*QPR wawaosha 1-0 Stramford Bridge*Liverpool sasa ni mwendo wa ushindi*Newcaastle bila Demba Ba kilio tupu
Unaweza kusema mende ameangusha kabati, kwa timu inayokalia mkia wa Ligi Kuu ya England, Queen Park Rangers (QPR) kuwafunga Chelsea. Alikuwa winga wa zamani wa Chelsea, Shaun Wright-Phillips aliyetokea benchi na kufunga bao pekee katika mechi hiyo, na kumwacha kocha Rafa Benitez na wachezaji wake wakiwa hawaamini. Chelsea walikuwa wakicheza nyumbani Stamford Bridge, na Benitez alipumzisha nyota kadhaa, wakiwamo Ashley Cole na Juan Mata. Wright-Philips aliingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Junior Hoilett aliyeumia, alifunga bao hilo dakika ya 78 na jitihada za Chelsea kusawazisha hazikuzaa matunda. Nusura Chelsea wabaki wachezaji 10 uwanjani dakika za mwanzo, baada ya Marko Marin aliyecheza kwa mara ya kwanza Jumatano hii kumfanyia rafu mbaya kiungo Stephen Mbia dakika ya nne. Marin na Frank Lampard walijaribu kucheza vyema, lakini kwa ujumla Chelsea walishindwa kuuvuka ukuta mgumu wa QPR ulioongozwa na Ryan Nielsen na Clint Hill. Kocha Harry Redknapp hakutarajia ushindi huo, kwani tangu siku moja kabla alikuwa akiwasifu Chelsea, akisema kocha Benitez amekuta kikosi imara. Redknapp alichukua timu ikiwa mkiani hapo hapo na ilifanikiwa kupata ushindi wa kwanza katika mzunguko wa 17. Pamoja na ushindi huo, QPR bado wapo mkiani, wakiwa na pointi 13 sawa na Reading, pointi tano nyuma ya Wigan na Southampton. Mechi yao ijayo ni dhidi ya West Bromwich Albion katika Kombe la FA Jumamosi hii. Chelsea wanashika nafasi ya nne. Liverpool wameendeleza mtiririko wa ushindi kwa kuwakandika Sunderland mabao 3-0. Wakicheza nyumbani Anfield, Liverpool walijisogeza hadi nafasi nzuri ya nane, kwa bao la kinda Raheem Sterling na mawili ya nyota wao, Luis Suarez. Nyota wao huyo wa timu ya taifa ya Uruguay amefikisha mabao 15 katika ligi kuu msimu huu. Ushindi huo ulishuhudiwa jukwaani na mshambuliaji wao mpya kutoka Chelsea, Daniel Sturridge. Sunderland wapo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi. Newcastle waliompoteza mmoja wa wafungaji bora msimu huu, Demba Ba, walipoteza mechi dhidi ya Everton, licha ya kupata bao dakika ya pili tu ya mchezo. Papis Cisse alifunga bao hilo nyumbani St James’ Park na kuwapa imani washabiki kwamba hapangekuwapo pengo kuondoka kwa Msenegali mwenzake Ba anayejiunga Chelsea. Hata hivyo Everton walitulia uwanjani, wakajipanga na kupokea maelekezo kutoka kwa mwalimu wao, David Moyes, wakafanikiwa kusawazisha na kuongeza bao la ushindi. Goli la kusawazisha lilipatikana kwa kombora kali la Leighton Baines baada ya Marouane Fellaini kuchezewa rafu ndogo ambayo huenda haingestahili mpira wa adhabu. Victor Anichebe aliwafungia Everton bao la ushindi. Dakika za mwisho zilitawaliwa na kila aina ya ushindani, Alan Pardew akijaribu kuwaokoa Newcastle kutumbukia eneo la kushuka daraja. Kwa matokeo hayo, Everton wamewashusha Arsenal kutoka nafasi ya tano hadi ya sita, wakati Newcastle wanashika nafasi ya 15. |
Comments
Loading…