*West Ham, Swansea nao washinda
*Newcastle, Villa, Saints, Brom sare
Chelsea wamepata ushindi wa pili mfululizo, baada ya kuwachapa Leicester City 2-0 katika mechi waliyobanwa kwa zaidi ya saa nzima bila kuliona lango la wapinzani wao, wakicheza katika dimba la Stamford Bridge.
Kocha Jose Mourinho aliyeanza ligi kwa kuwasifu wachezaji wake kwamba ni kikosi imara, aliona Diego Costa kifunga tena bao kwenye mechi yake ya pili ya ligi, na bao lilikuja dakika ya 63 kabla ya Eden Hazard kupachika la pili dakika ya 77.
Golini alimwanzisha Thibaut Courtois kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza, Petr Cech akibaki kwenye benchi, ambapo klabu kadhaa za Ulaya zinafikiria kumchukua, huku Mourinho akimsifu kwa utulivu wake, akisema anaamini atakubali hali halisi na kubaki Chelsea.
Mkongwe wa Stamford Bridge aliyekuwa ameondoka kwa miaka miwili, Didier Droba alichukua nafasi ya Costa dakika 10 kabla ya mpira kumalizika.
West Ham walimpa raha kocha wao Sam Allardyce, aliyekuwa ameanza kujikuta katika shinikizo, kwani waliwachapa wenyeji wenzao wa London, Crystal Palace kwa mabao 3-1.
Mabao ya West Ham yalifungwa na Mauro Zárate, Mauro Zárate na Carlton Cole, wakati la Palace lilifungwa na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Marouane Chamakh.
Swansea walioanza ligi kwa kuwacharaza Manchester United nyumbani Old Trafford, wameendelea kushinda, ambapo Jumamosi hii wamewafunga Burnley 1-0, bao likitiwa kimiani na Nathan Dyer dakika ya 23.
Katika mechi ya mchana, Astona Villa na Newcastle waligawana pointi moja, baada ya kwenda suluhu. Beki wa kati wa Newcastle, Mike Williamson alipewa kadi nyekundu baada ya kuwachezea vibaya mshambuliaji Darren Bent na kiungo Fabien Delph katika kipindi cha dakika nne tu.
Katika mechi nyingine Southampton waliowaalika West Bromwich Albion kwenye dimba la St Mary’s nao walishindwa kufungana. Saints waliambulia pointi ya kwanza chini ya kocha Ronald Koeman Jumamosi hii, ambapo ngome ya Baggies ilikataa kabisa kufunguka.
Comments
Loading…