in

Fahamu mambo muhimu kuhusu nyota mpya wa Yanga

Saido Ntibazonkiza

Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza anazidi kung’arisha  nyota yake Ligi Kuu Tanzania Bara. Nyota huyo kutoka nchini Burundi  amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga tangu alipoanza kusakata  kabumbu kwenye klabu yao kwenye mchezo wa kirafiki kati ya  mabingwa hao wa zamani na Singida United ya mkoani Singida.  Makala haya yanaeleza mambo muhimu kuhusu nyota huyo. 

1. Bao la Stars lampa ujiko 

Kama kuna siku ambayo itakumbukwa na mashabiki wa Tanzania ni  pale waliposhuhudia timu yao ya taifa ya Taifa Stars ikinyukwa bao 1-0  na Burundi katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Mkapa jijini  Dar es salaam. Katika mchezo huo Saido Ntibazonkiza alipachika bao  pekee la Burundi kwa njia ya adhabu ndogo, maarufu. Ni bao hilo ndilo  lililompa ulaji wa kusajiliwa na Yanga akiwa mchezaji huru. 

2. Umri mkubwa, kasi ya kijana 

Nyota huyo raia wa Burundi ana miaka 33 kwa sasa, lakini ana uwezo  mkubwa wa kucheza kwa kasi kama kijana wa miaka 25. Kasi, upigaji  wa chenga na namna anavyomudu kukaa na mpira ni vionjo ambavyo  vimewavutia mashabiki wengi wa soka. baadhi ya wachambuzi  wanaamini Yanga walipaswa kumpata nyota huyo mapema kuliko sasa  ambako uwezo wake unaelekea ukingoni. Hata hivyo wanatolea mfano  Zlatan Ibrahimovic kuendelea kucheza mpira akiwa na umri mkubwa,  ama alivyo Cristiano Ronaldo mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa  akiwa haonekani kuacha soka siku za karibuni. 

3. Bao mbili siku ya kwanza. 

Katika mchezo wake wa kwanza kuichezea Yanga ulikuwa dhidi ya  Singida United ya mkoani Singida. Yanga walicheza mchezo kama  sehemu ya kuimarisha kikosi chao. Saido Ntibazonkiza alifunga mabao  mawili kwenye mchezo dhidi ya Singida United. Katika mchezo huo  Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-0. Kiwango cha Saido  kiliwakosha wengi na kutajwa kuwa silaha nyingine ya kutaka kutwaa  ubingwa msimu huu. Ndoto za nyota huyo zipo wazi kuwa anatamani  kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Yanga. 

4. Kujinadi YoTube

Saido ni mchezaji wa kipekee ambaye amewekeza kutangaza kazi zake  za uwanjani kupitia mtandao wa YouTube. Katika video hizo kuna  matukio mbalimbali anapokuwa dimbhani na namna anavyoonesha  ubora kwenye mchezo wenyewe. Jambo hili limekuwa adimu kwa  wachezaji wengi wa kitanzania. Hiyo ni mbinu mojawapo ya  kujitangaza kama mwanasoka. Kupitia ukurasa wake wa Facebook  anawaomba wafuasi wake kutembelea chaneli ambayo anaweka video  hizo ili wajionee ufundi wake. 

5. Kipaji na maamuzi ya haraka.  

Ukizungumza na mashabiki wa soka nchini huwa wanatamka maneno  mawili mawili muhimu kumwelezea Saido Ntibazonkiza; ‘Kipaji’ na  ‘maamuzi’ ya haraka. Anatajwa kuwa mchezaji mwenye kipaji na  maamuzi ya haraka, anajua wapi aupige mpira ili kutoa pasi za mabao au  kufunga mabao kwa njia ya mipira ya adhabu ndogo. Hana uchoyo wa  kutoa pasi. Yanga walikuwa wanakosa mchezaji wa kupigapasi za  mwisho za uhakika na kusaidia washambuliaji kupachika mabao. Kwa  mashabiki wa kandanda wanaona nyota huyo ameleta elimu mujarabu  kwa wanasoka wazawa. 

6. Upara kama mastaa wa Ulaya

Saido Ntibazonkiza ni kundi la wachezaji maarufu duniani ambao wana  upara na ambao wamewahi kutamba katika vilabu vyoa na mataifa  mbalimbali duniani. Nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji wenye  upara, ambaye anafananishwa hali hiyo na mastaa wengine wenye upara  kama vile Arjen Robben,Andres Iniesta,Zinedine Zidane,Estaban  Cambiasso,Jaap Stam,Fabien Barthez,Pablo Zabaleta,Lee Carsley, Sir  Bobby Charlton, 

7. Mkali wa ‘Free kick’ 

Nyota huyu anasifika kwa uwezo wa juu wa kupiga mipira ya adhabu  ndogo, ambayo kwa kimombo imezoeleka na mashabiki kama’ free  kick’. Saido alipachika bao la kwanza la Ligi Kuu Tanzania bara  kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Dodoma Jiji uliofanyika kwenye  uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Baada ya mpira kutinga  wavuni katika pambano hilo wengi walirudisha kumbukumbu zao katika  mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Burundi ambako nyota huyo  alitumbukiza mpirani wavuni kwa free kick. Kwahiyo Yanga  wamekuwa hatari kwenye eneo la mipira ta faulo karibu na lango la adui  kwa sababu wana uhakika wa kufunga kutokana na kikosi chao kuwa na  mchezaji mwenye uwezo huo.  

8. Rollingstone na Ulaya 

Wanahistoria ya soka wanatueleza kuwa Saido Ntibazonkiza si mgeni  katika ardhi ya Tanzania. Wanasema nyota huyo amewahi kushiriki  mashindano ya mpira wa miguu ya Roollingstone yanayofanyika jijini  Arusha miaka kadhaa iliyopita. Kwa mantiki hiyo Saido anaijua  Tanzania, anafahamu hamasa za soka zilivyo nchini. Katika soka la  kulipwa amewahi kucheza soka katika nchi za Uholanzi, Ufaransa, Poland na Uturuki.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Huu ni mwisho wa utawala wa La Liga duniani?

Serengeti boys

Taswira ya soka Tanzania itabadilika kwa kufanya haya..