United sasa wamtaka Fellaini
Suarez asema aachwe aondoke
Pilikapilika za usajili zimeendelea, ambapo klabu ya Barcelona ya Hispania imetuma dau la kutaka kumsajili beki wa kati wa Chelsea, David Luiz.
Barca wanaofundishwa Gerardo Martino ‘Tata’ wamesema wanataka kuimarisha safu yao ya ulinzi kwa kumsajili Mbrazili huyo.
Luiz aliyechezea Chelsea mechi zaidi ya 100 alinunuliwa mwaka 2011 kutoka Benfica ya Ureno kwa pauni milioni 21, ambapo mabingwa hao wa Hispania wamekuwa wakimuwania Luiz kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kama ambavyo klabu nyingine zinawakatalia nyota wao, Chelsea wanaofundishwa na Mreno Jose Mourinho, wamesema kwamba mchezaji huyo hauzwi.
Inadaiwa kwamba Barca wamejiandaa kutoa fedha na wala si kumbadilisha na mchezaji mwingine kama ilivyodhaniwa awali.
Jitihada za Barca zinakuja wakati beki veterani wa kati, Carles Puyol (35) akiwa na matatizo ya goti msimu uliopita, ambapo alifanyiwa upasuaji.
Walinzi wengine wa klabu hiyo, Gerard Pique, Adriano Correia na Javier Mascherano nao pia ama waliumia au kuadhibiwa kutocheza wakati wa ligi hiyo.
Beki wa kati wa Paris St-Germain, Thiago Silva alikuwa pia akihusishwa na kutua Nou Camp, lakini Mbrazili huyo tayari amesaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Ufaransa.
Bayern Munich pia walihusishwa kutaka kumsajili Luiz, ambaye alicheza dakika 30 tu katika mechi dhidi ya Inter Milan wiki iliyopita na ameondoshwa kwenye kikosi cha kupambana na Real Madrid jijini Miami.
MANCHESTER UNITED WAMTAKA FELLAINI
Katika tukio jingine, Kocha wa Manchester United, David Moyes aliyekuwa Everton kwa miaka 11 iliyopita hadi msimu uliopita, amepanga kuibomoa klabu yake hiyo ya zamani.
Moyes anasemwa kujiandaa kupeleka ofa ya kumchukua Mbelgiji mrefu na mwenye nguvu, Marouane Fellaini.
Moyes ana wakati mgumu katika jitihada za usajili, ambapo bado hajasajili nyota yeyote, jitihada zake za kumchukua Cesc Fabregas wa Barca zikigonga mwamba zaidi ya mara moja.
SUAREZ: NIACHENI NIONDOKE LIVERPOOL
Naye mchezaji wa Liverpool, Luis Suarez ameiambia klabu yake anataka kuondoka Anfield, kwa sababu ndivyo walimwahidi tangu mwaka jana.
Kwamba makubaliano ilikuwa aondoke kama Liverpool haingefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo anasema alijitahidi kucheza kwa nguvu zote, lakini sasa wanamgeuka.
Anatakiwa na Arsenal ambao wameshatoa ofa mara mbili, ya mwisho ikiwa pauni 40,000,001 ikilenga kutengua kipengele kinachomweka Liverpool, lakini kocha Brendan Rodgers anashikia kwamba hauzwi, na hata akiuzwa si chini ya pauni milioni 50.
Suarez (26) anafikiria kuchukua hatua za kisheria, lakini kwanza awasilishe rasmi ombi la kuondoka kisha aende mahakamani ili kupata tafsiri halisi ya kipengele na kuachiwa ajiunge na klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Comments
Loading…