*Vermaelen Man U na Cleverly Arsenal ?
*Liverpool rada kwa Moreno, Rodriguez
*Kisa cha Fabregas kukataliwa hadharani
Tetesi za usajili katika Ligi Kuu ya England (EPL) zinaendelea kuchomoka na makubwa, ambapo Chelsea wanadaiwa kugonga Old Trafford wakimtaka Wayne Rooney.
Baada ya kumpata Cesc Fabregas kwa pauni milioni 33, Jose Mourinho amefungua kitita cha pauni milioni 40 akitaka dili la Rooney likamilike.
Licha ya ukame wake wa mabao kwenye Kombe la Dunia, Chelsea wanadhani kwamba Rooney atawafaa.
Inaelezwa kwamba Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alimwambia Mourinho kwamba alikuwa wazi kupokea ofa, ndipo Mourinho akaweka dau mezani.
Van Gaal anadaiwa kuwamini kwamba Rooney anaanza kupitwa na wakati na baada ya Chelsea kumkosa miezi 12 iliyopita, safari hii Man U wamewaambia wanafikiria ombi lao.
Chelsea wakimpata Rooney, watawauza Demba Ba na Fernando Torres ili kupunguza gharama za mishahara kama walivyokwishapunguza zaidi kwa kuwaacha Ashley Cole na Frank Lampard.
United wakipata kitita hicho cha pauni milioni 40 inasemekana watamsajili kiungo mkabaji na beki wa kati wa Timu ya Taifa ya Uholanzi na Ajax, Daley Blind (24) ambaye Van Gaal anaamini atafanya vitu adimu Old Trafford.
VERMAELEN KUBADILISHWA NA CLEVERLY
Lisemwalo lipo, kama halipo laja. Baada ya habari za Nahodha wa Arsenal, Thomas Vermaelen kukubali kimsingi kuhamia Manchester United kukanushwa, bado zinavuma zaidi.
Safari hii zimeongezewa kionjo kipya kwamba Kocha Arsene Wenger anafikria kumwachia Vermaelen kwa pauni milioni 10 halafu aongezwe na Tom Cleverly.
Vermaelen anataka kufuata nyayo za nahodha aliyemtangulia, Robin van Persie kwa sababu hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal ambapo nafasi yake imechukuliwa na Per Metersacker na Laurent Konscielny.
Cleverly (24) kwa upande wake angependa kundoka United kwa sababu kuna baadhi ya washabiki hawampendi na wamepata kumtukana waziwazi na hadi sasa inadaiwa hajawasamehe.
Haijajulikana washabiki wa Arsenal watapokea vipi uamuzi wa timu yao kukataa kumsajili Fabregas na sasa wanamchukua Cleverly.
Hata hivyo, Fabregas angewagharimu pauni milioni 30, lakini sasa wataondokana na Vermaelen na mshahara wake na kupata pauni milioni 10 juu na fursa ya kumjaribu Cleverly ambaye wanaweza kumuuza baadaye.
RADA ZA LIVERPOOL KWA RODRIGUEZ
Liverpool wanafikiria kupeleka tena dau katika Klabu ya Wolfsburg ili kumsajili beki ao wa kushoto, Ricardo Rodriguez ikiwa watakwama kumsajili Alberto Moreno.
Kocha Brendan Rodgers amekuwa akimfuatilia nyota huyo wa Sevilla kwa miezi kadhaa, akakaribia kumsajili kabla ya dili kugonga mwamba.
Klabu hiyo ya La Liga inadaiwa kuongeza dau ambalo mchezaji huyo anaweza kuwekewa na sasa wanataka kwenye pauni milioni 20 kwa mchezaji mwenye umri wamiaka 21.
SABABU ZA FABREGAS KUKATALIWA
Manchester City, Man United na Arsenal waliamua kumkataa Cesc Fabregas kwa maelezo kwamba nafasi yake imejaa.
Man U walikuwa na nia ya kumchukua kiungo huyo kutoka Barcelona, lakini kocha Louis van Gaal akasema kwamba madhali Juan Mata yupo, hawana sababu ya kumchukua Mhispania mwenzake huyo.
Man City wanasema wangemchukua iwapo wangekuwa na uhakika Yaya Toure angeondoka baada ya kutikisa kiberiti kwa madai haheshimiwi.
Fabregas mwenyewe anasema alizungumza na kocha Wenger mapema na mwalimu wake huyo wa zamani alimwambia atasugua benchi.
Fabregas anasema Wenger alimwambia angependa sana kumsajili ila awe tayari kutocheza kwa sababu ya uwapo wa Mesut Ozil ambaye anampa kipaumbele. Fabregas anasema alielewa, akafikiria vipaumbele vyake vitatu na kupata jibu la alichotaka kwa Mourinho wa Chelsea, akamwaga wino.
Comments
Loading…