*Bayern, PSG kilion
Robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) zimekuja na matokeo ya ushindi mzuri kwa timu mbili, zikiziwaachia kazi ngumu wapinzani wao kwenye mechi za mkondo wa pili.
Wakati Barcelona walitumia uzoefu wao kuwapiga Paris Saint-Germain (PSG) 3-1, Porto wa Ureno walishangaza kwa kuwapiga mabingwa wa zamani wa Ulaya, Bayern Munich idadi hiyo hiyo ya mabao.
Barcelona waliokuwa ugenini wamejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia nusu fainali ya michuano hii kwa msimu wa saba na mabao yao yalitokana na moja la Neymar mapema dakikaya 18 na mawili ya Luis Suarez dakikaya 67 na 79.
PSG hawakuamini kichapo hicho na ilikuwa mechi ya kwanza kupoteza wakiwa nyumbani msimu huu na walimkosa Zlatan Ibrahimovic aliyekuwa nje kwa kadi nyekundu aliyopewa walipocheza na Chelsea kwenye hatua iliyopita.
Suarez sasa ameanza kung’ara na amefunga mabao 13 katika mechi 15, na bila Ibrahimovic PSG walionekana wakipata tabu dimbani. Hata bao lao lilitokana na beki wa Barcelona, Jeremy Mathieu kujifunga.
Kabla ya bao hilo lililotokana na mkwaju wa yadi 20 wa Gregory van der Wiel drive kumkwaruza na kumshinda kipa wake, hali ilikuwa ngumu kwa PSG waliompoteza Thiago Silva aliyeumia na huenda wangefungwa zaidi.
Katika mechi nyingine, Porto waliwanyong’onyeza washabiki wa Bayern Munich kwa kuwatandika mabao 3-1 na kuwaacha vijana hao wa Pep Guardiola warudi nyumbani kujiuliza na kujipanga vyema kwa mechi ya mkondo wa pili.
Wareno hao walianza kuonesha cheche baada ya Ricardo Quaresma kufunga penati iliyotokana na kipa Manuel Neuer kumchezea vibaya Jackson Martinez. Alipata kadi ya njano na kushindwa kuzuia penati husika dakika ya tatu tu ya mchezo.
Alikuwa ni winga Quaresma tena aliyewapelekesha puta Bayern kwa kumpokonya mpira Dante, kabla ya kuchomoka na kutia wavuni mpira taratibu na kwa kujiamini dakika saba baadaye.
Thiago Alcantara alipunguza kasi ya Porto kwa kufunga bao kunako dakika ya 28 na timu zikaenda kupumzika hali ikiwa hivyo, kabla ya dakika ya 65 kushuhudia Martinez akifunga bao la tatu.
Porto walitwaa ubingwa wakiwa na kocha wa sasa wa Chelsea, Jose Mourinho mwaka 2004 na ushindi wa Jumatano hii umetokana na kufanya kazi kwa bidii na kujituma huku wakitia shinikizo kwenye lango la Wajerumani ambao hawakujilinda vyema.
Comments
Loading…