*Spurs wapanda, wachuana na Arsenal
Vita ya nafasi nne za kwanza Ligi Kuu ya England (EPL) imekolea, baada ya Tottenham Hotspurs kuwaondoa Chelsea katika nafasi ya tatu.
Spurs waliokuwa wageni wa West Ham United Jumatatu hii, walielekea kuzama robo saa ya mwisho ya mchezo, wakiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Hata hivyo, walifanikiwa kusawazisha kabla ya mfungaji wao mahiri aliye kwenye chati, Gareth Bale kufunga kwa kiki ya mbali katika dakika ya 90.
Lilikuwa bao la pili la Bale katika mchezo huo, kwani ndiye alifungua kitabu dakika ya 13, kabla ya Andy Carroll kusawazisha kwa penati dakika ya 25.
Joe Cole aliwafungia West Ham bao la pili na Gylfi Sigurdsson akasawazisha dakika ya 76, ikadhaniwa wawili hao wangegawana pointi moja moja.
Kwa goli la Bale, ambalo ni la nane katika mechi sita, Spurs wamepanda hadi nafasi ya tatu na kuwashusha Chelsea waliokuwa hapo kwa muda mrefu.
Chelsea wanashuka kwa sababu Jumapili walifungwa na Manchester City 2-0, ambapo kocha Rafa Benitez alisema kabla kwamba iwapo wangepoteza mchezo huo, huenda ikawawia vigumu kushika nafasi ya pili.
Spurs wamefikisha pointi 51, wakiwaacha Chelsea na pointi 49, Arsenal pointi 47 na Everton pointi 42. Manchester City wana pointi 56 wakati vinara wa ligi Manchester United wamefikisha pointi 68 na timu zote zimebakisha mechi 11.
Jumapili Spurs wanawakaribisha Arsenal, katika mechi ngumu ya klabu za London Kaskazini zinazokabana koo kuwania nafasi za uwakilishi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Comments
Loading…