in , , ,

Clattenburg asafishwa kashfa ya Chelsea

*Kibao chamgeukia John Obi Mikel

Hatimaye mwamuzi Mark Clattenburg aliyedaiwa kutumia lugha ya kibaguzi dhidi ya wachezaji wa Chelsea amesafishwa rasmi.
Chelsea waliwasilisha malalamiko rasmi dhidi ya mwamuzi huyo, wakidai aliwatukana kibaguzi John Obi Mikel na Juan Mata siku timu yao ilipofungwa na Manchester United.
Hata hivyo, baadaye Chelsea waliokuwa chini ya kocha Roberto Di Matteo ilifuta malalamiko kumhusu Mata, wakidai hawakuwa na ushahidi.
Polisi walifungua jalada na kuanza uchunguzi, lakini walilifunga hivi karibuni baada ya kutotokea mlalamikaji na wao kukosa ushahidi dhidi ya Clattenburg.
Mwamuzi huyo wa kimataifa anayetarajiwa kuchezesha mechi za Kombe la Dunia nchini Brazil, amekosa wikiendi tatu za kuchezesha, wakati akichunguzwa.
Chama cha Soka (FA) cha Uingereza kimetangaza kufuta rasmi mashitaka hayo na kumsafisha Clattenburg, huku kibao kikimgeukia Obi.
Siku ya tukio, Obi anadaiwa kumvamia Clattenburg kwenye chumba cha waamuzi akiwa na kocha Di Matteo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Sam Wallace baada ya mechi, wakimshinikiza awaombe radhi.
Obi anadaiwa kumtishia kumpiga buti, lakini Clattenburg alikataa madai hayo, na kushitushwa na taarifa kwamba alitoa lugha ya kibaguzi.
Inadhaniwa mwamuzi alijumuisha tukio hilo kwenye ripoti yake, na sasa Obi ameshitakiwa rasmi kwa kosa la mwenendo mbaya.
FA inasema kwamba haiamini kwamba kuna kesi yoyote dhidi ya Clattenburg, aliyedaiwa kumwita Obi ‘nyani’.
“FA imemaliza uchunguzi wake juu ya madai ya mwamuzi kutumia lugha isiyofaa Oktoba 28 katika mchezo kati ya Chelsea na Manchester United, hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya Clattenburg,” FA inasema katika taarifa yake.
Uamuzi huo umetangazwa wakati Chelsea wakimpokea kocha mpya, Rafael Benitez, siku moja baada ya kufukuzwa kazi Di Matteo kutokana na timu kufanya vibaya,
Clattenburg alihojiwa na FA Novemba 12, ambapo wachezaji kadhaa wa Chelsea, akiwamo Ashley Cole walihojiwa na hapakuwapo ukweli wowote kwenye madai ya klabu hiyo.
“Ushahidi wa madai ulitoka kwa shahidi mmoja, Ramires, ambaye lugha yake ya kwanza si Kiingereza. Huyu anasema alitaharuki akitaka ufafanuzi kutoka kwa John Obi Mikel ili ajue nini mwamuzi alikuwa amesema.
“John Obi Mikel aliyekuwa akizungumziwa na mwamuzi, alikuwa karibu zaidi naye kuliko Ramires na hakusikia kile anachodaiwa kuambiwa.
“Mashahidi wengine watatu ambao ni waamuzi wanaosikia kila kitu kinachosemwa na mwamuzi wanakataa kwamba mwamuzi alitoa maneno yasiyofaa.
“Kwenye mkanda wa video hakuna chochote kinachoweza kutumika kuunga mkono tuhuma dhidi ya Clattenburg. Kwa ujumla ni kwamba wachezaji wengine wawili ambao lugha yao ya kwanza ni Kiingereza na walikuwa mbali kidogo, hawakusikia chochote kilicho kinyume,” FA inasema.
Uamuzi huo, kama nilivyoandika wiki chache zilizopita, unawaweka Chelsea katika wakati mgumu, kwani wameshindwa kuthibitisha tuhuma nzito walizotoa.
Clattenburg (37) anasifika kwa kazi nzuri duniani, na Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson alionesha wasiwasi tangu awali juu ya tuhuma dhidi ya mwamuzi huyo.
Arsene Wenger wa Arsenal naye alisema Chelsea walipotoka kwa kutoa madai hayo hadharani, kwani wangeweza kwenda nayo taratibu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Shangwe Arsenal kufuzu Ulaya

Ni Benitez Chelsea