in , ,

FAINALI LIGI YA MABINGWA ULAYA: Chelsea inavyoweza kuikung’uta Bayern

Siku zimekwisha, saa na sekunde nazo zinamalizika kupisha mtafutano kati ya Chelsea na Bayern Munich zinazosaka heshima ya Kombe la Ubingwa wa Ulaya.
Jumamosi hii, nyasi za uwanja wa Allianz Arena zitawaka moto, huku jiji lote la Munich likitawaliwa na rangi nyeupe na nyekundu zinazotumiwa na timu mwenyeji.
Hata hivyo, Chelsea wanaovaa rangi za bluu na nyeupe wanaweza kuwalowesha Bayern, kama walivyoishangaza dunia kwa kuwasukuma pembeni timu bora zaidi duniani, Barcelona.
Ndani ya kambi ya Bayern lakini, morali imeshuka kiasi, baada ya timu yao kujikuta ikiaibishwa kwenye fainali ya Kombe la Ujerumani.

Vigogo hao walioingia fainali kwa kuwatoa Real Madrid kwenye nusu fainali, walipata kipigo kinachotatiza cha mabao 5-2 kutoka kwa Borussia Dortmund Jumamosi iliyopita.
Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness alijaribu kuondoa wingu la huzuni kwa wachezaji wake na kutoa matumaini mapya kwa ajili ya mechi hii muhimu.
“Pengine kuonyesha unyenyekevu si jambo baya sana kwa wakati huu,” Hoeness aliliambia gazeti la kila siku la Ujerumani, Sueddeutsche Zeitung.
Morali ya wachezaji na timu kwa ujumla imeshuka hivyo kwamba vyombo vya habari vya Ujerumani haviipi tena Bayern nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo.
Hali imebadilika na ilivyokuwa pale vijana hao wa Kocha Jupp Heynckes walipoishinda Real Madrid ya Jose Mourinho kwa penalti baada ya kutoshana nguvu kwenye muda wa kawaida.
Pamoja na mwelekeo huo wa vyombo vya habari, ukweli ni kwamba Bayern Munich bado ni timu kubwa na inayotarajiwa kutoa upinzani mkali kwa Chelsea.
Kwamba Bayern ni klabu kubwa na inayoogopewa si jambo lenye ubishani, kwani inajulikana zaidi kwa soka yake ya kitaalamu na yenye mafanikio zaidi nchini Ujerumani.
Wana Bavaria hao wameshatwaa mataji 22 ya kitaifa na vikombe vingine 15, ikifikia kilele cha mafanikio yake chini ya uongozi wa Franz Beckenbauer enzi hizo.
Jumamosi hii, Bayern wanaingia dimbani kutafuta heshima nyingine, kwani ni mara yao ya tisa kutinga fainali ya Kombe la Ulaya/Ligi ya Mabingwa, na wakishinda itakuwa mara ya tano kutwaa taji hilo.
Real Madrid na AC Milan tu ndio wamefika fainali hii mara nyingi kuliko Bayern wanaocheza fainali hii nyumbani mbele ya washabiki wake, hivyo wana kila sababu za kuhakikisha kombe linabaki nyumbani.
Udhaifu unaotarajiwa kwa Bayern katika mechi hii ni kwenye ulinzi wa kati, kwani Daniel Van Buyten ni majeruhi wakati David Alaba na Holger Badstuber wana kadi.
Kiraka katika nafasi ya mkoba anatarajiwa kuwa mchezaji wa Ukraine, Anatoly Tymoshchuk ‘Tymo’ mwenye rekodi ya kutwaa Kombe la UEFA mwaka 2008 alipokuwa nahodha wa timu ya Zenit St Petersburg.
Inawezekana Tymo akawa na kazi ya kumzuia mshambuliaji mkongwe wa The Blues, Didier Drogba aliyewaliza Barcelona katika dimba la Stamford Bridge kwa kuwafunga goli muhimu.
Timu mbili hizi zilikutana kwenye robo fainali ya mashindano kama haya mwaka 2004-05, ambapo Chelsea walishinda kwa uwiano wa mabao 6-5. Mabao matano kati ya hayo sita yalifungwa na wachezaji ambao bado wanakipiga kwenye klabu hiyo ya London.
