KATIKA mchezo wa soka mchezaji anapokuwa na umri wa miaka 30 tayari anaonekana kama mzee. Huyu anatajwa kuwa mchezaji aliyefika kikomo cha kuonesha makali yake. Wachache wanaweza kudumu katika mchezo huo wakipambana na vijana wenye kasi.
Miongoni mwa wachezaji ‘wazee’ katika dunia ya sasa ni Cristiano Ronaldo (40) na Luka Modric (39). Hawa ni wachezaji wanaotajwa kuwa ‘wazee’ na wamemzidi miaka mingi Fiston Mayele.
Katika mchezo wa soka wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mshambuliaji wa Pyramids Fiston Mayele ndiye aliibuka nyota wa mchezo huo kwa kupachika mabao mawili muhimu katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Orlando Pirates.
Mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye wiki moja iliypita nchini Afrika Kusini timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana, kwahiyo mchezo wa marudiano ulikuwa muhimu kwa timu zote. Orlando Pirates walihitaji sare ya mabao aina yoyote ili wavuke kwenda fainali na walitangulia kupachika bao la kuongoza, kabla ya Fiston Mayele kusawazisha kwa wenyeji Pyramids.

Hata hivyo jambo linaloshangaza katika klabu ya Pyramids ni mshambuliaji wake Fiston Mayele kuonesha ubora wake uzeeni. Nyota huyo raia wa Jmahuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisajiliwa na Yanga akiwa na umri wa miaka 27 na alikuwa mfungaji bora namba mbili katika Ligi ya Kongo. Akiwa Yanga alitinga fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini kubwa zaidi linalokumbukwa ni namna alivyokuwa akipachika mabao bora kwenye mashindano ya CAF.
Mayele hakuwa mchezaji chipukizi. Hakuanza kutamba akiwa na umri mdogo kama wengine wanaong’ara wkaiwa na umri wa miaka 17, 18, 19, 20, au 25, lakini Mayele alikuwa na miaka 27 ikiwa na maana mitatu kabla ya kuwa mzee katika mchezo wa soka.
Katika Kombe la Shirikisho akiwa na klabu ya Yanga alifanya mambo makubwa ambayo yaliwezesha vigogo wa soka waanze kuwinda saini yake. Mbio za vigogo kutaka kumnunua mshambuliaji huyo zilikuw anyingi lakini Pyramids pekee ndiyo walifanikiw akuinasa saini yake. Akiwa katika kikosi cha Pyramids yeye ndiye mshambuliaji namba moja na tegemeo katika eneo la ushambuliaji.
Amepachika mabao muhimu katika mechi muhimu, lakini Mayele anaonesha ubora wake uzeeni. Katika umri wa miaka 30 anapambana na mabeki ngangari chipukizi kama wa Orlando Pirates pamoja na wengine wa Ligi Kuu Misri. Katika umri wa miaka 30 anapachika mabao ya vichwa, miguu yote miwili, mpishi wa mabao, mchezaji mwenye kasi na zaidi anajua namna ya kuwasambaratisha wapinzani wake anapokuwa kwenye lango lao.
Mchezo wa nusu fainali wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Orlando Pirates, Fiston Mayele alionesha kitu kingine cha ziada katika mchezo wa soka. Kwanza alikuwa anafanya kazi ya kupika mabao akiamini mabeki wa wapinzani wao wamemkamia. Alikuwa anakokota vyema mpira, alirudia katika eneo la nusu ya uwanja kufuata mpira ili kucheza gonga safi na wachezaji wenzake kuelekea eneo la adui.
Katika moja ya matukio yanayokumbukwa ni namna alivyowatesa kwa kurukia krosi zilizotua eneo la hatari. Mayele aliweza kuruka na kupiga vichwa vya hatari vilivyomtesa golikipa wa Orlando.
Wakati mwingine alikuwa anachupia pasi za mbali na kuiwatisha mabeki wa Orlando. Matukio matatu yalikuwa hatari zaidi ni pale alipopachika bao la tatu baada ya kuruka kupiga kichwa kisha golikipa wa Orland kupangua, lakini Mayele alinusu namna ya udakaji wa kipa huyo kwa vyovyote ungekuwa wa kupangua, kwahiyo ikawa rahisi zaidi kwake kuokota dodo lililokuwa linaambaaambaa.
Bao la tatu la Pyrmids limedhihirisha sababu ya klabu hiyo kumsajili haraka kwa kuwalipa fedha nyingi Yanga ili wapate huduma yake. Na sasa amewafikisha hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo wanakwenda kuchuana na wakali wengine wa kandanda Mamelodi Sundowns.
Katika uchezaji ilitegemewa Mayele awe na umri wa miaka 25 kama akina Kylian Mbappe, Vinicius Junior, Martin Matinneli, Bukayo Saka, na wengineo wengi katika ulimwengu wa kandanda. Isivyo bahati mashabiki wa soka Misri wanakishuhudia kipaji cha Fiston Mayele katika hatua za mwisho kuelekea uzeeni.
Baada ya misimu miwili au mitatu Fiston Mayele atakuwa si huyu wa sasa mwenye miaka 30. Ni sawa na kusema kipaji chake kimeibukia zaidi uzeeni kuliko alivyokuwa kinda. Hata Zinedine Zidane kipaji chake kilikithiri zaidi alipokuwa na miaka 25, lakini kwa Fiston Mayele mambo ni tofauti.
Kibiashara Mayele si wa kununuliwa na timu zenye mipango ya muda mrefu, kwani hawezi kuwahakikishia kucheza katika kiwnago hiki kwa miaka minne ijayo ambayo atafikisha miaka 34. Kwa maana hiyo Pyramids watalazimika kubaki na dhahabu yao ambayo hakuna timu kubwa itakayoweza kuweka kiasi cha kikubwa cha fedha kupata huduma yake. Kwani kwa sasa Fiston Mayele anaonesha umahiri huku jua linamchwea.
Comments
Loading…