Chelsea, Arsenal wachovu
*Spurs, Man United waendelea kutakata
*Everton, City na QPR bado kigugumizi
Mzunguko wa 15 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umetoa mshituko, Chelsea na Arsenal wakiambulia kipigo kisichotarajiwa.
Rafa Benitez anakuwa kocha wa kwanza Chelsea kukosa ushindi katika mechi tatu za mwanzo tangu enzi za Gianluca Vialli.
Kadhalika, Chelsea wameweka rekodi ya kutoshinda mechi saba za EPL mfululizo, hii ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1995.
Chelsea waliadabishwa na West Ham United walio chini ya Sam Allardyce na ambao kwa siku za karibuni hawakuwa fiti kimchezo, wakipoteana.
Chelsea walipoteza uongozi wa bao moja la Juan Mata alilofunga dakika ya 13, na kuruhusu mabao matatu dhidi yao, kikawa kichapo kikubwa na cha aibu.
Maisha yameanza vibaya kwa Benitez, kwani aliambulia sare mbili kabla ya kipondo hiki, huku washabiki wa Chelsea wakimzomea na kutoa kejeli; “unafukuzwa asubuhi” na “kuna Di Matteo mmoja tu”, wakidhihirisha hasira yao kwa Roman Abramovich kumfukuza Mtaliano huyo na kumwajiri Mhispania mwenye uhasimu nao kutokana na kuwa kwake Liverpool muda mrefu.
Bila shaka Allardyce aliwapa maelekezo vijana wake wakati wa mapumziko, kwani waliporejea, Carlton Cole, Mohamed Diame na Modibo Maiga walitumbukiza mabao kimiani, wakiwaacha Chelsea wakihamaki.
Huu ndio mwanzo mbaya zaidi wa msimu kwa Chelsea ya Abramovich na sasa wanasubiri Jumatano shughuli ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, watakapocheza na Nordsjaelland.
Wakati mgeni Benitez akiugulia kichapo, mkongwe Arsene Wenger amekosa majibu ya maswali yake ya katikati ya wiki, kwa kuongezewa mzigo mwingine.
Washika Bunduki wa London wanaelekea kujielekeza wenyewe silaha hizo, pale Swansea City walipowafyatua kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Emirates.
Ilikuwa kana kwamba Arsenal wanapata sare walizozizea msimu huu, lakini dakika mbili za mwisho wa mechi zilibadili kila kitu.
Mwiba ambao Arsenal hawatausahau ni Mhispania Miguel Michu aliyeyapachika dakika ya 88 na ya 90, na kuwafanya Swansea waondoke kifua mbele, Arsenal wakibaki kama waliomwagiwa maji.
Arsenal waliadhirika wakati golikipa Wojciech Szczesny akijiuliza bao la kwanza lilivyoingia, wenzake nao wakitafakari jinsi ya kulirudisha.
Baada ya kushindwa kuona lango kwa dakika zote 88, Michu alimtazama tena Szeczesny na kuweka mpira kimiani, Mpolishi huyo akikosa la kufanya.
Upande mwingine, jirani za Arsenal, Tottenham Hotspurs waliwachambua wenzao wa London, Fulham kwa mabao 3-0, wakimwacha kocha wao, Andre Villas-Boas na furaha isiyo kifani.
Spurs walifunga kupitia Jermain Defoe aliyetikisa nyavu mara mbili na jingine likifungwa na Raniere Sandro.
Gareth Bale anayeng’ara na kupigiwa chapuo la kwenda Real Madrid, alilimwa kadi ya njano kwa mechi ya pili mfululizo, kutokana na kujirusha akidai alifanyiwa faulo.
Hata hivyo kadi hiyo haikuharibu hali ya hewa kutokana na ushindi huo, ambapo sasa Spurs wanashika nafasi ya nne.
Liverpool nao wameibuka na ushindi mwembamba baada ya kupotezwa na Tottenham katikati ya wiki, safari hii wakiwafunga Southampton.
Bao pekee la mchezo lilifungwa na Daniel Agger, na kumrejeshea furaha Brendan Rodgers, ambaye sasa timu yake inaipumulia Arsenal katika nafasi ya 11.
Manchester United waliozoea kufungwa kabla ya kukomboa mabao na hatimaye kushinda, Jumamosi hii walifanya hivyo hivyo kwa Reading.
Wakicheza ugenini, United walikuwa nyuma kwa mabao 3-2 kabla ya kusawazisha na kisha kupachika la ushindi.
Mabao ya Manchester United yalifungwa Oliveira Anderson, Wayne Rooney kwa penati na Robin Van Persie mawili.
Reading waliwafurahisha washabiki wao kwa mabao kutoka kwa Hal Robson-Kanu, Adam Le Fondre na Sean Morrison.
Mabingwa wa England, Manchester City wameendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo tangu kuanza msimu huu, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Everton.
Walikuwa Everton walioanza kuliona lango la wafalme hao wa soka kupitia kwa Marouane Fellaini, lakini Carlos Tevez alifunga kusawazisha mambo baada ya kufunga penati kutokana na Fellaini kumwangusha Edin Dzeko eneo la penati.
Queens Park Rangers (QPR) walio chini ya kocha mpya, Harry Redknapp wanaendelea kutafuta ushindi wa kwanza wa msimu bila mafanikio.
Hata hivyo, baada ya kumfuta kazi Mark Hughes ‘Sparky’, QPR wanaonekana sasa kutengeneza nafasi zaidi, kilichobaki ni kuzigeuza kuwa mabao.
Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa nyumbani kwa Redknapp aliyeshuhudia timu yake ikifungwa dakika ya nane, lakini wakakomboa bao dakika 10 baadaye.
Bosi wa Villa, Paul Lambert anaelekea kupoza tetesi za kwamba nyota aliyesajiliwa kwa fedha nyingi, Darren Bent anaondoka, kwani alimweka kwenye orodha ya wachezaji wa akiba. Mechi iliyopita alimwengua kabisa kikosini na timu ikashinda, ndipo maswali mengi yakaanza juu ya hatima ya mshambuliaji huyo. Lambert anasisitiza anao wachezaji 20 na kila mmoja ana nafasi sawa.
West Bromwich walioanza ligi vizuri wanaelekea kuanza kuporomoka taratibu, baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo.
Wamepoteza fursa ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Stoke City waliofunga dakika ya tano ya nyongeza baada ya 90 za kawaida kumalizika.
Comments
Loading…