*Watakipiga na Benfica jijini Amsterdam
Ulikuwa usiku wa ushindi wa 3-1 kwa timu zilizoingia fainali ya Ligi ya Europa, Chelsea wakiwafunga FC Basel na Benfica wakiwaangamiza Fenerbahcle.
Timu hizo mbili zitakwaana kwenye fainali ya ligi hiyo ndogo ya Ulaya itakayofanyika Amsterdam, Uholanzi Mei 15. Kocha wa muda wa Chelsea, Rafa Benitez amezidi kukata ngebe za wapinzani wake, kwa kuandika rekodi muhimu katika fani yake, kuingiza timu fainali.
Benitez anayeondoka mwisho wa msimu huu baada ya kuwaongoza Chelsea tangu Roberto Di Matteo alipofutwa kazi, alimwanzisha Mhispania mwenzake, Fernando Torresi aliyekuwa akilichachafya lango la Basel na kuwa na kosa kosa nyingi, kabla ya kuja kupata bao la kusawazisha muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili.
Basel walifunga kwa kiki ya mwisho ya kipindi cha kwanza, baada ya gonga nzuri iliyoishia kwa Mohamed Salah kumtungua kipa Petr Cech, baada pia ya kuwa amemkosakosa awali.
Hata hivyo, Chelsea waliingia kipindi cha pili kama mbogo waliojeruhiwa, ambapo baada ya kusawazisha, Victor Moses alifunga bao kama la Torres na David Luiz alifunga jingine la kuvutia. Luiz ndiye alifunga lile la ushindi kwenye nusu fainali ya kwanza nchini Uswisi, kwa kiki ya mwisho ya mechi wiki iliyopita.
Ushindi huo unawafikisha Chelsea kwenye kipute cha fainali, ikiwa ni kupoza majeraha ya kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo walivunja rekodi ya kuwa mabingwa watetezi waliotolewa katika hatua ya makundi.
Watakabiliana na Benfica ya Ureno ambao Alhamisi hii walishuhudia Oscar Cardozo akiwafungia mabao mawili dhidi ya Fenerbahce jijini Lisbon. Benfica walikuwa nyuma kwa bao 1-0 waliloshinda wapinzani wao wiki iliyopita. Bao jingine la Benfica lilifungwa na Nicolas Gaitan aliyefungua kitabu cha mabao.
Fenerbahce walijibu mapigo kupitia mchezaji wa zamani wa Liverpoo, Dirk Kuyt kwa penati na kuwa bao muhimu la ugenini, lakini halikuwafaa chochote, kwani Cardozo aliondoa udhia wote kwa kufunga mawili.
Chelsea ndiyo timu pekee ya Uingereza iliyobaki kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu, na pia wanafukuzia nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu, ili kupata uwakilishi Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, na wamekuwa na ratiba ngumu ya mechi.
Comments
Loading…