in ,

FAINALI KAGAME: HISTORIA ITAJENGWA

Kesho ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam Azam FC itaingia uwanjani kupambana na Gor Mahia ya Kenya kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la CECAFA (Kagame). Kila timu kati ya hizi mbili ina shauku kubwa ya kutwaa ubingwa huo.

Kila aliyepata nafasi ya kutazama michezo kadhaa ya nyuma ambayo timu hizi zimecheza tangu kuanza kwa michuano hii atakubaliana na mimi kuwa hizi ndizo timu zilizoonyesha ubora zaidi ya timu zote. Ni timu zilizostahili kupata nafasi ya kucheza fainali hii.

Gor Mahia ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye michuano hii. Imefanikiwa kufumania nyavu za wapinzani mara 14 kwenye michezo sita iliyocheza mbaka sasa huku ikifanikiwa kufunga katika kila mchezo.
Safu ya ushambuliaji ya timu hii inayoongozwa na Michael Olunga ni moto wa kuotea mbali.

Kwa upande mwengine Azam FC inaingia kucheza fainali hii ikiwa haijaruhusu bao hata moja. Serge Pascal Wawa, Aggrey Morris na walinzi wengine wa Azam wameunda ukuta wa chuma.

Hivyo mchezo huu wa fainali unaikutanisha timu yenye safu kali zaidi ya ushambuliaji dhidi ya timu yenye ulinzi mkali zaidi kwenye michuano ya mwaka huu.

Michael Olunga na timu yake wana kibarua kigumu mno dhidi ya ulinzi mkali wa Azam FC.

Serge Wawa na wenzie pia watakuwa na kibarua kigumu mno kumdhibiti Olunga aliyefunga mabao matano mbaka sasa hali kadhalika na washambuliaji wengine wa Gor Mahia.

Azam FC haijawahi kushinda ubingwa wa michuano hii tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007. Wachezaji na mashabiki wa timu hiyo wanataka kuona timu hiyo ikijenga historia kwa kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza.

Hawako tayari kuona timu yao ikiacha kombe uwanjani kama mwaka 2012 iliponyukwa 2-0 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Yanga.

Kushinda mchezo wa kesho ni njia pekee ya Azam kujenga historia wanayoitamani. Historia ya kushinda Kombe la CECAFA.

Pia itakuwa ni timu pekee ya Tanzania iliyowahi kuchukua ubingwa wa michuano hii ukiitoa Simba iliyowahi kushinda mara 6 na Yanga iliyoshinda mara 5.

Vile vile itaweka rekodi ikiwa itashinda mchezo huo wa kesho bila kuruhusu bao. Sina uhakika sana na rekodi za miaka ya nyuma ila rekodi za miaka kumi ya karibuni zinaonyesha hakuna timu iliyowahi kushinda michuano hii bila kuruhusu bao.

Kwa upande mwengine Gor Mahia pia wanakusudia kujenga historia. Wababe hawa wa nchini Kenya kwa mara ya mwisho walicheza fainali ya michuano hii mwaka 1985. Hata nyota wao Michael Olunga alikuwa hajazaliwa.

Kwenye fainali hiyo iliyopigwa huko nchini Sudan Gor Mahia waliwatungua ndugu zao AFC Leopards mabao mawili kwa sifuri na kushinda taji la michuano hii kwa mara ya mwisho.

Wakati huo rais wao wa Kenya alikuwa Daniel Arap Moi. Tangu kuondoka kwa rais huyo Gor Mahia hawajawahi kushinda kombe hili tena.

Ukaingia utawala wa rais Mwai Kibaki na ukaondoka pasipo timu hiyo kushinda taji la michuano hii.

Ila sasa wamepata nafasi ya kushinda kombe hili wakati nchi yao ikiwa chini ya rais Uhuru Kenyatta. Wanataka kujenga historia mpya. Kuna uwezekano Gor Mahia wakajenga historia hii.

Mtanange mkali wa hapo kesho utaamua ni timu gani ijenge historia. Nawaona Azam FC kama timu itakayojivunia zaidi ubingwa huo ikiwa itafanikiwa kuutwaa kuliko namna ambavyo Gor Mahia wanaweza kujivunia.

Washinde Azam FC ama washinde Gor Mahia, historia itajengwa tu. Hakuna namna nyingine.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Zamalek mabingwa Misri

NGAO YA JAMII ENGLAND: