*Wahusishwa na Vitesse ya Uholanzi
*Waizuia kutwaa ubingwa isiingie UCL
Klabu ya Chelsea imeanza kuchunguzwa juu ya uhusiano wake na klabu ya Vitesse Arnhem ya Uholanzi.
Uchunguzi wa awali unafanywa na Chama cha Soka (FA) cha Uholanzi, ambapo pamekuwapo madai kwamba kuna umiliki wa pamoja na Chelsea wamekuwa wakizuia Vitesse kutwaa ubingwa huko.
Klabu mbili hizo zina uhusiano wa karibu sana, ikiwa ni pamoja na Chelsea kupeleka wachezaji wake huko kwa mkopo.
Vitesse wanadaiwa kujaribu kuchupa ili wapande juu na kutwaa ubingwa lakini wanazuiwa kinamna na Chelsea ili wasije kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Sheria za Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) zinakataza timu zinazo chini ya umiliki mmoja kushiriki mashindano ya aina moja zote. Pamoja na mambo mengine, umiliki wa Vitesse unachunguzwa.
Mmoja wa wanahisa wakubwa wa zamani wa Vitesse, Merab Jordania amebainisha kwamba Chelsea wamekuwa wakiwafisha moyo Vitesse kutwaa ubingwa wa Eredivisie ili kuepuka kushiriki UCL.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich ana uhusiano wa karibu na mmiliki wa sasa wa Vitesse, Alexander Chigrinsky.
Wachezaji wa Chelsea, Lucas Piazon, Bertrand Traore, Patrick van Aanholt na Christian Atsu kwa sasa wapo kwa mkopo Vitesse, ambapo Chelsea wanasema lengo lao ni kuwapa wachezaji hao wadogo uzoefu.
Mshambuliaji Gael Kakuta (22) naye alikuwa Vitesse msimu uliopita kwa mkopo kabla ya kuitwa London na kisha kupelekwa Laziom Italia kwa mkopo pia.
Chelsea pia ilimwita mlinzi wake Sam Hutchinson (24) aliyekuwa kwa mkopo huko Vitesse na kumpeleka Sheffield Wednesday ya England kwa mkopo pia.
Vitesse kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ya huko, lakini wameshinda mechi tatutu kati ya 10 zilizopita.
Julai Mkurugenzi wa Michezo wa Ajax ya Uholanzi, Marc Overmars alisema kwamba klabu yake ilizuiwa kufanya mazungumzo na kiungo wa Vitesse, Marco van Ginkel juu ya uwezekano wa kuhamia Ajax, sababu iliyotolewa ikiwa ni mkono wa Chelsea hapo.
Na kweli, Van Ginkel (21) alikuja kusajiliwa katika mkataba wa miaka mitano na Chelsea kwa ada ambayo haikubainishwa, lakini hadi sasa amecheza mechi nne tu kwenye kikosi cha kwanza kwani aliumia mguu Septemba.
Comments
Loading…