Chelsea wamefanya vyema kwenye nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Europa ugenini.
Wakicheza nchini Uswisi, Chelsea waliosheheni nyota wengi, walifanikiwa kuwafunga Basel 2-1, japokuwa ilibidi wafanye kazi ya ziada kupata matokeo hayo.
Rafa Benitez, kocha mwenye sera za kuzungusha kikosi chake badala ya kuwa na ‘First 11’, Alhamisi hii aliwaanzisha wakongwe wao – John Terry, Ashley Cole, Frank Lampard, Fernando Torres na chipukizi Victor Moses, Eden Hazard kabla ya Juan Mata kuingia kipindi cha pili.
Alikuwa Mnigeria Victor Moses aliyempa Benitez na washabiki wa Chelsea furaha, kwa kufunga bao la kwanza mapema dakika ya 12.
Moses aliunganisha wavuni mpira wa kona wa Lampard, ulioelekea kumgusa Branislav Ivanovic au kwamba aliwapoteza maboya mabeki wa Basel, na Moses hakufanya ajizi akacheka na nyavu.
Basel wanaocheza pasi fupi fupi walitokea kuwa tishio, wakishitukiza kila mara, lakini walionekana kuwa na tatizo la kumalizia, hasa kwenye krosi ndefu ambazo ama ziliishia mkononi mwa Petr Cech au mpira uliishia kuwa mwingi na kutoka nje.
Basel walifanikiwa kusawazisha kwa penati dakika ya 88 kupitia kwa Schar. Ilitolewa baada ya beki Cesar Azpilicueta kucheza rafu. Schar alimpeleka Cech kulia, akatikisa nyavu katikati chini.
Hata hivyo, wakati wengi wakichukulia mechi ingeisha kwa sare, Chelsea walipata mpira wa adhabu ndogo uliopigwa vyema na David Luiz, ukaupita ukuta wa Basel na kumshinda nguvu kipa Summer, ukajaa wavuni.
Chelsea sasa watawakaribisha Basel Stamford Bridge kwenye mechi ya kukata mzizi wa fitna, ambapo historia inaonesha Chelsea hawajapata kushindwa hapo katika mashindano haya, wakati Basel haijui ushindi ukoje katika ardhi ya Uingereza.
Katika nusu fainali nyingine, Egemen Korkmaz aliyefunga bao pekee kwa kichwa kwenye mechi ya nyumbani, aliwaweka pazuri Fenerbahce dhidi ya Benfica. Timu zitakazocheza fainali zitajulikana baada ya marudiano Alhamisi ijayo Uingereza na Ureno.
Comments
Loading…