Chelsea na Liverpool wamepata mapigo baada ya washambuliaji wao, Diego Costa na Daniel Sturridge kuumia wakiwa na timu za mataifa yao.
Costa (25) aliumia akiwa na Timu ya Taifa ya Hispania iliyofungwa 1-0 na Ufaransa kwenye mchezo wa kirafiki, ambapo alitoka dakika ya 67 na sasa amejitoa kwenye mechi ijayo dhidi ya Macedonia.
Chelsea wanasubiri kwa hofu matokeo ya vipimo kutoka Hispania lakini pia vya kwao wenyewe, ili wajue iwapo mshambuliaji wao namba moja aliyewafungia mabao manne katika mechi tatu za Ligi Kuu ya England atakaa nje ya dimba kwa muda gani.
Wikiendi ijayo Chelsea wanakabiliana na Swansea ambao waliwapiga Manchester United 2-1 dimbani Old Trafford. Mchezaji huyo aliumia kidogo pia mazoezini kabla ya mechi ya Chelsea dhidi ya Everton, lakini baadaye alionekana kuwa fiti.
Alianza kuumia mara kwa mara msimu uliopita akichezea Atletico Madrid na watu wa Chelsea lazima wawe na wasiwasi, kwani ndiye tegemeo kubwa katika kupachika mabao, ambapo namba mbili wake ni Didier Drogba.
Naye Sturridge wa Liverpool aliumia akiwa mazoezini kujiandaa kwa mechi ya kufuzu kwa michuano ya Euro 2016 dhidi ya Uswisi Jumatatu hii. Amejiondoa kwenye kikosi hicho tayari.
Sturridge (25) ndiye tegemeo la uhakika kwa Liverpool kwenye ushambuliaji, ambapo msimu uliopita alishirikiana vyema na Luis Suarez aliyehamia Barcelona kiangazi hiki, wakawezesha Liverpool kushika nafasi ya pili EPL.
Kwa sasa anacheza na Raheem Sterling lakini pia kuna mchezaji mpya, Mario Balotelli kutoka AC Milan na Rickie Lambert aliyesajiliwa kutoka Swansea, katika jitihada za kuziba pengo la Suarez aliyekuwa mfungaji na mchezaji bora EPL msimu uliopita.
Sturridge mwenyewe amesema kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba ameumizwa moyo na kuumia kwake, kwani hakuna kitu kibaya zaidi ya kuumia lakini ana matumaini kwamba atapona mapema ili aipiganie timu yake ya Liverpool.
Sturridge amefunga mabao matano katika mechi 16 alizochezea taifa lake na katika mechi za mazoezi ziarani kwa Liverpool aliacha wachezaji wenzake kwa ajili ya matibabu baada ya kuumia.
Kocha wa England, Roy Hodgson sasa amebakiwa na nahodha Wayne Rooney, Lambert na mshambuliaji mpya wa Arsenal, Danny Welbeck kwa ajili ya mechi za kufuzu. Beki wa kati wa Chelsea, Gary Cahil anasema emchi ijayo kwa England ni ngumu katika kundi linalohusisha pia timu za mataifa ya Slovenia, Estonia, Lithuania na San Marino.
Comments
Loading…