*Liverpool waoga kichapo kwa Newcastle
Chelsea wameendeleza rekodi ya kutofungwa baada ya kuwachapa QPR 2-1, Arsenal wakavuna pointi tatu na mabao matatu bila majibu kwa Burnley huku Liverpool wakipoteza mechi.
Chelsea sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi nne, baada ya kufikisha 26 katika michezo 10, wakiwa mbele ya Southampton. Diego Costa alirejea dimbani baada ya kukosekana katika mechi nne zilizopita, lakini hakufunga bao.
QPR walicheza vyema na kuwabana wenyeji, kwani hadi dakika ya 74 mabao yalikuwa 1-1, Chelsea wakaja kubahatika kwa bao la penati la Eden Hazard dakika moja baadaye na kutoka na ushindi. Bao jingine lilifungwa na Oscar wakati la QPR lilifungwa na Charlie Austin.
Kocha Jose Mourinho amesema hakufurahia ushindi huo akisema timu yake hawakucheza vizuri, tofauti na alivyotarajia. Kocha wa QPR, Harry Redknapp alisononeshwa na penati iliyotolewa, akisema haikuwa haki.
Katika mechi nyingine Arsenal wamewafurahisha washabiki wao kwa kuwatandika Burnley 3-0 kwa mabao mawili ya Alexis Sanchez ambaye kwa msimu huu amefikisha 10 wakati furaha nyingine ilikuwa kwa beki kinda Calum Chambers aliyefunga bao lake la kwanza tangu aanze kuchezea timu ya wakubwa.
Theo Walcott alicheza kwa mara ya kwanza tangu alipoumia Januari, akichukua nafasi ya Alex Oxlade-Chamberlain dakika 10 kabla ya mechi kumalizika na Arsene Wenger anasema alivyocheza ni dhahiri atarudi kwenye hali yake ya kawaida mapema.
Newcastle wameendelea kufufuka ambapo wamefanikiwa kuwalaza Liverpool 1-0, hali inayozidi kumfedhehesha kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers na kumpa ahueni kubwa yule wa Magpies, Alan Pardew.
Bao pekee la mchezo lilifungwa na Perez Guiterez katika dakika ya 73, ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo wakati Liverpool wamefikisha mechi mbili bila ya kufunga hata bao moja. Watu walikuwa wakimwangalia Mario Balotelli awe mkombozi wa Liver, lakini sasa amefikisha mechi nane pasipo kuzifumania nyavu.
Washabiki wa Newcastle waliokuwa wakitaka kocha wao afukuzwe jana walijitokeza na bango lililokuwa na maandishi yanayomaanisha kuwa Pardew amerejea kutoka kwa wafu, licha ya kwamba wapinzani wao walitawala mechi kwa asilimia zaidi ya 60.
Katika mchezo mwingineEverton walikwenda suluhu na Swansea, Hull wakakubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Southampton, Leicester nao wakaoga 1-0 kwa West Bromwich Albion wakati Stoke walitoshana nguvu 2-2 nma West Ham.
Leo ni mechi ya watani wa jadi na mahasimu wa Jiji la Manchester, kwani Manchester United watapepetana na Man City kwenye dimba la Etihad katika moja ya mechi kubwa za msimu huu.
Comments
Loading…