwa na nafasi kwenye majukwaa makubwa ya soka, sasa limejikuta likikosa tiketi ya kushiriki mashindano ya AFCON 2025 huko Morocco.

Jumapili iliyopita ilionekana kama fursa ya kufuta machozi. Mchezo dhidi ya Angola ulionekana kuwa mwanya wa mwisho wa kujisafisha na kurudi kwenye reli. Lakini badala yake, ndoto hiyo ikageuka jinamizi. Matokeo ya kushindwa yaliacha mzigo mzito wa huzuni, sio tu kwa timu, bali pia kwa mashabiki walioshuhudia matumaini yao yakizama zaidi.

Athari hizi si za kawaida. Kutokuwepo kwa majina makubwa kama Thomas Partey Antoine Semenyo na Mohammed Kudus kwenye viwanja vya Morocco itakuwa pengo kubwa si kwa Ghana pekee, bali kwa mashindano yenyewe. Soka la Afrika litakosa nguvu na haiba ya vipaji vya aina hii vilivyosheheni kwenye taifa hilo la Magharibi mwa Afrika, jambo ambalo limezidisha masikitiko kwa wengi wanaoelewa umuhimu wa Ghana katika historia ya michuano ya AFCON.

Ghana wamekuwa wabovu kwenye mechi za kufuzu. Kwa kiwango walichoonyesha ni dhahiri wamestahili kutokufuzu. Walipata matumaini kiasi kwenye michezo miwili ya mwisho. Walipaswa kushinda yote na kuiombea Sudan inayonolewa na kocha wa zamani wa Ghana, Kwesi Apiah ipoteze michezo yake yote miwili. Sudan ikaanza kupoteza ugenini dhidi ya Niger kwa kuchapwa 4-0. Hakuna aliyetarajia. Ni kipigo kiichotoa angalau matumaini fulani kwa Ghana ambao walipaswa kushinda dhidi ya Angola. 

Goli la kichwa la Antonio Cabaca ‘Zini’ aliyeunganisha krosi ya Felício Milson lilitosha kuzima matumaini ya Ghana waliotangulia kupata goli kupitia kwa mshambuliaji wake Jordan Ayew katika dakika ya 18.  Kinachouma zaidi kwa waghana sio kushindwa kufuzu, ila kushindwa kufuzu kwenye kundi linaloonekana ni la kawaida, sio gumu uilinganisha sifa, uzoefu, historia na vipaji ilivyo navyo Ghana. 

Taifa hilo halijawahi kukosa fainali za Africa (AFCON) toka mwaka 2004. Hii ni mara ya kwanza Ghana kushindwa kufuzu tangu kuanza kwa mfumo mpya wa fainali za AFCON unaoshirikisha zaidi ya timu nane. 

Kwa kushinda fainali za mwaka 1963 na 1965, ‘the Black Stars’ wamekuwa miongoni mwa miamba ya soka la Afrika. Katika fainali sita kati 2006 na 2017, wamekuwa wakifanya vizuri na kufika angalau nusu fainali lakini sasa licha ya kuwa na Partey, Kudus na Semenyo, na nyota wengine kama Iñaki Williams, Abdul Fatawu na Tariq Lamptey, matokeo yamekuwa ya ajabu huku dalili za kuyumba kwao zilianza kujionyesha wazi mapema. 

Baada kupoteza kwa penati dhidi ya Tunisia katika hatua ya 16 bora mwaka 2019, mara mbili wametupwa nje katika hatua za makundi. Katika michezo yote mitatu kwenye fainali za mwaka 2022 waliruhusu mabao dakika za jioni kuanzia dakika ya 80 wakiondolewa kwa fedheha kwa kuchapwa 3-2 Comoro. 

Tanzania Sports
Baadhi ya wachezaji wa Ghana, wanaowika na Vilabu vyao Ulaya

Wakamtimua kocha wao Milovan Rajevac na kumleta Addo huku Chris Hughton akiwa Mkurugenzi wa ufundi.  Licha ya kufuzu fainali za kombe la dunia huko Qatar mwaka 2022 tena kwa shida kwa mikwaju ya penati katika mchezo wao dhidi ya Nigeria, hakuna mabadiliko yoyote ya maana yaliyofanyika baada ya hapo. Katika fainali hizo, waliondolewa katika hatua ya makundi. Mwaka 2023 kwenye AFCON, Hughton akikabidhiwa mikoba ya ukocha, wakaleta aibu nyingine, wakachapwa jioni na Cape Verde, kabla ya kwenda sare na Msumbiji, licha kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Hughton akatimuliwa, Addo akarejeshwa, wakiamini atarejesha matumaini, lakini yale yale. Bao walilochapwa katika dakika ya 93 huko Angola liliwalaza hoi. Siku nne baadaye ukawa msiba kabisa, bao la kusawazisha la dakika ya 81 lililofungwa na Oumar Sako lilitosha kuhakikisha Ghana inapoteza alama mbili dhidi ya Niger. 

Mwezi uliopita walipata alama mbili tu kwenye michezo dhidi ya Sudan. Walibadili uwanja kutoka mji wa Kumasi kwenda Accra kwa sababu za kiusalama kwenye uwanja wa Baba Yara. Hilo halikutosha. Uwanja ulikarabatiwa harakaharaka tu, kuonyesha namna miundo mbinu ilivyotelekezwa.

Kuelekea chezo huo dhidi ya Sudan, Rais wa shirikisho la soka la Ghana, Kurt Okraku, alisema “Mkitoka sare, halafu naona wachezaji wakicheka, haikubaliki, watu milioni 30 wanaumia.” Wakatoka 0-0; katika mchezo wa kwanza. Hakuna aliyecheka wala kulia. Mambo yakawa mabaya zaidi mechi ya marejeano wakalala 2-0.

Nini kimewaendea kombo Ghana? Wanataja kuwepo kwa matatizo kwenye maendeleo ya mpira wa vijana. Kingine ni tatizo la kuleta muunganiko wa timu. Kuwaunganisha pamoja wachezaji lukuki nyota iliyonao, huku Semenyo, Lamptey na Williams wakiwa miongoni mwa wachezaji 8 waliondolewa katika kikosi cha hivi karibuni. Kutokuwepo kwa Partey dhidi ya Sudan, huku André Ayew akistaafu soka la kimataifa, Ghana inabaki kuwa na uhaba wa uzoefu wa uongozi ndani ya uwanja.

Mambo haya na suala la kukosekana kwa muelekeo sahihi ni mwiba kwa soka la Ghana. Wamebadili makocha mara 7 tangu wamtimue Avram Grant mwaka 2017, kitu ambacho Rais wa Shirikisho, Okraku anapaswa kuwajibika nacho. Kwa vipaji ilivyonavyo Ghana ilipaswa kufuzu michuano ya Morocco. Kutofuzu kwao wengi wanakutaja kama ni uzembe na wanapaswa kubeba lawama na kujilaumu wenyewe. Wana kila kipaji cha kuwafanya wafuzu michuano yote mikubwa ya soka, achilia mbali AFCON. Kusuasua kwao kunachochea mjadala wengi wakijiuliza je taifa hili linapoteza kizazi chake cha dhahabu?

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Sakuru Na Deni Zito Kwa Simba Ya Fadlu

Tanzania Sports

Jinsi kocha wa Yanga alivyoaibishwa kimbinu