*Nahodha Spurs ahamia Hull
Mshambuliaji mkongwe wa Cameroon, Samuel Eto’o amejiunga na Everton, akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Chelsea.
Eto’o (33) amesaini mkataba wa miaka miwili na ataungana na mchezaji wa zamani wa Chelsea, Romelu Lukaku aliyesajiliwa majira haya ya joto kwa pauni milioni 28, na wote wanacheza kama washambuliaji wa kati.
Eto’o alishaonesha awali nia ya kujiunga Arsenal ili amwoneshe Jose Mourinho kwamba si mzee kama alivyodai, lakini Arsene Wenger hakuonesha kumtaka. Kadhalika Liverpool walimchukua na kumsubirisha ili iwapo wangeshindwa kumsajili Mario Balotelli wamchukue yeye.
Kocha Roberto Martinez wa Everton anasema kwamba walikutana an Eto’o na kufanya mazungumzo mazuri, akaridhika naye kwamba bado ana njaa ya kucheza na kufunga mabao, akasema Everton ndiyo mahali mwafaka kwake.
Mchezaji huyo bora wa Afrika kwa miaka minne, alifunga mabao 12 katika mechi 35 msimu uliopita kwa Chelsea, ambao walimsajili Agosti mwaka jana kutoka Anzhi Makhachkala. Anaweza kucheza katika mechi dhidi ya Chelsea Jumamosi hii.
Eto’o alianzia soka yake Real Madrid kabla ya kuhamia kwa mahasimu wao, Barcelona na akiwa hapo Nou Camp alifanya vyema kati ya 2006 na 2009 na kutwaa ubingwa wa Ulaya, akafunga mabao katika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na pia alitwaa makombe matatu ya La Liga.
DAWSON ATOKA SPURS KUJIUNGA HULL
Nahodha wa Tottenham Hotspur, Michael Dawson ameihama klabu yake hiyo na kujiunga na Hull City kwa pauni milioni sita, licha ya kocha Mauricio Pochettino kuwa amemhakikishia kwamba ana nafasi ya kucheza bado.
Dawson (32) amekuwa na Spurs tangu 2005 na msimu uliopita alicheza mechi 41 kwa timu hiyo. Hull wanajaribu kuongeza wachezaji katika safu ya ulinzi kwa ajili ya mechi nyingi watakazokuwa nazo, ikiwamo uwezekano wa Ligi ya Europa.
Dawson amecheza zaidi ya mechi 300 kwa klabu hiyo ya London Kaskazini na alijiunga hapo akitoka Nottingham Forest. Kaka mkubwa wa Dawson aitwaye Andy, alichezea Hull kwa miaka 10, akiwasaidia kupanda daraja na mdogo wake anasema anaifahamu vyema klabu hiyo.
Comments
Loading…