*Januzaj ajiunga na Borussia Dortmund
*Javier Hernendez aenda Bayer Leverkusen
*De Gea atua Real Madrid
*Man U wamnasa Martial kutoka Monaco
* Borini njiapanda, Jelavic ni West Ham
Hatimaye Manchester City wamekamilisha usajili wa kiungo waliyekuwa wakimsaka kwa udi na uvumba, Kevin De Bruyne kutoka Wolfsburg, kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 55.
De Bruyne, 24, amesaini mkataba wa miaka sita Etihad na anakuwa mchezaji wa nne mkubwa kusajiliwa kiangazi hiki, baada ya Raheem Sterling kutoka Liverpoo na Timu ya Taifa ya England, Fabian Delph wa Aston Villa na mchezaji wa kimataifa wa Argentina, Nicolas Otamendi aliyekuwa Valencia.
De Bruyne ni mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji, ambaye anakuwa wa pili aghali katika usajili kwa klabu za England, nyuma ya Angel Di Maria aliyesajiliwa kiangazi kilichopita na Manchester United kwa pauni milioni 59.7 kutoka Real Madrid, akashindwa kung’ara na sasa ameuzwa Paris Saint-Germain (PSG).
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini alionesha furaha yake kumpata mchezaji huyo, na alikuwa na haya ya kusema kumhusu: “Inabidi uwe na mchezaji wa kipekee ili kuboresha kikosi. Sisi hupenda mchezo wa kushambulia sana na unaovutia, kwa hiyo kusajili mchezaji kama huyu utakuwa msaada mkubwa sana kwetu. Ana kila tunachohitaji – utimamu wa mwili, akili, ufundi na mbinu zinazotakiwa uwanjani.”
De Bruyne aliyekuwa Chelsea kabla ya kutupwa kwa madai hana kiwango, amesema anataka kufika katika kilele cha mafanikio kwa maana ya kiwango cha juu cha uchezaji soka huku akiwapatia klabu yake mataji. Amepewa jezi namba 17 na aliuzwa na Chelsea Wolfsburg Januari 2014 kwa pauni milioni 16 tu na sasa thamani yake imepanda zaidi ya mara tatu.
Rekodi ya ada kubwa pia anayo Fernando Torres aliyeuzwa kwa pauni milioni 50 akitoka Liverpool kwenda Chelsea na sasa yupo Atletico Madrid; Sterling ambaye Liver walimuuza kwa pauni milioni 49 kwa City; Mesut Ozil aliyenunuliwa na Arsenal kwa pauni milioni 42.4 mwaka juzi kutoka Real Madrid.
MARTIAL WA MONACO KUTUA MAN UNITED
Manchester United wanakamilisha taratibu kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Monaco, Anthony Martial, 19, kwa pauni milioni 36.6. alikuwa pia akihusishwa na mipango ya kujiunga na Arsenal.
Mchezaji huyo ameruhusiwa na Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) kuondoka kwenye kambi ya Timu ya Taifa ya Ufaransa ili akakamilishe taratibu za kuingia Old Trafford. Martial alifunga mabao manane katika mechi 31 msimu uliopita wa Ligi Kuu nchini Ufaransa.
“Anthony Martial amemwomba kocha Didier Deschamps ruhusa ya kusafiri hadi England to kusaini mkataba na Manchester United. Kwa sababu ya mazingira ya kipekee, kocha amemruhusu na aliondoka Clairefontaine Jumatatu asubuhi na atarudi Jumanne asubuhi,” taarifa ya FFF imesema.
Martial alianza soka yake klabuni Lyon, ambapo alicheza mechi yake ya kwanza kama mchezaji wa kulipwa Desemba 2012 kabla ya kuhamia Monaco Juni, 2013. Kiangazi hiki alikuwa ameshakubali kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja hadi 2019.
FABIO BORINI KWENDA SUNDERLAND
Liverpool wamepokea pauni milioni 10 ili mshambuliaji wao, Fabio Borini, 24, ajiunge na Sunderland japokuwa bado hakuna uhakika iwapo hilo litatokea. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia alipata kukaa Sunderland kwa mkopo msimu wa 2013/14 ambapo alifunga mabao saba muhimu katika mechi 32.
Hata hivyo, baada ya muda huo alikataa kujiunga na Sunderland moja kwa moja. Mezani kwa Liverpool, kulikuwapo ofa kutoka klabu za Inter Milan na Fiorentina za Italia na Watford ya England, lakini hazikukubaliwa na klabu hiyo ya Anfield.
Ofa ya Inter ilikuwa pauni milioni sita, ya Watford pauni milioni saba wakati ya Fiorentina haijulikani vyema. Uamuzi wa mwisho juu ya wapi anakwenda ni juu ya mchezaji mwenyewe, vinginevyo atabaki Anfield.
Borini ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, ambapo aliwalipa Roma pauni milioni 11 mnamo Julai, 2012, baada ya kupata kufanya naye kazi katika klabu za Chelsea na Swansea miaka iliyotangulia. Amefunga mabao 38 kwa Liverpool tangu ajiunge nao.
NIKICA JELAVIC HUYOO WEST HAM
West Ham wamekubaliwa maombi yao ya kumsajili mshambuliaji wa Hull walioshuka daraja, Nikica Jelavic kwa pauni milioni tatu hivi. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ukraine alikuwa jijini London Jumatatu hii kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.
Jelavic, 30, alifunga mabao 12 katika mechi 50 alizochezea Hull katika msimu ambao waliishia kushuka daraja. Ataungana na bosi wake wa zamani wa Timu ya Taifa ya Croatia, Slaven Bilic, aliyefundisha timu hiyo tangu 2006 hadi 2012.
Wote ni raia wa taifa hilo, ambapo Jelavic alipata kuchezea Rangers kabla ya kujiunga na Everton alikoondoka Januari mwaka jana.
Kiungo wa Napoli nchini Italia, Mholanzi Jonathan de Guzman, 27, anatarajiwa kurejea England kwa ajili ya kujiunga na Bournemouth kwa mkopo wa msimu mzima. Winga wa Nigeria, Victor Moses, 24, anatarajiwa kujiunga na West Ham kwa mkopo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Comments
Loading…