in , , ,

Drogba, Falcao kwaheri

*Arsenal waja na Arturo Vidal, Chelsea na Baba Rahman
*Glen Johnson, Mulumbu, Allardyce Jua limewachwea

Baada ya Ligi Kuu ya England kumalizika, mambo yanazidi kufunguka juu ya wanaoondoka au kuingia kwa ajili ya msimu ujao.

Mshambuliaji mkongwe wa Ivory Coast, Didier Drogba ni mmoja wa wachezaji walioaga baada ya kuwatumikia Chelsea kwa msimu mmoja wa ziada, aliporejeshwa mwaka jana na kocha Jose Mourinho.

Drogba amesema kwamba mechi ya Jumapili dhidi ya Sunderland ilikuwa ya mwisho kwake akiwa mchezaji wa Chelsea, baada ya kutwaa na timu hiyo ubingwa mara nne lakini pia safari hii akapata pia medali ya Kombe la Ligi.

“Nataka kucheza walau msimu mmoja tena na ili kucheza soka mara kwa mara nahisi natakiwa kwenda kwenye klabu nyingine. Washabiki wote wanajua mapenzi yangu kwa Chelsea na natumaini kuwa hapa siku zijazo kwa jukumu jingine,” akasema.

Drogba anadhaniwa kwamba baadaye ataajiriwa katika benchi la ufundi baada ya kuwa na historia ndefu na nzuri na Stamford Bridge. Ndiye alichangia kwa kiasi kikubwa Chelsea kutwaa ubingwa pekee wa Ulaya kabla hajaondoka kwa mara ya kwanza London.

Mchezaji mwingine aliye njiani kuondoka ni Radamel Falcao ambaye muda wake wa mkopo na Manchester United unaisha kiangazi hiki na Man U wameamua kutomsajili. Kipengele cha mkataba wake kilitoa fursa ya Old Trafford kumsajili moja kwa moja kiangazi hiki kwa pauni zaidi ya milioni 40.

Liverpool walioaibishwa kwa kufungwa 6-1 na Stoke siku ya mwisho ya msimu wanahangaika kupata mshambuliaji kwa ajili ya msimu ujao, ambapo wapo tayari kumtoa Rickie Lambert, 33, aende Aston Villa kama sehemu ya dili la kumsajili mshambuliaji wa kati wa Villa, Christian Benteke, 24.

Arsenal wameibuka na tetesi mpya, ikielezwa kwamba wapo katika hatua za mwisho zakumsajili kiungo wa Juventus, Arturo Vidal, 28, lakini usajili wa raia huyo wa Chile utatangazwa baada ya kumalizika kwa mechi za mataifa ya Amerika, maarufu kama Copa America.

Vidal alikuwa akiwindwa na Manchester United msimu uliopita, lakini kocha Louis van Gaal alikuwa na wasiwasi juu ya utimamu wa mwili wake. Everton wanapanga kumsajili kiungo wa Wolves, Bakary Sako, 27 ili kurekebisha makosa ya msimu huu.

Chelsea wanafikiria kutoa pauni milioni 20 kwa beki wa kimataifa wa Ghana, Baba Rahman, 20, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Ujerumani ya Augsburg, wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant.

Licha ya kuwapo taarifa kwamba nafasi ya kocha Sam Allardyce anayeondoka kiangazi hiki West Ham, ingechukuliwa na mlinzi wao wa zamani, Slaven Bilic, 46, kuna tetesi kwamba wanasubiri kuona iwapo Carlo Ancelotti atafukuzwa Real Madrid ili wamshawishi ajiunge nao.

Hata hivyo, maofisa wengi wa Real Madrid wanataka abaki nao kwa msimu ujao na mingineyo, japokuwa mwenyewe anasema hana uhakika kama atabaki. Hakuambulia taji lolote msimu huu, na waliomtangulia ambao hawakupata walifutwa kazi.

Anfield nako kunatokota,ambapo baada ya Brendan Rodgers kukiri kwamba ana hali mbaya, kocha wa Borussia Dortmud anayetimka kiangazi hiki, Jurgen Klopp, 47, anapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi yake.

Kocha wa muda wa Newcastle, John Carver anatumaini kwamba atabakishwa klabuni hapo na mmiliki Mike Ashley aliyeahidi Jumapili baada ya kunusurika kushuka daraja kwamba atawekeza katika wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Leicester wanapanga kumsajili mlinzi wa zamani wa Manchester United, Tom Thorpe, 22, ambaye mkataba wake unamalizika klabuni hapo na angependa kupata muda zaidi wa kucheza katika kikosi cha kwanza kwenye timu nyingine.

Kocha wao, Nigel Pearson, amesema kwamba anataka kujielekeza kumaliza ligi msimu ujao katika nafasi za juu badala ya kuwa timu inayolenga kuepuka kushuka daraja. Msimu huu wamepambana hadi kufanikiwa, na kumaliza wakiwa katika nafasi ya 14.

Kocha wa Crystal Palace, Alan Pardew amesema anatafuta wachezaji wanne mahiri kwa ajili ya kikosi cha kwanza, baada ya kuwaongoza kutoka kushuka daraja hadi kumaliza katika anfasi ya 10 msimu huu.
Muda wa Youssouf Mulumbu, 28, katika klabu ya West Brom umekatika baada ya kocha wake, Tony Pulis kukataa kubofya kipengele cha mkataba ambacho kingeweza kumwongezea mwaka mmoja zaidi klabuni hapo.

Beki wa kushoto wa Liverpool, Glen Johnson, 30, naye anaelekea kuwa muda wake Anfield umeisha kwani mkataba wake unamalizika kiangazi hiki na hakuna yeyote aliyeanzisha mazungumzo ya mkataba mpya. Amesema anatarajia kuanza ngwe mpya katika maisha baada ya kukaa miaka sita klabuni hapo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Raila Odinga awapa ‘tano’ Arsenal

Norwich warudi Ligi Kuu