Wakicheza kwa kumtumbukizia Drogba mipira mirefu, Chelsea walifanikiwa kuwa tishio mbele ya wenyeji wao wa sasa, kiasi kwamba Drogba mwenyewe alifunga mabao mawili.
Hofu nyingine kwa Bayern safari hii ni bahati mbaya aliyo nayo Jerome Boateng ambaye ni sehemu muhimu ya ulinzi kukatika katika nyakati muhimu za mchezo.
Kadhalika, mlinzi huyo wa zamani wa Manchester City hachukuliwi kuwa na uwezo kama wa Badstuber ambaye hatakuwa mchezoni.
Diego Contento anatarajiwa kuchukua nafasi ya Alaba ya beki wa kushoto. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ni mwepesi wa kubadilika kadiri ya mchezo unavyokwenda, japokuwa udhaifu unaweza kuibukia kwake pia.
Beki wa kulia, Philipp Lahm, akitofautishwa naye, ni mzuri hivyo kwamba hata Kocha wa Chelsea, Roberto Di Matteo alimtaja kama watu wa kutupiwa macho, kwa uzito sawa na Franck Ribery, Arjen Robben na Mario Gomez.
Nahodha wa Bayern na Ujerumani, Philipp Lahm amekuwa mchezaji muhimu katika mechi nyingi kiasi cha kufananishwa na mashine, kwa jinsi anavyohaha kuwalisha mipira washambuliaji wake, hasa Robben.
Chelsea wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kumpiga pini tangu dakika za mwanzo na kuhakikisha hawatambi uwanjani.
Imekuwa kawaida yao kuwahisha krosi katika eneo la hatari, hivyo Chelsea watatakiwa kuhakikisha bughudha zote za aina hiyo hazikatizi nyuma ya mabeki wa kati wala kumfikia kipa wao, Petr Chech.
Pamoja na kasi ambayo wamekuwa nayo, kukosekana kwa Luiz Gustavo anayetumikia adhabu kunatarajiwa kuiacha Bayern isiwe na kiungo wa kuaminika kwa vile Tymo atakuwa ameshahamia pembeni kuziba pengo jingine. Ni kweli kwamba kuna akina Toni Kroos na Bastian Schweinsteiger watakaocheza kwa pamoja, lakini huenda wasiweze kutoa ukabaji na utengenezaji nafasi kwa kiasi kinachotakiwa.
Ni kwa sababu hiyo, Juan Mata wa Chelsea atatakiwa kuwa macho ili atumie kila upenyo unaojitokeza katika maeneo hayo kuifaidisha timu yake.
Thomas Mueller atakayecheza nafasi ya Gustavo anajulikana zaidi katika mashambulizi kuliko kwenye kiungo.
Kwa msingi huo, Bayern huenda ikawa nzuri zaidi mbele kuliko katika kiungo, ambako Chelsea wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kutawala.
Chelsea hawatakiwi kufurahia mno uimara wao kwenye kiungo, bali wanatakiwa kuwa waangalifu pia kwa sababu Robben na Ribery wanaweza kuwasababishia matatizo makubwa.
Hali hiyo itatokea iwapo mabeki wa Chelsea hawatapata usaidizi kutoka kwa viungo. Jose Bosingwa, beki mtarajiwa wa kulia, anaweza kuwa mwathirika wa hali hiyo.
Mkakati muhimu unaweza ‘kujaza’ watu kwenye sehemu watakazokuwapo Robben, Lahm, Mueller na Ribery, kuwanyima kupumua na pia The Blues wakafanya mashambulizi kutoka upande huo huo.
Chelsea wanatakiwa kujijenga hivyo tangu mwanzo kuhakikisha inawakaba vilivyo wachezaji hao wenye mbio, hata kama mwanzo wataonekana kana kwamba hawaendi popote.
Mario Gomez anaweza kuwa muuaji katika mechi hii kutokana na mtindo anaoutumia katika uchezaji wake.
Ni mchezaji mwenye magoli 41 katika mashindano yote, 12 kati ya hayo kwenye Ligi ya Mabingwa, kwa hiyo ni mtu mwenye ufunguo muhimu.
