in ,

Corona inavyoharibu utamu wa michezo

Hapana shaka moja ya kitu ambacho huwa kinawaleta kwa pamoja watu wote ni michezo. Michezo ni mkusanyiko wa hisia mbalimbali unazozijua duniani. Hisia hizi hukusanyika na kukutana kwenye kitu kinachoitwa michezo.

Furaha huungana na machozi, mdomo utacheza, macho hutoa machozi, Mioyo kuna wakati hukasirika, kuna wakati mioyo hiyo hiyo hutabasamu kwa sababu ya michezo.

Undugu huanza kujengwa hapa, biashara huimarika hapa, umoja huongezeka hapa, michezo kuna wakati huwaleta kwa pamoja wanaopigana na kushikana mikono kwa pamoja huku wakitabasamu.

Hisia hizi zinaanza kupotea taratibu kwenye michezo kwa sasa kwa sababu ya virusi vya Corona. Virusi ambavyo vilianzia kwenye bara la Asia na kusambaaa kwenye mabara yote duniani kasoro bara moja la Antarctica.

Kila unapofika lazima uje na mvua ya majonzi. Wenzetu China mpaka sasa wanaumia sana na wanalia kila uchwao kwa sababu tu ya ugonhljwa huu hatari duniani.

Achana na vifo zaidi ya elfu kumi vilivyotokea kwenye nchi ya China. Virusi vya Corona vimesababisha mpaka vilio kwenye michezo mbalimbali nchini humo. Serikali mpaka sasa hivi imezuia mkusanyiko wa watu kuanzia watano.

Serikali ya nchini China imeenda mbali zaidi na kuzuia mashindano yote ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika nchini humo. Hapa ndipo ladha ya mbio za magari yanayoondoka kwa kasi duniani inapopungua.

China walipewa Grandprix katika jiji la Shanghai, yani Shanghai Grandprix, ambayo ingefanyika mwezi wa nne. Hata hivyo mamlaka inayosimamia mchezo huu, wametangaza kutofanyika kwa Grandprix hiyo nchini China kwa sababu ya Coronavirus.

Coronavirus imejipenyeza kwenye mpira tena. Mchezo unaopendwa zaidi duniani. Italy ndiyo mhanga mkubwa kwa sasa baada ya kuripotiwa kuwepo kwa ugonjwa huo kaskazini mwa nchi hiyo.

Hali ambayo ilisababisha wiki iliyopita baadhi ya michezo kuchezwa bila uwepo kwa mashabiki. Mfano mchezo wa UEFA EUROPA LEAGUE kati ya Intermilan na Ludogorets ulichezwa bila mashabiki.

Achana na hilo. Michezo ambayo ilitazamiwa kuchezwa mwishoni mwa juma hili nayo imetangazwa kutochezwa tena na kusogezwa mbele mpaka mwezi wa tano.

Kwa hiyo tunaenda kutazama ligi kuu ya Italy “Seria A” mwezi wa tano kutokana na ugonjwa huu wa Corona, ugonjwa ambao umeleta huzuni kwenye sekta zote kuanzia uchumi mpaka michezo.

Ligi kuu ya England nayo inayo hatari sana ya kusimamishwa kama kutaendelea kuripotiwa matukio mengi ya ugonjwa huu wa Corona. Tayari ugonjwa huu umeshaingia nchini humo na watu kadhaa wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Mwaka huu wa 2020, ni mwaka ambao kutafanyika mashindano ya Olympic mjini Tokyo, Japan. Lakini mpaka sasa hivi michezo ya kufuzu mashindano hayo imeshindwa kuendelea kwa ufasaha kwa sababu ya ugonjwa huu.

Mwaka 2022 kutakuwepo na michezo ya kombe la dunia nchini Qatar. Na michezo ya kufuzu mashindano imeshaanza kuchezwa na kuna hatari michezo hii ikaahirishwa kutokana na hofu ya ugonjwa huu.

Jana Ferrari wametangaza kutokupeleka timu yao kama hakutakuwepo na taarifa rasmi ya Grandprix ya kwanza inayochezwa Australia ambayo itaitwa Australian Grandprix.

Australia ni moja ya nchi ambayo imeripotiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huu, na ni nchi ambayo mashindano ya langalanga msimu huu yanaanzia huko hivo Kujenga hofu kwa timu ambazo zinashiriki michuano hii.

Mpaka sasa hakuna dawa iliyozunduliwa kwa ajili ya kuponesha ugonjwa huu. Mpaka sasa hivi hatujui ni lini utakwishwa . Ugonjwa ambao umekuja kusimamisha kila aina ya furaha ambayo tulikuwa tumezoea kuwa nayo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Tuanze kumuonea huruma kwanza Ajib au Yanga ?

mchezo wa soka, mahasimu wakiwa uwanjani

Kariakoo Dabi: Jua chanzo, ukali wake