in , , ,

FEI TOTO NI YULE YULE WA JUZI, JANA NA LEO

Ananifurahisha mchezaji wa Azam FC anayeitwa Feisal Salum. Nasikia mashabiki zake wanamuita Fei Toto. Sijali! Katika jezi za Azam FC, Fei Toto ameanzia pale pale alipoishia alipokuwa katika jezi za Yanga SC. Vizuri.

Mpaka Fei Toto anaamua kuachana na Yanga SC mwishoni mwa mwaka 2022 na kurudi kwao Zanzibar alikuwa katika kiwango bora.
Binafsi nilijiapiza ule ndiyo ulikuwa msimu wake bora. Kumbe nilijidanganya na mawazo yale bila kujua.

Ndani ya msimu huu Feisal amezifikia namba zile za Yanga SC na kuziacha kwa mbali. Kwa mbali mno. Na atazidi kuziacha takwimu zile zilizonifanya niamini ni takwimu bora zaidi kwake. Msimu huu na jezi za Azam FC, Feisal yuko katika kiwango bora. Ndiyo anashika usukani wa ufungaji bora.

Ameshafunga mabao 12. Haya ni mabao ambayo hakuwahi kuyafunga msimu mmoja alivyokuwa na Yanga SC tangu alivyosajiliwa akitokea kwao Zanzibar katika klabu ya JKU.  Huenda akamaliza msimu kama mfungaji bora wa msimu huu. Nani ajuae?

Ilitegemewa Feisal angeanzia chini kidogo au apotee kabisa. Imewahi kuwatokea mastaa wengi walipoamua kuondoka timu za Kariakoo kwa mbwembwe na kuhamia Azam FC. Idadi ni nyingi. Ni kweli walivyohamia Azam FC  walikuwa na maisha magumu na baada ya muda wakajifia. Inahuzunisha tukianza kuwakumbuka.

Inawezekana Feisal akawa anayakumbuka baadhi ya matukio tofauti tofauti ndani ya Yanga SC. Sana ni maisha ya nje ya uwanja jinsi mashabiki wanavyoshangilia timu yao, lakini ndani ya uwanja pale Azam FC Feisal ameendelea kubakia yule yule.

Uncle Mrisho Ngassa ni mmoja wa mhanga. Ramadhan Singano ‘Messi’ anafuatia. Hawa ndani ya Simba SC na Yanga SC walikuwa katika ubora mkubwa, walivyojiunga na Azam FC ni kama vile walijichimbia ‘Makaburi’ yao. 
Kule walienda ‘kujizika’. Akaunti zao za Benki zilinona, lakini wakapoteza marafiki na wafuasi waliokuwa wanawapenda. Kuna namna ambayo Ngassa na Singano waliwahi kusema na mioyo yao jinsi walivyojisikia upweke wa kucheza timu iliyokosa mashabiki tofauti na timu walizotoka.

Inawezekana wasiwe wamekuja hadharani kuonesha majuto yao kwa maamuzi waliyofanya, lakini wenyewe ndani ya mioyo yao walijisononekea, kujisikitikia. Simba SC na Yanga SC haziishii kukupa tu ukubwa wa jina na umaarufu, lakini pia zinakupa na idadi ya mashabiki.

Feisal wa leo hana tena namba kubwa ya mashabiki wanaochizika nae, licha ya Akaunti yake kunona. Hii ni faraja kwake. Udogo wa Azam FC ulishuhudia Uncle Ngassa kuwa mfungaji bora wa ligi yetu. Lakini sijui kama watu wengi wanalijua hili.

Unadhani sababu ni nini? Ngassa amekuwa mfungaji bora katika timu ambayo haina mashabiki. Haifuatiliwi na hata mabao yake aliyokuwa anayafunga yaliishiwa kushangiliwa na watu wachache.

Ni kama mabao ya Prince Dube hivi sasa pale Azam FC yanavyoshangiliwa na namba ndogo ya watu. Jibu la Uncle Ngassa ni hili.
Angalau Feisal ameanza vyema katika jezi za Azam FC. Ni faraja kwake, lakini pia ni faraja kwa timu. Hapa kwa Feisal na Azam FC kila mmoja anamfurahia mwenzake.

Njia pekee ya kumfanya Feisal ajutie haya maamuzi ya kuachana na Yanga SC na kujiunga Azam FC ni kufanya vibaya binafsi na timu. Binafsi yuko sawa, japo timu ilipotea njia kwa kutolewa mapema katika mashindano ya kimataifa, lakini katika ligi Azam FC ni washindani wa kikweli kweli.

Katika msimamo wako katikati ya Simba SC na Yanga SC. Lakini kama timu ingekuwa vibaya na Feisal mwenyewe akawa vibaya, kivyovyote vile Feisal angekuwa anajisikia maumivu makali, hasa akitazama kinachofanyika upande wa Yanga SC hivi sasa.

Kuna mahala mwanadamu hutazama nyuma na kuona mabaya na mazuri yake aliyowahi kufanya. Mwanadamu huyu hujisikia furaha akitazama nyuma na kuona mazuri, lakini kama nyuma alifanya vibaya huwa hatamani sana kugeuka kuitazama nyuma yenyewe.

Hivi sasa Feisal anaweza kutazama nyuma bila wasiwasi wala kujutia maamuzi yake. Kiufupi tu Feisal bado ni yule yule. Wa juzi, jana na leo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Pogba: Historia, mwisho wake umefika?

Tanzania Sports

RIP John Zambetakis