Mjerumani huyo ni mshambuliaji mwenye kipaji, anayejua kunusa na asiyeachia nafasi inayojitokeza hata katika mazingira magumu kabisa. Hutokea wakati mwafaka kwa timu yake na mara nyingi huizawadia.
Kiufundi hachukuliwi kuwa mchezaji bora sana katika mazingira ya kawaida, lakini kinachompandisha chati ni kwamba hufunga ni kila kiungo cha mwili wake kinachoruhusiwa kufanya hivyo, karibu kama alivyowahi kufanya Gerd Mueller.
Kwa mtu wa umbo lake, hana nguvu nyingi na huwa hapendi kucheza dhidi ya mabeki imara wa kati na mara nyingi hajishughulishi sana kama ambavyo angepaswa.
Chelsea wakifanikiwa kumnyamazisha, wanaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuchukua kombe hilo, kwani Bayern wana nafasi finyu kwa kuangalia mbadala ulio kwenye benchi lao.
Msingi wa mchezo wa Bayern huwa ni katika kumiliki mpira, lakini kwa vile Mueller anapocheza pembeni umiliki wao wa mpira hauwi mzuri.
Kwa hali hiyo Chelsea watatakiwa kujizatiti kwa kutumia mipira mirefu, kuwahadaa viungo wa Bayern na kujaribu kufunga.
Hata hivyo, uzoefu walioupata Bayern kwenye fainali ya Kombe la Uerumani kwa kuchabangwa mabao 5-2 na Borussia Dortmund ni utawasaidia. Vijana hao wa kocha Jupp Heynckes watachukua hadhari kwa vile hawatakuwa na kungo wa uhakika.
Kwa uhakika wa kuzuia mabao dhidi yao, Chelsea wanatakiwa kutibua ushirikiano wa Robben na Ribery kwenye winga, huku wakiziba mianya ya Mueller kupata mipira, kwani ndiye humlisha Gomez mara kwa mara.
Bao la kwanza kwenye mechi ni muhimu sana, lakini sasa Bayern wanalihitaji zaidi ya timu nyingine. Katika msimu mzima, ni mara moja tu walishinda mechi walizoanza kufungwa bao, ukiondoa ushindi wake dhidi ya Real Madrid uliopatikana kwa penalti.
Mara nyingi Bayern wakishatangulia kufungwa, Robben na Ribery hukosa uvumilivu hivyo kucheza hovyo na wakati mwingine kwa hasira na Gomez hubadilika na kuweza kuiumiza timu, hasa mpira unapoelekea kumkataa.
Hata hivyo, wachezaji wa Bayern wametupilia mbali nadharia kwamba kwa vile wanacheza nyumbani, basi patakuwapo shinikizo kubwa upande wao, lakini ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya washabiki wake wataishiwa nguvu ikiwa Chelsea wataonyesha uimara mchezoni.
Ipo pia hatari ya mgawanyiko wa chini chini ulio miongoni mwa Bayern ukajitokeza waziwazi. Kwa kadiri Chelsea watakavyoweza kuwabana na matokeo kubaki walau suluhu au sare, ndivyo Bayern watakavyoathirika kwa njia hasi.
Hizo ndizo njia zinazoweza kutumiwa na Chelsea kama watataka kuwakata maini wababe hao wa Bavaria ambao chini ya uongozi wa Beckenbauer walitwaa Kombe la Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 1974.
Upepo unaweza ukaelekea kwingine lakini, hasa ikizingatiwa kwamba Bayern katika miaka ya karibuni imedhihirisha ubora wake kuliko timu nyingine za Ujerumani, ikitwaa ubingwa wa Bundesliga mara sita katika misimu 10 iliyopita.
Taji lake la mwisho katika ngazi ya kimataifa ni Kombe la Mabara ililotwaa mwaka 2001, mwaka ambao pia walitwaa Kombe la Ulaya kwa mara ya nne. Bayern ni klabu inayoendeshwa kwa msingi wa kuwa na wanachama na washabiki wanaosajiliwa rasmi.
[email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Simba`s industrious midfielder Patrick Mutesa Mafisango (32) died in a car crash in Dar es Salaam yesterday morning.

Chelsea inavyoweza kuikung’uta Bayern Munich…